14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Mipaka Ya Kumwangalia

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

14:   Mipaka Ya Kumwangalia:

 

Inajuzu kumwangalia uso na vitanga viwili vya mikono.  Ni kauli isiyo na mvutano kati ya ‘Ulamaa waliojuzisha hili.  Lakini walichokhitilafiana ni sehemu ambazo inajuzu kuziangalia zaidi ya uso na vitanga.  Katika hili, kuna kauli nne:

 

Kauli ya kwanza: 

 

Haangaliwi isipokuwa uso na mikono tu.  Ni kauli ya Jumhuwr wanaosema kwamba uso ndio sehemu inayoonyesha uzuri na ujamala wa mwanamke, na vitanga ndivyo vinavyoashiria urutuba wa mwili wake.  Lakini pia, viungo hivi viwili ndivyo ambavyo kikawaida huonekana, na hivyo basi, kuonekana vingine zaidi yake hairuhusiwi.

 

Kauli ya pili: 

 

Ni halali kumwangalia viungo ambavyo aghlabu huonekana kama shingo, mikono miwili na miguu miwili.  Hii ni kauli ya Mahanbali.  Dalili yao wanasema kwamba wakati Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliporuhusu mwanamke kuangaliwa bila yeye kujua, ina maana aliruhusu kumwangalia zile sehemu ambazo kikawaida huonekana.  Isitoshe, kwa vile sharia imeruhusu mwanamke huyo atazamwe, hapo mwanaume ana ruhusa ya kumwangalia sawa na wanavyomwangalia maharimu zake.

 

Kauli ya tatu:

 

Anaruhusika kumwangalia sehemu yoyote aitakayo isipokuwa utupu.  Haya ni madhehebu ya Al-Awzaaiy.

 

Kauli ya nne: 

 

Anaruhusika kumwangalia mwili wote.  Ni madhehebu ya Daawuwd, Ibn Hazm na riwaayah ya tatu toka kwa Ahmad.  Ni kwa ubayana wa neno la Rasuli:

 

"انْظُرْ إِلَيْهَا"

“Mwangalie”.

 

Ninasema:  “Lenye nguvu ambalo nafsi inatulia kwalo ni kwamba mtu anapokwenda kumposa mwanamke, basi mwanamke huyo atamwonyesha uso wake na viganja viwili kama walivyosema Jumhuwr.  Ama ikiwa mposaji huyo atajificha, basi atamwangalia sehemu zile ambazo zitamvutia na kumfanya amwoe.  Hatakikani kumtaka amfunulie mwili wake zaidi ya uso na viganja.  Lakini pamoja na hayo, ana haki ya kuulizia viungo vingine zaidi ya hivyo viwili kutoka kwa mama ya mwanamke au dada yake, au akajificha ili kuona hayo ayatakayo ya ziada.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.  

 

 

Share