16-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake: Je, Mwanaume Anaruhusiwa Kumwangalia Kwa Matamanio Au Kwa Hisia Ya Ladha?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

16:   Je, Mwanaume Anaruhusiwa Kumwangalia Kwa Matamanio Au Kwa Hisia Ya Ladha? 

 

Ili kumwangalia mwanamke kuruhusike, ‘Ulamaa wa Kihanbali wameshurutisha kuwepo usalama wa fitnah.  Hivyo basi kumwangalia mwanamke kwa hisia ya ladha na matamanio ni haramu.

 

Ama Jumhuwr, wao hawajashurutisha hilo, bali wanasema kwamba mwanamume anaruhusika kumwangalia kwa lengo la kumwoa hata kama atahofia kumtamani au kuwepo fitnah kutokana na mambo mawili:

 

1-  Kwamba Hadiyth zilizogusia uhalali wa kumwangalia mwanamke kwa ajili ya kumwoa, hazikuainisha kumwangalia kwa kumtamani au bila kumtamani, bali zimeuachia mlango wazi.

 

2-  Maslaha yanayopatikana kwa hilo ni makubwa zaidi kuliko madhara.

 

Kumwangalia Mchumba Zaidi Ya Mara Moja:

 

Mposaji ana haki ya kumwangalia anayemposa kwa zaidi ya mara moja ili kutaamuli mazuri zaidi aliyonayo na kupata picha wazi zaidi ya alivyo, ili asije kujuta baada ya kumwoa.  Anaweza kufanya hivyo hata bila ya idhini.  Lengo mara nyingi halipatikani kwa mtizamo wa mara moja.  Lakini pamoja na hivyo, anatakikana ajidhibiti vizuri kwa kiasi cha haja ya kumwezesha kupata uhakika tosha wa kumkubali.  Ikiwa mara moja au zaidi itatosha kujikinaisha na kujiridhisha, basi zaidi ya hapo ni haramu, na mwanamke huyo atarudi kuwa ajnabiyya (mwanamke wa kando) kwake mpaka atakapofunga naye ndoa.

 

Ninasema:  “Kwa muktadha huu, haitakikani mwanaume kukutana mara kwa mara na mchumba wake kama inavyofanyika siku hizi.  Utamwona mvulana anamtembelea mchumba wake takriban kila siku, anakaa naye masaa mengi na kumwangalia juu chini, wakati ambapo mara za mwanzo alikwisha mkagua vyema na akaridhishwa naye.  Haya ayafanyayo hayana maana nyingine zaidi ya kujipumbaza kwa uzuri wa mwanamke huyo jambo ambalo ni haramu, kwa kuwa msichana huyo bado ni ajnabiyya kwake (mwanamke wa kando)”.

 

 

Share