25-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Posa Na Hukumu Zake:Posa Ikivunjwa, Nini Hatima Ya Zawadi Zilizotolewa?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الخِطْبَةُ وأَحْكَامُهَا
Posa Na Hukumu Zake
25: Posa Ikivunjwa, Nini Hatima Ya Zawadi Zilizotolewa?:
Ikiwa mposaji atampa zawadi mchumba wake au akamgharamikia -wakati wa kipindi cha posa- kisha ndoa isifungwe, basi zawadi na gharama hizo hazikosi kuwa: ima sehemu ya mahari, au zawadi ya kuimarisha mapenzi na utangamano kati ya wachumba wawili.
(a) Alichokitoa kama sehemu ya mahari, hiki kina hali mbili:
Hali ya kwanza:
Kitu chenyewe kiwepo kwa dhati yake. Ni kama seti ya mkufu, pete, na bangili za dhahabu au vito ambayo mposaji anamnunulia mchumba wake baada ya posa kukubaliwa, na seti hii inajulikana kama “shabkah” (kwenye baadhi ya nchi za Kiarabu). Anaweza kumnunulia kabla ya ndoa kufungwa au baada yake kwa mujibu wa ada na desturi za eneo husika. Hii na mfano wake, ni haki ya mposaji kudai kama posa itavunjwa kwa itifaki ya ‘Ulamaa, ni sawa awe yeye kaivunja au msichana, au kwa sababu yoyote iliyo nje ya uwezo.
Hali ya pili:
Awe amenunua kifaa au chombo ili kitumike baada ya kuoana. Kuhusu hukmu ya kurejesha thamani ya mahari au chombo alichonunua, Fuqahaa wana kauli mbili:
Kauli ya kwanza:
Ni lazima arejeshewe mahari aliyolipa, kwa sababu mahari ni fidia kwa mkabala wa kustarehe na mke, na starehe haijapatikana. Hivyo ni lazima arejeshewe kitu chenyewe kama kipo, au thamani yake kama kimeharibika au kimechakaa. Haya ni madhehebu ya Jumhuwr.
Kauli ya pili:
Mwanamke hatotakwa arejeshe chombo alichokinunua ikiwa mposaji alimruhusu kununua, au alijua kimenunuliwa, au ikawa hiyo ndio ada na desturi. Na kama si hivyo, atatakiwa arejeshe mahari ambayo mposaji amelipa.
Ninaloliona kuwa lina nguvu ni kwamba ikiwa mwanaume ndiye aliyevunja posa na akawa amejua kwamba chombo kimenunuliwa kutokana na pesa ya mahari, au ikawa hiyo ndiyo ada, hapo atachukua chombo hicho, lakini haruhusiwi kumlazimisha mwanamke huyo akiuze ili amkabidhi pesa ya mauzo. Ama ikiwa mwanamke ndiye aliyevunja posa, basi atalazimika kurejesha pesa ya mahari, na kama kanunulia chombo, itabidi akiuze na arejeshe pesa.
(b) Alichokitoa kama zawadi, hiki ‘Ulamaa wana kauli nne kuhusiana na hukmu ya kurejeshewa mposaji:
Ya kwanza:
Inajuzu kukidai ikiwa bado kiko katika umiliki wa mwanamke, kiwe ni kile kile na si chingine, na asiwe amefanya lolote la kukitoa nje ya umiliki wake. Na kama kitakuwa kimeharibika au kimebadilika hali yake, hapo hawezi kukidai.
Ya pili:
Hakirejeshwi chochote hata kama sababu ya kuvunjika posa ni mwanamke isipokuwa kama waliwekeana sharti hilo. Hoja ya msingi ya kauli hii ni kwamba zawadi inabeba maana ya tunu, na mtoaji tunu haruhusiwi kisharia kuitaka tena tunu yake kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
" لَيْسَ لَنَا مَثَلُ اَلسَّوْءِ، اَلَّذِي يَعُودُ فِي هِبَتِهِ كَالْكَلْبِ يَرْجِعُ فِي قَيْئِهِ"
“Haitakikani kwetu (sisi Waislamu) kuwa mfano wa sifa mbovu. Mwenye kurejelea zawadi aliyotoa ni kama mbwa anayerejea kula matapishi yake”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2622) na Muslim]
Wakati ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu) alipojitolea farasi wake na kumpa mtu mmoja ili amtumie katika Jihaad na mtu yule akashindwa kumtunza ipasavyo, ‘Umar alitaka kumnunua. Lakini Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:
"لاَ تَشْتَرِهِ، وَإِنْ أَعْطَاكَهُ بِدِرْهَمٍ وَاحِدٍ، فَإِنَّ الْعَائِدَ فِي صَدَقَتِهِ كَالْكَلْبِ يَعُودُ فِي قَيْئِهِ"
“Usimnunue, hata akikupa kwa dirham moja, kwani mwenye kuirejea swadaqah yake ni mfano wa mbwa anayelamba matapishi yake mwenyewe”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2623)]
Ya tatu:
Zawadi itarejeshwa vyovyote aina yake iwavyo. Ikiwa bado iko kama ilivyo, itarejeshwa hivyo hivyo, na kama imechakaa, basi itarejeshwa thamani yake. Hii ni kauli ya Jumhuwr ambayo maana yake ni kwamba zawadi hizi si kama tunu, kwa kuwa miongoni mwa masharti ya tunu kwao ni kwamba isiwe na mkabala, na mtoaji (mposaji) alitoa tunu hiyo wakati wa posa kwa mkabala wa kupatikana ndoa, na ndoa haikufanyika.
Ya nne:
Ikiwa aliyevunja posa ni mwanaume, basi hana haki ya kuidai, na ikiwa ni mwanamke, basi mwanaume ana haki ya kuidai, kwa kuwa lengo la kutoa zawadi hiyo halikufikiwa. Hii ni kauli ya Ar-Raafi’iy na Ibn Arshad, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah, nayo ndiyo kauli iliyo na uadilifu zaidi. Kwa sababu, kulazimisha kurejesha zawadi kama mposaji mwenyewe ameivunja posa kunasababisha machungu mawili kwa mwanamke; uchungu wa posa kuvunjika na uchungu wa kurejesha zawadi alizopewa. Kadhalika, kuzuia zawadi zisirejeshwe kama aliyevunja posa ni mwanamke, kunaleta machungu mawili; uchungu wa kuvunjika posa na uchungu wa gharama za zawadi hizo.