14-Majini: Sampuli Za Majini Kwa Upande Wa Imani Zao Na Ukafiri Wao Na Wema Wao Na Ufisadi Wao
Majini
14- Sampuli Za Majini Kwa Upande Wa Imani Zao
Na Ukafiri Wao Na Wema Wao Na Ufisadi Wao
Allaah Akilizungumzia hili Anasema:
"وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا"
“Na kwamba miongoni mwetu ni wema, na miongoni mwetu wako chini ya hivyo; tumekuwa makundi ya njia mbali mbali”. [Al-Jinn: 11]
Ibn Jariyr amesema: “Tumekuwa makundi ya njia mbali mbali”, yaani tumekuwa wenye matamanio tofauti, makundi mbalimbali, na kati yetu yuko Muumini na yuko kafiri”.
Naye Al-Qurtubiy kasema: “Waliambiana wenyewe kwa wenyewe wakati walipowalingania wenzao wamuamini Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Hakika sisi kabla ya kuisikiliza Qur-aan, tulikuwa baadhi yetu walio wema na baadhi yetu walio makafiri”.
Na Anasema tena Allaah Ta’aalaa:
"وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ ۖ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُولَـٰئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا"
“Na kwamba miongoni mwetu ni Waislamu, na miongoni mwetu wako wakengeukaji haki; hivyo atakayesilimu, basi hao ndio waliofuata uongofu”. [Al-Jinn: 14]
Ibn Al-Qayyim amesema: “Aayaat hizi zinatuonyesha mgawanyiko wao wa matabaka matatu: Walio wema, walio chini ya walio wema na makafiri. Matabaka haya ndio yale yale waliyo nayo wanadamu ambao wako wema, walio kati na kati na makafiri. Vigawanyo hivi ndivyo vile vile ambavyo Allaah Ta’aalaa Aliwagawa Bani Israaiyl kama Anavyosema:
"وَقَطَّعْنَاهُمْ فِي الْأَرْضِ أُمَمًا ۖ مِّنْهُمُ الصَّالِحُونَ وَمِنْهُمْ دُونَ ذَٰلِكَ ۖ وَبَلَوْنَاهُم بِالْحَسَنَاتِ وَالسَّيِّئَاتِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ "
“Na Tuliwafarikisha katika ardhi mataifa mbalimbali. Miongoni mwao ni wako wema na miongoni mwao wako kinyume chake. Na Tukawajaribu kwa ya faraja na ya dhiki ili wapate kurejea (katika utiifu). [Al-A’araaf: 168]
.
Ibn Al-Baaz amesema: “Kuna majini wema, wazushaji (bid’a), makafiri na mafasiki kama walivyo wanadamu”.
Naye Ibn ‘Uthaymiyn kasema: “Majini wapo Waumini, makafiri, watiifu na waasi. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"قَالَ ادْخُلُوا فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُم مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ فِي النَّارِ"
“(Allaah) Atasema: Ingieni motoni pamoja na ummah zilizokwishapita kabla yenu miongoni mwa majini na wana Aadam”. [Al-A’araaf: 38]
Na akasema tena: “Ulimwengu wa majini asili yake ni kutokana na moto, kwa kuwa baba yao ni shetani Ibliys. Huyu, Allaah Alimuumba kutokana na moto. Kisha katika ulimwengu wao, wako walio wema na wasio wema, wako Waislamu na wako makafiri, ijapokuwa asili yao ni Ibliys aliye kafiri. Wako pia wenye kutafuta elimu na wako waliobobea kwenye ibada”.