06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Kumchumbia Mwanamke Ambaye Amekwishachumbiwa Na Muislamu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

06:  Kumchumbia Mwanamke Ambaye Amekwishachumbiwa Na Muislamu:

 

Mwanaume Muislamu akimchumbia mwanamke, basi si halali kwa mwanaume mwingine kumposa. 

 

1-  Abu Hurayrah:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"ولَا يَخْطُبُ الرَّجُلُ عَلَى خِطْبَةِ أَخِيهِ حَتَّى يَنْكِحَ أَو يَتْرُكَ"

 

“Na mtu asipose juu ya posa ya nduguye mpaka aoe au aachilie”.  [Swahiyh.  Al-Bukhaariy (5143) na Muslim (1413)] 

 

2-  Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu):

 

"نَهَى النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يَبِيعَ بَعْضُكُمْ عَلَى بَيْعِ بَعْضٍ، وَلاَ يَخْطُبَ الرَّجُلُ عَلَى خِطْبَةِ أَخِيهِ، حَتَّى يَتْرُكَ الْخَاطِبُ قَبْلَهُ، أَوْ يَأْذَنَ لَهُ الْخَاطِبُ‏"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuuziana kitu ambacho kimekwishauzwa, au mtu kuposa juu ya posa ya nduguye mpaka mposaji aliyetangulia avunje posa au mposaji amruhusu”.  [Swahiyh.  Al-Bukhaariy (5142) na Muslim (1412)]

 

3-  ‘Uqbah bin ‘Aamir:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"الْمُؤْمِنُ أَخُو الْمُؤْمِنِ فَلاَ يَحِلُّ لِلْمُؤْمِنِ أَنْ يَبْتَاعَ عَلَى بَيْعِ أَخِيهِ وَلاَ يَخْطُبَ عَلَى خِطْبَةِ أَخِيهِ حَتَّى يَذَرَ‏"

“Muumini ni ndugu ya muumini, hivyo basi, haifai muumini kununua kitu alichokwisha nunua nduguye, au kuposa juu ya posa ya nduguye mpaka aiachie posa”.  [Swahiyh.  Muslim (1414)]

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba katazo hili linabeba sifa ya uharamu kwa sababu kufanya hivi kunasababisha madhara kwa mhusika, kunajenga uadui, chuki, na adha, lakini pia ni uchupiaji wa mipaka ya haki ya Muislamu.

 

 

Share