09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (f) Ni Nani Mawalii?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
09: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (f) Ni Nani Mawalii?
Mawalii wa mwanamke ambao wana haki ya kumwozesha ni (العَصَبَةُ)“Al-‘Aswabah”, nao ni akaribu zake wanaume kwa upande wa baba yake na si kwa upande wa mama yake. Haya ndiyo madhehebu ya Jumhuwr kinyume na Abu Haniyfah ambaye anasema kwamba hata jamaa wa mama yake pia ni mawalii.
‘Ulamaa wamekhitilafiana katika suala la nani mwenye haki zaidi ya kutangulizwa na vipi unakuwa mpangilio.
- Mahanafiy: Kwanza watoto wa kiume wa mwanamke, kisha watoto wao, halafu baba kisha babu, halafu makaka kisha watoto wao, halafu maami, na mwisho watoto wao.
- Wamaalik: Kwanza watoto wa kiume, kisha watoto wao, halafu baba, kisha makaka halafu watoto wao, na mwisho babu.
- Mashaafi’iy: Kwanza baba, halafu babu, kisha makaka halafu watoto wao, halafu maami na hatimaye watoto wao.
- Mahanbali: Kwanza baba, halafu babu, kisha watoto halafu watoto wao, kisha makaka halafu watoto wao, kisha maami na mwisho watoto wao.
Ninasema: “Kidhibiti kwa walii ni ukaraba, kuwa na pupa na maslaha ya mwanamke, na kumsimamia. Na baba kiuhalisia, ndiye walii aliye karibu zaidi, na ndiye mwenye penzi na huruma zaidi. Katika hili, anafuatiwa na babu, yeye ni kama baba, na anaweza kuwa na huruma na mapenzi zaidi kwa mabanati wa mwanaye.
Wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), baba (kama yuko) alikuwa ndiye anayefunga ndoa ya binti yake. Abu Bakr na ‘Umar waliwaozesha ‘Aaishah na Hafswah kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaozesha mabinti zake. Kadhalika, Maswahaba pia. Na kama baba au babu hawako, basi jamaa wa karibu zaidi kisha anayefuatia atasimamia hilo. Mimi ninavyoona, kauli yenye nguvu zaidi ni ya Mashaafi’iy kisha Mahanbali (Rahimahumul Laah) kutokana na yaliyotangulia, na kwa vile mtoto anaweza kugoma kumwozesha mama yake kinyume na kaka na ami. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
Mawalii Walio Ngazi Moja Wakivutana, Nini Kifanyike?
Ni kama ndugu wawili kuzozana, kila mmoja wao ana mtu anayetaka kumwozesha dada yao, au mama yao kwa mfano. Ikiwa mwanamke atamkubali yeyote katika hao wanaume wawili bila kuainisha, na ndugu zake wakawa kila mmoja ameozesha, basi ndoa iliyofungwa mwanzo ndio itakayozingatiwa. Na hii ni kwa Hadiyth ya Samurah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَيُّمَا امْرَأَةٍ زَوَّجَهَا وَلِيَّانِ، فَهِيَ لِلْأَوَّلِ مِنْهُمَا"
“Mwanamke yeyote ambaye ameozeshwa na mawalii wawili (mmoja kamwozesha mume na mwingine mume mwingine), basi ni mke wa mume wa kwanza (kwa walii wa kwanza)”. [Imesimuliwa na Ahmad. At-Tirmidhiy kasema ni Hasan]
Hii ni kwa vile ndoa ya mume wa pili, inakuwa ni kumwozesha mwanamke ambaye ameshaolewa, na hili halifai.
Ama ikiwa mwanamke atamkataa mmoja wao, basi ndoa ya mkataliwa haiswihi, kwa kuwa ridhaa yake mwanamke ni sharti ya kuswihi ndoa yake.
Ikiwa mvutano utaendelea kati ya mawalii, basi mwanamke atakuwa na haki ya kuwasilisha shauri lake kwa kadhi, na kadhi atakuwa na haki ya kumwozesha wakati huo kutokana na kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"فَإِنِ اشْتَجَرُوا فَالسُّلْطَانُ وَلِيُّ من لَا وَليَّ لَهُ ".
“Na kama watavutana, basi kiongozi (kadhi) ndiye walii kwa asiyekuwa na walii”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2083), At-Tirmidhiy (1101), Ibn Maajah (1879) na Ahmad (6/156)]