11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (h) Masharti Ya Walii:
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
11: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (h) Masharti Ya Walii:
(a) Awe Muislamu. Kafiri hana uwalii kwa mwanamke wa Kiislamu. Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema:
"وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ"
"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao", [At-Tawbah: 71]
Anasema tena:
"وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ"
“Na wale waliokufuru ni marafiki wandani wao kwa wao”. [Al-Anfaal: 73]
Na Anasema tena:
"وَلَن يَجْعَلَ اللَّـهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا"
“Na Allaah Hatojaalia kwa makafiri njia ya kuwashinda Waumini”. [An-Nisaa: 141]
Hii ni kauli ya ‘Ulamaa wote. Ibn Al-Mundhir amesema: “Wote tunaowajua vyema, wamelikubali hili”.
(b) Awe mwanaume: Ni sharti lililopata itifaki ya wote.
(c) Awe na akili timamu: Asiye na akili hawezi kusimamia maslaha yake, vipi ataweza kusimamia maslaha ya mwingine!
(d) Awe amebaleghe: Ni sharti kwa ‘Ulamaa walio wengi.
(e) Awe huru: Ni sharti kwa ‘Ulamaa walio wengi. Mtumwa hana uwezo wa kujisimamia mwenyewe, hivyo hawezi kumsimamia mwingine.
Ash-Shaafi’iy ameshurutisha jingine ambalo ni uadilifu. Ni lazima walii awe mwadilifu, akiwa kinyume chake, basi haaminiki kumchagulia mwanamke mtu afaaye. Lakini Jumhuwr wanasema kwamba uadilifu si sharti kwa walii, kwa sababu hali ambayo walii anamchagulia binti yake mtu mwenye vigezo, inakuwa ni hali ya kimaumbile, nayo ni kumtakia lenye kheri kwake, na uadilifu hapo unakuwa hauna nafasi, ni sawa awe mwadilifu au asiwe mwadilifu, yote ni sawa.