13-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Je, Mwanaume Anaruhusiwa Kumwangalia Kikaguzi Mwanamke Aliyekusudia Kumposa?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا
Posa Na Hukumu Zake
13: Je, Mwanaume Anaruhusiwa Kumwangalia Kikaguzi Mwanamke Aliyekusudia Kumposa?:
Jumhuwr ya Wanazuoni wamekubaliana kwamba mwanaume anayekusudia kumwoa mwanamke anaruhusiwa kisharia kumwangalia. Na asili ya hili ni:
1- Neno Lake Ta’aalaa:
"لَّا يَحِلُّ لَكَ النِّسَاءُ مِن بَعْدُ وَلَا أَن تَبَدَّلَ بِهِنَّ مِنْ أَزْوَاجٍ وَلَوْ أَعْجَبَكَ حُسْنُهُنَّ"
“Si halali kwako wanawake wengine baada ya hao na wala kuwabadilisha kwa wake wengine japo kama uzuri wao umekupendeza”. [Al-Ahzaab: 52]
Uzuri hauwezi kujulikana ila kwa kumwangalia.
2- Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema:
"كُنْتُ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَتَاهُ رَجُلٌ فَأَخْبَرَه أَنَّه تَزَوَّجَ امْرَأَةً من الأَنْصَارِ، فَقَالَ له رَسُوْلُ الله: أَنَظَرْتَ إِلَيْهَا؟ قَالَ: لا، قَالَ: اذْهَبْ فَانْظُرْ إِلَيْهَا فَإِنَّ فِي أَعْيُنِ الْأَنْصَارِ شَيْئًا"
“Nilikuwa kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha mtu mmoja akamjia na kumweleza kwamba amemwoa mwanamke wa Kianswaar. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: Je, umemwangalia? Akasema: Hapana. Akamwambia: Nenda ukamwangalie, kwani hakika katika macho ya Answaar kuna ila fulani”. [Hadiyth Swahiyh. Muslim (1424) na An-Nasaaiy (6/69)]
3- Hadiyth ya Jaabir aliyesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
“إذا خَطَبَ أحدُكمُ المرأةَ فَقَدرَ أَنْ يَرَى مِنْهَا بَعْضَ ما يَدْعُوهُ إِلَيْهَا فَلِيَفْعَلْ"
“Mmoja wenu akimposa mwanamke na akaweza kumwona baadhi ya sehemu zitakazomshawishi amwoe, basi na afanye”. [Hadiyth Hasan. Abu Daawuwd (2082), Ahmad (3/360), Al-Haakim (2/165) na Al-Bayhaqiy (7/84)]
4- Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad:
"أَنَّ امْرَأَةً جَاءَتْ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، جِئْتُ لأَهَبَ نَفْسِي لَكَ. فَنَظَرَ إِلَيْهَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَصَعَّدَ النَّظَرَ إِلَيْهَا وَصَوَّبَهُ ثُمَّ طَأْطَأَ رَأْسَهُ"
“Kwamba mwanamke mmoja alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Nimekuja ili kujitoa mwenyewe kwako (unioe bila mahari). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamtazama, kisha akamwangalia juu hadi chini halafu akainamisha kichwa chake chini”. [Swahiyh. Al-Bukhaariy (5126) na Muslim (1425)]
5- Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia:
"أُرِيْتُكِ فِي الْمَنَامِ يَجِيءُ بِكِ الْمَلَكُ فِي سَرَقَةٍ مِنْ حَرِيرٍ، فَقَالَ لِي: هَذِهِ امْرَأَتُكَ. فَكَشَفْتُ عَنْ وَجْهِكِ الثَّوْبَ، فَإِذَا أَنْتِ هِيَ فَقُلْتُ: إِنْ يَكُ هَذَا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ يُمْضِهِ".
“Nilionyeshwa wewe kwenye njozi (kabla ya kukuoa). Nilimwona Malaika anakuleta ndani ya kitambaa cha hariri akaniambia: Huyu ni mkeo, nami nikakufunua uso, tahamaki nikakuona ni wewe. Nikasema: Ikiwa hili linatoka kwa Allaah, basi Atalipitisha”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (5125) na Muslim]
6- Al-Mughiyrah bin Shu’ubah alimchumbia mwanamke, na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"انْظُرْ إِلَيْهَا فَإِنَّهُ أَحْرَى أَنْ يُؤْدَمَ بَيْنَكُمَا "
“Mwangalie, kwani hakika hilo lina nguvu kuleta zaidi matangamano mema kati yenu wawili”. [Al-Albaaniy kasema ni swahiyh. Imechakatwa na At-Tirmidhiy (3087), na iko katika Swahiyh At-Tirmidhiy (934). Ad-Daaraqutwniy ameitia kasoro, lakini hata hivyo ina Hadiyth wenza]
Hikma ya kumwangalia mwanamke wa kumposa ni mtu kujiridhisha mwenyewe kutakakomsukuma kumwoa, na hili bila shaka litakwenda kudumisha maisha ya ndoa kati ya wawili hao. Na hali inaweza kuwa kinyume ikiwa hakumwona hadi ndoa ikafungwa. Anaweza mwanaume kushtukizwa na asiyoyapenda, na matokeo yake ni maisha ya ukorofi.
Ninasema: “Hukmu ya mtu kumwangalia mwanamke aliyemposa kwa Wanachuoni inazungukia kati ya kuwa ni mubaah na kuwa jambo lenye kupendeza ambalo liko karibu zaidi na dalili zilizopita. Hakuna yeyote aliyesema kwamba ni lazima kumwangalia -kwa mujibu wa ninavyojua- mbali na kuwa si sharti ya kuswihi kwa ndoa. Kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu amesema: “Ndoa inaswihi hata kama hakumwona”.