15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Je, Ni Sharti Mwanamke Anayeposwa Atakwe Idhini Ya Kuangaliwa Na Ajue Hilo?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا
Posa Na Hukumu Zake
15: Je, Ni Sharti Mwanamke Anayeposwa Atakwe Idhini Ya Kuangaliwa Na Ajue Hilo?
Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba si sharti mwanamke ajue au atakwe idhini yeye au walii wake, inatosha tu kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameruhusu hilo. Ni kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Jaabir iliyotangulia kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا خَطَبَ أَحَدُكُمُ الْمَرْأَةَ فَإِنِ اسْتَطَاعَ أَنْ يَنْظُرَ إِلَى مَا يَدْعُوهُ إِلَى نِكَاحِهَا فَلْيَفْعَلْ". قَالَ: فَخَطَبْتُ جَارِيَةً فَكُنْتُ أَتَخَبَّأُ لَهَا حَتَّى رَأَيْتُ مِنْهَا مَا دَعَانِي إِلَى نِكَاحِهَا وَتَزَوُّجِهَا فَتَزَوَّجْتُهَا"
“Akimposa mmoja wenu mwanamke na akaweza kumwangalia pale ambapo patamshawishi kumwoa, basi na afanye. Akasema: Nikamposa msichana, na nikawa najificha kumwangalia, mpaka nikaona kilichonivuta kumwoa, na nikamwoa”. [Hadiyth Hasan. Abu Daawuwd (2082), Ahmad (3/360), Al-Haakim (2/165) na Al-Bayhaqiy (7/84)]
Kadhalika, imesimuliwa kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا خَطَبَ أَحَدُكُمُ امْرَأَةً فلا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ يَنْظُرَ إِلَيْهَا إِذَا كَانَ إِنَّمَا يَنْظُرُ إِلَيْهَا لِخِطْبَتِهَا وإِنْ كَانَتْ لا تَعْلَمُ"
“Akiposa mmoja wenu mwanamke, basi hakuna ubaya kama atamwangalia, lakini kuwe kumwangalia huko ni kwa ajili ya kumwoa tu na si vinginevyo, hata kama mwenyewe hajui”.
Bali hata baadhi ya Fuqahaa wamesema kwamba mwanamke kutojua kwamba anaangaliwa inakuwa ni bora zaidi, kwa kuwa akijua, anaweza kujitengeneza akaonekana kinyume na alivyo na mwanamume akahadaika na uzuri bandia.
Lakini wanachuoni wa Kimaalik wanaona kwamba ni lazima mwanamke ajulishwe au walii wake ili kuziba mwanya kwa mafasiki kuweza kuangalia wanawake kwa malengo yao mengine wakidai kwamba wao ni waposaji.
Ninasema: “Kauli ya Jumhuwr iko karibu zaidi na maneno ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Halafu, ikiwa mwanaume ataweza kumwangalia kabla ya kumposa, itakuwa vyema zaidi, kwa kuwa posa yake inaweza kukataliwa, na hapo akaumia na kujeruhika kisaikolojia”.