20-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake: Kukaa Faragha Na Mchumba

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

20:   Kukaa Faragha Na Mchumba:

 

Ni haramu mposaji kukaa faragha na mchumba wake, ni sawa kwa ajili ya kumwangalia au kwa jambo jingine.  Kukaa faragha kati ya wawili hawa hakusalimiki na hatari ya kutumbukia kwenye haramu.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kukaa faragha kati ya mwanamke na mwanaume akisema: 

 

"لَا يَخْلُوَنَّ رَجُلٌ بِامْرَأَةٍ إِلَّا كَانَ ثَالِثُهُمَا الشَّيْطَان"

 

“Haipati kutokea mwanaume akakaa faragha na mwanamke isipokuwa shaytwaan anakuwa wa tatu wao”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Ahmad (1/18) na At-Tirmidhiy]

 

Na amesema tena: 

 

 "لَا يَخْلُوَنَّ رَجُلٌ بِاِمْرَأَةٍ إِلَّا مَعَ ذِي مَحْرَمٍ" 

 

“Asithubutu mwanaume kukaa faragha na mwanamke isipokuwa aweko pamoja nao mahram yake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3006) na Muslim (1341)]

 

Waliotoka nje ya mstari wa Dini ya Allaah na Sharia Yake, wanadai kwamba mposaji kuongozana na mchumba wake, kukaa naye pamoja faraghani, na kusafiri naye, ni jambo lisilo na budi, eti kwa kuwa kila mmoja atapata kumjua na kumsoma mwenzake vizuri.

 

Na anayeutizama mwenendo wa nchi za magharibi katika suala hili, atakuta kwamba mwenendo huu haujaleta matokeo yoyote chanya ya kutambuana au kuvaana vilivyo kati ya wachumba wawili, bali zaidi ni mvulana kumhama mchumba wake baada ya kumvunja bikira.  Kadhalika, anaweza kumwacha akiwa mja mzito, halafu baadaye msichana anakuja kutaabika peke yake katika kubeba jukumu la ulezi.  Msichana huyu anaweza pia kuitoa mimba bila kujali chochote.

 

Na hata wale ambao wanakaa muda mrefu kwenye posa na kisha kuoana, kila mmoja anakuja kugundua baadaye kwamba uchumba huo mrefu haukuweza kumfanya kila mmoja kumgundua mwenzake katika uhalisia wake.  [Ahkaamuz Zawaaj cha Dk. ‘Umar Al-Ashqar (uk. 58)]

 

 

Share