12-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (i) Je, Walii Anaweza Kujiozesha Mwenyewe Mwanamke Ambaye Yeye Anasimamia Mambo Yake?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

عَقْدُ الزَّوَاجِ

 

Kufunga Ndoa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

12:  Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (i) Je, Walii Anaweza Kujiozesha Mwenyewe Mwanamke Ambaye Yeye Anasimamia Mambo Yake?

 

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa akiwemo Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy, Abu Haniyfah, Maalik, Al-Layth, Ibn Hazm na wengineo wanasema kwamba yeyote mwenye kusimamia jambo la mwanamke -na hakuwa katika maharimu zake- basi inajuzu kwake kujiozeshea yeye mwenyewe kama mwanamke ataridhia hilo, na mwanaume huyu hahitajii mwanaume mwingine ili amwozeshe.  Dalili zao ni haya yafuatayo:

 

1-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ"

 

“Na waozesheni wajane miongoni mwenu na walio Swalihina kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu”.  [An-Nuwr:  32]

 

Basi yeyote atakayejiozesha mwenyewe mjane kwa ridhaa yake, basi anakuwa amefanya Aliloamrishwa na Allaah Ambaye Hakumzuia mwozeshaji wa mjane kuwa huyo huyo ndiye mwenye kumwoa.

 

2-  Hadiyth ya Anas bin Maalik kwamba:

 

 "أَنَّ رَسُوْلَ اللهِ َصَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَعْتَقَ صَفِيَّةَ، وَجَعَلَ عِتْقَهَا صَدَاقَهَا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwacha huru Swafiyyah, na akaufanya uhuru huo kuwa ndio mahari yake”.  [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4200) na Muslim (1365)]

 

Hapa tunaona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amejiozesha mwenyewe kijakazi wake.

 

3-  Bibi ‘Aaishah akiizungumzia aayah hii:

 

"وَيَسْتَفْتُونَكَ فِي النِّسَاءِ ۖ قُلِ اللَّـهُ يُفْتِيكُمْ "

 

“Na wanakuuliza wewe hukmu ya kishariy’ah (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu wanawake.  Sema: Allaah Anakubainishieni hukmu ya kishariy’ah kuhusu wao”, anasema kwamba inahusiana na binti yatima anayelelewa na mwanaume, na yatima akawa na mali ambayo mwanaume huyo akaichanganya na mali yake.  Halafu ikatokea kwamba mwanaume asipende kumwoa yatima huyu, na pia akahofia kumwozesha kwa mwanaume mwingine asije kufaidika na mali yake na hivyo akamfunga asiolewe.  Na hapo ndipo Allaah Alipowakataza jambo hilo”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4200) na Muslim (1365)]

 

4-  Toka kwa Sa’iyd bin Khaalid kwamba Ummu Hakiym bint Qaaridh alimwambia ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf:

 

"إِنَّه قَدْ خَطَبَنِي غَيْرُ وَاحِدٍ، فَزَوِّجْني أَيَّهُم رَأَيْتَ، قَالَ: أَتَجْعَلِيْنَ أَمْرَكِ إِلَيَّ ؟ قالت: نَعَمْ، فَقَالَ: قَدْ تَزَوْجُتِكِ"

“Mimi nimeposwa na zaidi ya mtu mmoja, basi niozeshe yeyote unayemwona ananifaa.  Akasema:  Je, utaniachia mimi hilo (la kukuoa)?  Akasema:  Na’am.  Akasema:  “Basi nimekuoa”.  [Al-Bukhaariy ameizingatia mu’allaq (9/94)]

 

Ash-Shaafi’iy na Daawuwd wamesema kwamba haijuzu kujiozesha mwenyewe mwanamke ambaye mtu ana madaraka juu yake bali mtu mwingine ndiye atamwozesha.  Sababu waliyotoa ni:

 

1-  Asili ya Rasuli katika kujiozesha ni kwamba hilo ni jambo mahsusi kwake mpaka ipatikane dalili ya kuwahusisha Waislamu wote.  Hivyo haiwezekani kutolea dalili kwa Hadiyth ya Swafiyyah.

 

 2-  Haijuzu mwoaji kuwa mwozeshaji.  Ni kama kutowezekana hakimu kuwa shahidi kwa wakati mmoja.

 

Ninasema:  “Kauli inayosema kwamba inajuzu ndiyo yenye nguvu zaidi kwa vile hakuna dalili yoyote yenye kuzuia.  Ama ndoa ya Swafiyyah, tukichukulia kwamba ndoa za Rasuli zina umahususi- na hili halina shaka- basi mbali ya hili, tunaona kwamba kuna Hadiyth nyingi tu sana zinazohimizia kumwoa kijakazi baada ya kumfundisha maadili mema na kumwacha huru.  Na hili linawahusu wote.

 

 

Share