10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (g) Kuozesha Walii Wa Mbali Kama Wa Karibu Hayuko

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

عَقْدُ الزَّوَاجِ

 

Kufunga Ndoa

 

Alhidaaya.com

 

 

10:  Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (g) Kuozesha Walii Wa Mbali Kama Wa Karibu Hayuko:

 

 

Kiasili, haijuzu walii wa mbali kuozesha ikiwa wa karibu yuko.  Ikiwa wa karibu hayuko, na kumsubiri hadi awepo kutapoteza maslaha ya mwanamke, basi hapo uwalii utahamia kwa wa mbali.  Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ahmad na Maalik.  Kadhalika, ikiwa walii wa karibu atamzuia asiolewe na mtu mwenye vigezo, basi hapo uwalii utahamia kwa wa mbali.

 

Na ikiwa walii wa mbali ataruhusu na mwanamke akaolewa, basi baada ya hapo, walii wa karibu hatokuwa na haki ya kupinga ndoa hiyo au kutaka ivunjwe.

 

Je, Inajuzu Kwa Walii Kumwakilisha Mtu Mwingine Au Kutoa Wasiya Wa Kuozesha?

 

Inajuzu kwa walii kumwakilisha mtu kumwozesha mwanamke ambaye yeye anasimamia mambo yake.  Mwakilishi huyo atabeba yote yanayomuhusu walii.

 

Ama wasiya wa kuozesha baada ya yeye kufa, kauli sahihi zaidi ya ‘Ulamaa inasema kwamba hilo halijuzu.  Uwalii haupatiwi manufaa kwa wasiya, kwa kuwa uwalii wa muusiaji unakatika kwa kifo chake mbali na kwamba penzi na huruma vinavyomfanya walii kuwa walii, vinakuwa haviko tena.

 

Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, riwaayah toka kwa Ahmad, Ath-Thawriy, An Nakh’iy, Ibn Al-Mundhir, Ibn Hazm na Ash-Shawkaaniy.

 

 

Share