17-Majini: Ibliys
Majini
17- Ibliys
Neno Ibliys "إِبْلِيْسُ" katika lugha ya kawaida limenyambulika kutokana na "الإبْلاسُ" lenye maana ya kuwekwa mbali na kheri, au kukata tamaa kutokana na Rahma za Allaah. Kwa maana hii, Ibliys kawekwa mbali na kheri zote, na hana tamaa kamwe ya kuzipata Rahma za Allaah, na kwa hivyo, ni kiumbe wa kuishia motoni milele.
Ama kiistilahi, Ibliys ni kiumbe aliyeumbwa kutokana na moto. Alikuwa pamoja na Malaika akifanya pamoja nao ibada, lakini hakuwa ni katika aina yao. Na wakati Allaah Alipowaamuru Malaika Wake wamsujudie Aadam, Ibliys alikataa kutii Amri ya Mola Wake kwa kujiona kwamba yeye ni bora zaidi kuliko Aadam kwa kuwa yeye ameumbwa kutokana na moto aliouona ni bora zaidi kuliko udongo alioumbiwa nao Aadam. Yakawa matokeo ya kukaidi kwake amri ni kufukuzwa toka kwenye Rahma ya Allaah na kuteremshwa toka mbinguni kuja ardhini.
Lakini Ibliys alimwomba Allaah Ampe muhula wa kuishi mpaka Siku ya kufufuliwa. Na hapo Allaah Ambaye Ni Mwingi wa Subira Akamkubalia ombi lake, na Ibliys akachukua ahadi ya kuwapoteza wanadamu mpaka wakati huo kama inavyosema Qur-aan:
"قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ● إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ"
(Ibliys) akasema: Naapa kwa Utukufu Wako, bila shaka nitawapotosha wote • Isipokuwa waja Wako miongoni mwao waliokhitariwa kwa ikhlasi zao. [Swaad: 82-83]