22-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Kuzungumza Na Mchumba

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا

 

Posa Na Hukumu Zake

 

 

 

Alhidaaya.com

 

 

22:   Kuzungumza Na Mchumba:

 

Inajuzu mposaji kuzungumza na mchumba wake kama atahitajia lakini kwa sharti ya uwepo wa mahram yake.  Na hii ni ima kutaka kuijua sauti yake, au kuchukua rai yake kuhusiana na maisha yao yajayo ya ndoa.  Mwanamke naye ana haki hiyo pia lakini kwa sharti ya kuwajibika na vidhibiti vya kisharia.  Maneno yake yawe kwa mujibu wa haja, asilegeze sauti wala mwenyewe asijilainishe.  Allaah Amesema:

 

"فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا"

 

“Basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi, na semeni kauli inayokubalika.  [Al-Ahzaab: 32]

 

Na kati ya yanayoonyesha kujuzu kuzungumza kwa vidhibiti vya kisharia ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ"

 

“Na mnapowauliza wake zake haja, waulizeni nyuma ya pazia”.  [Al-Ahzaab: 53]

 

Kadhalika, Nabiy Muwsaa (‘alayhis salaam) aliwasemesha wanawake wawili wa Madyan kama inavyoeleza Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِّنَ النَّاسِ يَسْقُونَ وَوَجَدَ مِن دُونِهِمُ امْرَأَتَيْنِ تَذُودَانِ ۖ قَالَ مَا خَطْبُكُمَا ۖ قَالَتَا لَا نَسْقِي حَتَّىٰ يُصْدِرَ الرِّعَاءُ ۖ وَأَبُونَا شَيْخٌ كَبِيرٌ"

 

Alipofikia maji ya Madyan, alikuta kundi la watu linanywesha maji (wanyama wao), na akakuta kando yake wanawake wawili wanawazuia (wanyama wao).  Akasema:  Mna nini?  Wakasema:  Hatunyweshi mpaka waondoke wachungaji, na baba yetu ni mtu mzima sana”.  [Al-Qaswas:  23]

 

 

Kadhalika, kuna Hadiyth nyingi zinazogusia suala hili.  Kati yake ni ya Anas kuhusiana na kisa cha kufariki Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo sehemu yake inasema:

 

 "فَلَمَّا دُفِنَ، قَالَتْ فَاطِمَةُ عَلَيْهَا السَّلاَمُ: يَا أَنَسُ، أَطَابَتْ أَنْفُسُكُمْ أَنْ تَحْثُوا عَلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم التُّرَابَ"

 

 

Alipozikwa, Faatwimah (‘alayhas Salaam) alimwambia Anas:  Ee Anas!  Hivi kweli mmejisikia vizuri kummiminia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mchanga!”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4462)]

 

Baadhi ya nyakati anaweza kuhitaji kuzungumza naye kwa njia ya simu.  Hili halikatazwi ila tu la muhimu ni kuchunga vidhibiti vya kisharia, watu wa mchumba wajue kwamba atazungumza naye, na yawe kwa mujibu wa haja.  Ama ikiwa simu hiyo itajenga kati yao mazingira yanayofanana na yale ya ufaragha ambayo kisharia yamekatazwa, na yakaweza kuwakokota taratibu kuingia kwenye haramu, basi kuachana nayo ni wajibu.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

 

Share