07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Ni Upi Mpaka Wa Posa Ambayo Ni Haramu Kuiposea?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

07:  Ni Upi Mpaka Wa Posa Ambayo Ni Haramu Kuiposea?

 

‘Ulamaa kwa sauti moja wameharamisha posa juu ya posa ya Muislamu ikiwa mposaji amejibiwa jibu la wazi la kukubaliwa posa yake, lakini pia awe hajatoa idhini kwa mwingine kuposa, na posa awe hajaiachilia, isitoshe mposaji wa pili ajue kwamba kuna mposaji aliyemtangulia ambaye posa yake imekubaliwa.

 

‘Ulamaa wa Kihanbali hawakushurutisha kukubaliwa posa kwa tamko wazi kuwe ndio kigezo cha kuharamisha posa juu ya posa ya mwingine.  Wamesema hata kukubaliwa kwa fumbo ni kigezo cha cha kuharamisha posa juu ya posa ya mwingine.  Huenda wamefarijika na Hadiyth isemayo:

"وَإِذْنُهَا صُمَاتُهَا"

 

“Kunyamaza kwake ndio kukubali kwake”.  [Hadiyth Swahiyh]

 

Hivyo kunyamaza kwake kunakuwa ni dalili ya kukubali kwake!

 

Ama ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy, Kihanafiy na Kimaalik, wao wanaona kwamba kujibiwa mposaji kwa jibu la fumbo hakuharamishi mwingine kuposa juu ya posa yake.  Wameitolea dalili hoja yao hiyo kwa Hadiyth ya Faatwimah bint Qays wakati alipomweleza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Abu Jahm na Mu’aawiyah wamemposa, na Rasuli akamwamuru aolewe na Usaamah.  Wanasema kwamba Rasuli hakukemea kwa nini wachumbie posa juu ya posa, bali yeye mwenyewe akamposea kwa Usaamah.

 

Na ili posa iwe haramu juu ya posa nyingine, ‘Ulamaa wa Kimaalik wameshurutisha ridhaa ya mwanamke aliyeposwa au walii wake, na mposaji asiwe mtu asiyejali madhambi.

 

Ninasema:  “Ninaloona mimi ni kuwa kwa kule tu Muislamu kupeleka posa kwa mwanamke, kunaifanya posa ya mwingine kuwa haramu kama atajua kuna posa iliyomtangulia.  Haitojuzu kupeleka posa wakati huo isipokuwa tu kama atajua kwamba mposaji wa awali amekataliwa, au ameruhusu mwingine apose, au akafuta posa yake.  Haya ni madhehebu ya Abu Muhammad bin Hazm, na chaguo la Ash-Shawkaaniy (Allaah Awarehemu wote).  Msimamo huu unatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Umar kuhusiana na kisa cha ‘Umar bin Al-Khattwaab kumnadia binti yake Hafswah kwa ‘Uthmaan na Abu Bakr, na kisha Abu Bakr kuja kumweleza ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) akimwambia:  “Hakika hakuna kilichonizuia kukujibu kuhusiana na uliyonidokezea (kuhusu Hafswah) isipokuwa tu mimi nilikwisha jua kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemtaja. Nisingeliweza kutoboa siri ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Na lau Rasuli asingelimwoa, basi mimi ningelimkubali”.  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (5145)]

 

Na hapa tunaona kwamba Abu Bakr kwa kule tu kujua kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ana nia ya kumposa Hafswah, hakuthubutu kumposa au hata kumjibu baba yake ‘Umar, akasubiri Rasuli kama atatimiza azma yake au la.  Basi itakuwaje kwa yule ambaye ameshawasilisha posa yake?  Na vipi kwa ambaye posa yake isharidhiwa na kukubaliwa?

 

Ama Hadiyth ya Faatwimah bint Qays, Hadiyth hii haikinzani na Hadiyth nyingine Swahiyh zinazokataza posa juu ya posa.  Kwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwelekeza baada ya kumshauri huku maamuzi yakiwa bado mkononi mwake. 

 

Na kama itaulizwa:  Kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakujua kwamba bibi huyu (Faatwimah) ameposwa na zaidi ya mtu mmoja?  Na vipi alimkubalia baada ya kukataza mtu kuposa juu ya posa ya nduguye?

 

Swali hili linajibiwa hivi:  Kuna uwezekano wa kuwa mposaji wa pili alimposa bila kujua kwamba kuna mposaji wa kwanza aliyemtangulia, au posa mbili zilikuja wakati mmoja au muda unaokaribiana.  Kadhalika, inawezekana yeye mwenyewe alimkataa mposaji au walii wake, lakini tu yeye akataka ushauri wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na kila aliyemposa.

 

Tunakumbushia hapa tena kwamba hikma ya kukataza posa juu ya posa, ni kuepusha chuki, mipasuko na uadui kati ya ndugu Waislamu.  Ni vizuri kuepukana na hili isipokuwa tu kama mposaji wa awali ataruhusu, au ataiachia posa, au akakataliwa na mwanamke au walii wake, hapo hakuna tatizo.  Allaah Ndiye Mjuzi wa yote.

 

 

Share