18-Majini: Shaytwaan
Majini
18 Shaytwaan
Ama shaytwaan "الشَّيْطَانُ"katika lugha ya kawaida, ni kila aliye mwasi, mwovu, mshari, ni sawa akiwa katika majini, au wanadamu au wanyama. Asili yake ni kutokana na neno "شَطَنَ" (kitenzi cha wakati uliopita) chenye maana ya “amejiweka mbali”, na hii ni kwa vile shaytwaan amejiweka mbali na kheri zote au Rahma za Allaah
Qur-aan imemwita kwa jina la Shaytwaan katika aayah mbalimbali. Ni kama katika Kauli Yake Ta’alaa:
"فَوَسْوَسَ لَهُمَا الشَّيْطَانُ لِيُبْدِيَ لَهُمَا مَا وُورِيَ عَنْهُمَا مِن سَوْآتِهِمَا وَقَالَ مَا نَهَاكُمَا رَبُّكُمَا عَنْ هَـٰذِهِ الشَّجَرَةِ إِلَّا أَن تَكُونَا مَلَكَيْنِ أَوْ تَكُونَا مِنَ الْخَالِدِينَ "
“Basi shaytwaan (naye ni Ibliys) akawatia wasiwasi ili awafichulie sehemu zao za siri zilizositiriwa. Na akasema: Rabb wenu Hakukukatazeni huu mti isipokuwa msijekuwa Malaika wawili au kuwa miongoni mwa wenye kudumu milele”. [Al-A’araaf: 20]
Na Kauli Yake Ta’aalaa:
"يَا بَنِي آدَمَ لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُم مِّنَ الْجَنَّةِ يَنزِعُ عَنْهُمَا لِبَاسَهُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوْآتِهِمَا"
“Enyi wana wa Aadam! Asikufitinisheni kabisa shaytwaan kama alivyowatoa wazazi wenu katika Jannah, huku akiwavua nguo zao ili awaonyeshe sehemu zao za siri”. [Al-A’araaf: 27]
Ama kiistilahi, tamko la "الشَّيطانِ" linaweza kukusudiwa kwa maana ya Ibliys mwenyewe hasa kama katika kisa cha Aadam na Ibliys. Pia linaweza kukusudiwa kila mbaya, mharibifu, na mwenye kulingania upotevu katika majini au binadamu. Ni kama Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ"
“Na hivyo ndivyo Tulivyojaalia kwa kila Nabiy maadui mashaytwaan wa kibinadamu na kijini, wanadokezana wenyewe kwa wenyewe maneno ya kupambapamba”. [Al-A’araaf: 112]