05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Wanawake Wasiofaa Kuchumbiwa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

05: Wanawake Wasiofaa Kuchumbiwa:

 

1-  Wanawake Walioharamishwa kuwaoa milele au kwa muda:

 

Kwa kuwa posa ni utangulizi wa ndoa, na madhali ndoa imezuilika, basi na posa pia inazuilika.  Wanawake walioharamishwa kuwaoa wametajwa nyuma.

 

Ni vizuri kudokeza hapa kwamba ni halali kumposa mwanamke wa kikafiri (mmajusi na mfano wake) ili mtu amwoe atakaposilimu.  [Nihaayatul Muhtaaj]

 

2-  Mwanamke aliye kwenye eda (katika kipindi cha eda tu):

 

Huyu ingawa anaingia kwenye ujumla wa wanawake walioharamika kuolewa kwa muda -kama ilivyotangulia- ila tu yeye ana ahkaam na changanuo maalumu.  Kadhalika, hukmu ya kumchumbia mwenye eda inatofautiana kwa mujibu wa hali yake.

 

Mwenye Eda Anakuwa Na Hali Tofauti:

 

(a)  Eda ya aliyefiwa na mumewe:

 

Huyu, mwanaume haruhusiwi kumweleza wazi wazi nia yake ya kumwoa.  Kama kumwambia:  “Ninataka kukuoa”, au “Eda yako ikimalizika nitakuoa”.  Itifaki ya Fuqahaa imeharamisha hili.  Pamoja na hivyo, inajuzu kumdokezea hamu ya kumwoa kwa tamshi la kufumbia (lisilo wazi) kama “Huenda nikakutaka”, au “Nani atapata mfano wako?”.  Allaah Amesema:

 

"وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا عَرَّضْتُم بِهِ مِنْ خِطْبَةِ النِّسَاءِ أَوْ أَكْنَنتُمْ فِي أَنفُسِكُمْ ۚ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ سَتَذْكُرُونَهُنَّ وَلَـٰكِن لَّا تُوَاعِدُوهُنَّ سِرًّا إِلَّا أَن تَقُولُوا قَوْلًا مَّعْرُوفًا"

 

“Wala si dhambi juu yenu katika ambayo mmedokezea ya kuposa wanawake hao au mliyoficha katika nafsi zenu. Allaah Anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka lakini msifunge nao ahadi kisiri isipokuwa mseme kauli inayoeleweka kawaida”.  [Al-Baqarah: 235] 

 

Sababu ni kuwa ikiwa mwenye nia ya kumwoa mwanamke huyu atamwelezea wazi wazi, basi utashi wake utapata nguvu, na mwanamke huyo anaweza kuongopa kuhusu muda wa kumalizika eda yake.

 

Sheikh wa Uislamu amesema (32/8):  “Na mwenye kufanya hivyo (yaani kumweleza wazi nia ya kumwoa), huyo atastahiki adhabu ya kumkomesha yeye na walio mfano wake.  Kadhalika, hatoozeshwa mwanamke huyo kama adhabu kwake”.

 

Ninasema:  “Kati ya picha za kumfumbia, ni ile iliyogusiwa na Ibn ‘Abbaas wakati alipoifasiri Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا عَرَّضْتُم بِهِ مِنْ خِطْبَةِ النِّسَاءِ"

 

“Wala si dhambi juu yenu katika ambayo mmedokezea ya kuposa wanawake hao”.  [Al-Baqarah: 235]

 

Akasema:  Atasema kumwambia (kwa mfano):  “Mimi nataka kuoa, na ningependa zaidi Allaah Anifanyie wepesi kumpata mwanamke mwema”.

 

(b)  Eda ya talaka rejea (ya kwanza na ya pili):

 

 Huyu haijuzu kumchumbia posa ya wazi wala ya kufumbia wakati wa eda yake, kwa sababu mumewe bado ana nafasi ya kumrejea.  Allaah Ta’aalaa Amemwita mwenye eda ya talaka rejea mke pale Aliposema:

 

"وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ إِذَا تَرَاضَوْا بَيْنَهُم بِالْمَعْرُوفِ"

 

“Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao; basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali) ikiwa wameridhiana baina yao kwa mujibu wa ada”.  [Al-Baqarah:  232]

 

Ndoa ya mwanamke huyu bado ipo, na kumchumbia posa isiyo wazi (ya kufumbia) kunazingatiwa kama ni kuharibu mahusiano yake na mumewe.  Na kwa vile talaka imemkwaza na kumsababishia taharuki, anaweza kuongopa kuhusu muda wa kumalizika eda yake ili kulipiza kisasi.  Haya ndiyo waliyokubaliana Fuqahaa kwa sauti moja.

 

(c)  Mwenye eda ya talaka tatu:

 

Kwa itifaki ya ‘Ulamaa, haijuzu kumchumbia mwanamke huyu posa ya wazi.  Ama posa ya kufumbia, ‘Ulamaa wamekhitalifiana katika kauli mbili:

 

Kauli ya kwanza:  Inajuzu posa ya kufumbia.  Ni madhehebu ya Jumhuwr; wanachuoni wa Kimaalik, Kishaafi’y na Kihanbali.  Dalili zao ni:

 

1-  Ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا عَرَّضْتُم بِهِ مِنْ خِطْبَةِ النِّسَاءِ"

 

“Wala si dhambi juu yenu katika ambayo mmedokezea (mmefumbia) ya kuposa wanawake”.  [Al-Baqarah: 235]

 

2-  Hadiyth ya Faatwimah bint Qays ambaye mumewe alipompa talaka tatu, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

 

" اعْتَدِّي عِنْدَ ابْنِ أُمِّ مَكْتُومٍ فَإِنَّهُ رَجُلٌ أَعْمَى تَضَعِينَ ثِيَابَكِ عِنْدَهُ فَإِذَا حَلَلْتِ فَآذِنِينِي"

 

“Kaa eda yako kwa Ibn Ummi Maktuwm, yeye ni kipofu, utaweza kuvua nguo zako huko kwake, na eda ukimaliza, basi nijulishe”.  [Muslim (1480)]

 

An-Nawawiy kasema:  “Hadiyth hii inaonyesha kwamba inajuzu kumposa aliyepewa talaka tatu kwa kauli fumbo, na hili kwetu ni sahihi”.

 

3-  Ni kwamba mwanamke huyu hawezi kurejea tena kwa mumewe, na hali yake hii ni sawa sawa na yule aliyefiwa na mumewe ambaye hawezi tena kurudi.  Hawa wote wawili wako duara moja kinyume na mwenye eda ya talaka rejea.

 

Kauli ya pili:  Haijuzu posa ya kufumbia.  Ni madhehebu ya ‘Ulamaa wa Kihanafiy.  Dalili zao ni:

 

1-  Kwamba Aayah Tukufu inayohalalisha posa ya kufumbia ilikuja kuhusiana na mwenye eda ya kufiwa na mumewe.  Hivyo haijuzu kuwahusisha wanawake wengine wenye eda tofauti na hiyo.

 

2-  Mume aliyetaliki anaweza kupata adha kutokana na posa fumbo hii kwa mkewe, na kuzalisha uadui.

 

Ninasema:  “Kauli yenye nguvu ni kwamba inajuzu kumposa kwa kufumbia kutokana na Hadiyth ya Faatwimah bint Qays.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Faida Mbili:

 

1-  Ikiwa mtu atamchumbia mwanamke posa ya wazi wakati wa eda yake kisha akamwoa baada ya kumalizika eda, mtu huyu atapata madhambi lakini ndoa itakuwa ni sahihi.  Na kama atamwoa wakati wa eda yake, hapa ndoa itakuwa ni batili.

 

2-  Endapo mtu atamwoa mwanamke wakati wa eda yake, hawa ni lazima watenganishwe, na mwanamke atakamilisha eda ya mume wa kwanza.  Kisha atakaa eda ya mume wa pili kama aliwahi kumuingilia, na mahari atapewa kama alikuwa hajui hukumu ya  hilo, na kama anajua kwamba haijuzu kuolewa kabla ya eda kwisha, basi kiongozi wa Waislamu ana haki ya kumpa mahari hiyo au kuipeleka Baytul Maal kama adhabu adabishi (ta’aziyr).

 

Toka kwa Ibn Al-Musayyib na Sulaymaan bin Yasaar: 

 

"أَنَّ طُلَيْحَةَ الأَسَدِيَّةَ، كَانَتْ تَحْتَ رُشَيْدٍ الثَّقَفِيِّ فَطَلَّقَهَا فَنَكَحَتْ فِي عِدَّتِهَا، فَضَرَبَهَا عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ وَضَرَبَ زَوْجَهَا بِالْمِخْفَقَةِ ضَرَبَاتٍ وَفَرَّقَ بَيْنَهُمَا، ثُمَّ قَالَ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ: أَيُّمَا امْرَأَةٍ نَكَحَتْ فِي عِدَّتِهَا فَإِنْ كَانَ زَوْجُهَا الَّذِي تَزَوَّجَهَا لَمْ يَدْخُلْ بِهَا فُرِّقَ بَيْنَهُمَا ثُمَّ اعْتَدَّتْ بَقِيَّةَ عِدَّتِهَا مِنْ زَوْجِهَا الأَوَّلِ ثُمَّ كَانَ الآخَرُ خَاطِبًا مِنَ الْخُطَّابِ، وَإِنْ كَانَ دَخَلَ بِهَا فُرِّقَ بَيْنَهُمَا ثُمَّ اعْتَدَّتْ بَقِيَّةَ عِدَّتِهَا مِنَ الأَوَّلِ ثُمَّ اعْتَدَّتْ مِنَ الآخَرِ ثُمَّ لاَ يَجْتَمِعَانِ أَبَدًا"

 

“Kwamba Tulayha Al-Asadiyyah, alikuwa mke wa Rushayd Ath-Thaqafiy ambaye alimwacha talaka tatu.  Tulayha akaolewa wakati wa kipindi cha eda.  ‘Umar bin Al-Khattwwaab akampiga Tulayha, na akamchapa mumewe (mpya) fimbo kadhaa kisha akawaachanisha.  Halafu ‘Umar akasema:  Mwanamke yeyote atakayeolewa wakati eda yake bado haijamalizika na mumewe akawa hajamuingilia, basi lazima waachanishwe, kisha atamalizia eda ya mume wake wa awali, na mume wa pili atabaki na nafasi ya kuweza kumposa na kumwoa tena.  Na kama atakuwa amemuingilia, basi wataachanishwa, kisha atamalizia eda iliyosalia ya mumewe wa awali.   Akimaliza hiyo, atakaa eda ya mume wa pili ambaye hatoruhusiwa kumuoa milele”.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bayhaqiy (7/441) na Abdulrazzaaq (10539)]

 

Je, Inafaa Mume Wa Pili Kumposa Na Kumwoa Tena Baada Ya Kumaliza Eda Mbili? 

 

Katika Hadiyth hii, ‘Umar amezuia asimwoe tena milele.  Maalik, Al-Layth na Al-Awzaaiy wamesema hivyo hivyo.  Ama ‘Aliyy bin Abiy Twaalib, yeye amejuzisha.  Toka kwa ‘Atwaa:  “Kwamba ‘Aliyy aliletewa kesi kama hiyo akawaachanisha, halafu akamwamuru mwanamke amalizie eda yake ya kwanza, kisha akae eda nyingine ya kando ya wa mume wa pili, na ikimalizika basi atakuwa mwenyewe na hiari; akitaka ataolewa na asipotaka basi”.  [Ni Dhwa’iyf, ina Hadiyth wenza.  Imechakatwa na Ash-Shaafi’iy katika Al-Ummu (5/233), Al-Bayhaqiy (10/441) na Abdulrazzaaq (10532)]

 

Jumhuwr wameiunga mkono kauli hii ya ‘Aliyy ambayo ndiyo yenye nguvu kwa kuwa ndio asili mbali na kwamba hukmu ya ‘Umar haina dalili.  Inawezekana alihukumu hivyo kama ni adhabu adabishi (ta’aziyr).

 

(d)  Eda inayotokana na nikaha batili au iliyovunjwa:

 

Ni kama eda ya li’aan (mume kuikataa mimba kwa kumshuhudilia Allaah) au kuritadi, au kwa mwenye kuangalia kama tumboni kuna kitu baada ya kuzini, au aliyeachishwa kutokana na kasoro, au mume kukosa nguvu za kiume na mfano wa hayo.  Jumhuwr ya ‘Ulamaa wamesema kwamba inajuzu kumchumbia kwa kufumbia kutokana na ujumuishi wa aayah tukufu, na kwa kuchukulia qiyas cha mwenye talaka tatu, na kwa vile pia mamlaka ya mume yanakuwa hayako tena.

 

 

Share