15-Majini: Majina Ya Majini

 

 

Majini

   

Alhidaaya.com 

 

15-  Majina Ya Majini:

 

 

1-  Ifriti "العِفْرِيتُ"

 

"قَالَ عِفْرِيتٌ مِّنَ الْجِنِّ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن تَقُومَ مِن مَّقَامِكَ ۖ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ"

 

Akasema ‘Ifriti miongoni mwa majini:  Mimi nitakuletea kabla hujasimama kutoka mahali pako, na hakika mimi kwa hilo, bila shaka ni mwenye nguvu mwaminifu”.  [An-Naml:  39]

 

Ibn Jariyr amesema:  “Ifriti miongoni mwa majini ni mkuu wao, aliye shupavu zaidi na mwenye nguvu”.

 

Toka kwa Abu Hurayrah:  “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"إنَّ عِفْريتًا مِنَ الجِن ِّتَفَلَّتَ البارِحةَ ليَقطَعَ عَليَّ صَلاتي، فأمكَنَني اللَّهُ مِنه فأخَذْتُه، فأرَدتُ أن أربِطَه على ساريةٍ من سَوارَي المَسجِدِ حَتَّى تَنظُروا إليهِ كُلُّكُم، فذَكَرْتُ دَعوةَ أخي سُلَيمانَ: رَبِّ هَبْ لي مُلْكًا لا يَنبَغي لأحَدٍ من بَعْدي، فرَدَدتُه خاسِئًا" 

 

“Hakika ifriti mmoja katika majini alinitokezea ghafla ili anivurugie swalah yangu, lakini Allaah Alinipa nguvu nikaweza kumdhibiti.  Nikataka kumfunga kwenye nguzo moja kati ya nguzo za Msikiti ili nyinyi nyote muweze kumwona.  Na hapo nikakumbuka dua ya ndugu yangu Sulaymaan:  Rabb wangu!  Nitunukie ufalme asiupate mtu yeyote baada yangu, kisha nikamwachia aende zake akiwa amedhalilika”..  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (461)]

 

 

2- Ghoul  الغُولُ: (Mashetani wa majangwani)

 

Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لا عَدوَى ولا طِيَرةَ ولا غُولَ"

 

“Ugonjwa hauambukizi (ila kwa Idhni ya Allaah), wala hakuna mkosi (kwa kuona ndege anakwenda kushoto), wala mashetani wa majangwani hawadhuru kwa lolote (ila kwa Idhni ya Allaah)”.  [Swahiyhul Jaami (7531)]

 

Ibn Hajar amesema:  “Jopo la ‘Ulamaa wamesema:  “Waarabu walikuwa wakidai kwamba maghoul ambao ni aina ya mashetani, wapo kwenye majangwa.  Mashetani hawa huwatokezea watu wakiwa katika rangi tofauti tofauti, halafu huwapoteza njia, na hatimaye huwaua.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaja na kuiondosha itikadi hii”.

 

Na makusudio hapa si kukanusha uwepo wa maghoul, bali wapo, isipokuwa tu hayo waliyokuwa wakiyaamini Waarabu ndio ambayo hayapo.

 

Ibn ‘Uthaymiyn amesema:  “Waarabu walipokuwa wanasafiri, au wanakwenda kulia au kushoto, mashetani walikuwa wakiwatokezea kwa rangi za kutisha na kuogopesha na nyoyo zao zikaingia hofu kubwa.  Na hapo wanapatwa na majonzi na huzuni kubwa ya kutoweza kwenda kule walikokusudia.  Na hili bila shaka linadhoofisha nguvu ya kumtegemea Allaah.  Na shetani wakati wote ni mwenye pupa ya kuingiza wasiwasi na huzuni kwa Muislamu kiasi anavyoweza.  Allaah Anasema:

 

"إِنَّمَا النَّجْوَىٰ مِنَ الشَّيْطَانِ لِيَحْزُنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيْسَ بِضَارِّهِمْ شَيْئًا إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ"

 

Hakika mnong’ono unatokana na shaytwaan ili awahuzunishe wale walioamini, na wala hawezi kuwadhuru kwa chochote isipokuwa kwa Idhini ya Allaah.  Na kwa Allaah watawakali Waumini”[Al-Mujaadalah:  10]

 

Na mtu mara nyingi hutahiniwa kwa mambo haya ikiwa moyo wake umefungamanika nayo.  Ama ikiwa ni mwenye kumtegemea Allaah, basi hakuna lolote la kumdhuru.

 

 

Share