030-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-BASWIYR
أسماء الله الحسنى وصفاته
Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake
الْبَصِير
Al-Baswiyr
30-Al-Baswiyr: Mwenye kuona yote daima
Allaah (Tabaaraka wa Ta'aalaa) Ndiye Mwenye kuona: Uoni Wake unaenea kila yenye kuonwa ardhini na mbinguni.
Jina hili tukufu lina maana mbili:
Kwanza: Uoni kwa njia ya kuona, yaani Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasifika kwa ukamilifu wa kuona, iliyo laiki na Utukufu Wake, na Ukamilifu Wake na Ukubwa Wake, hakuna chenye kuzuia kuona Kwake; yaliyo chini ya ardhi mbili saba, wala juu ya mbingu saba.
Pili: Mwenye Uoni wa vitu, ulimwengu na vilivyojificha, Mwenye Ujuzi navyo, Mwenye kuona yaliyo ndani yake Yeye ni Mjuzi wa wanayoyajua.
Jina hili tukufu limekariri mara nyingi mno katika Qur-aan likifuatana na Majina mengineyo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Mojawapo ni Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَأَنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ ﴿٦١﴾
Hivyo ni kwa kuwa Allaah Anaingiza usiku katika mchana, na Anaingiza mchana katika usiku, na kwamba Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Al-Hajj: 61]
Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah; Al-Baswiyr:
1-Tahadhari kufanya maasi kwa siri ukidhania kwamba hakuna anayekuona ilhali Al-Baswiyr Anaona yaliyodhahiri na yaliyofichika.
2-Fikia daraja ya Ihsaan ambayo ni kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kana kwamba unamuona, kama ilivyothibiti katika Hadiyth ndefu, pindi Jibriyl (‘alayhis-salaam) alipofika kuwafundisha Waislamu mambo ya Dini yao kupitia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Basi katika maswali aliyomuuliza likukuwa ni swali kuhusu Ihsaan:
فأَخْبرني عَنِ الإحْسَانِ. قَالَ: ((أنْ تَعْبُدَ اللهَ كَأنَّكَ تَرَاهُ فإنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فإنَّهُ يَرَاكَ)).
Nielezee kuhusu Ihsaan. Akasema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona na kama humuoni basi Yeye Anakuona.” [Muslim]
3-Kumbuka pia Al-Baswiyr Anakuona unapofanya ibaada zako, hivyo basi zitekeleze kwa ikhlasi na unyenyekevu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kumwambia Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٢١٨﴾
Ambaye Anakuona wakati unaposimama.
وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ ﴿٢١٩﴾
Na mageuko yako katika wenye kusujudu.
إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٢٢٠﴾
Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Ash-Shu’araa (218-220)]
4-Unapodhulumiwa kwa vyovyote vile, thibitika katika subira, na kukumbuka na kuwa na yaqini kwamba, Al-Baswiyr Anaona yote uliyotendewa ya dhulma na Atalipiza dhulma ulizotendewa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alikuwa Akimpooza Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila alipokuwa akiudhiwa na kudhulumiwa na makafiri wa Makkah, Akimwambia:
وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٤٨﴾
Na vuta subira (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa hukumu ya Rabb wako, kwani hakika wewe uko chini ya Macho Yetu. [Atw-Twuwr (48)]
5-Tumia neema ya kuona kwa mambo yanayomridhisha Al-Baswiyr, na jiepushe na kutazama yasiyomridhisha. Neema mojawapo kubwa ni kujaaliwa kuweza kuyaona Maneno ya Allaah katika Mswahafu ukaweza kuyasoma.
6-Mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kukujalia kuwa na macho mazima na muombe aithibitishe neema hiyo Asiijaalie kukuondoshea, kwani wangapi walikuwa na macho mazima, hatimaye wakapofuka macho?
7-Omba duaa iliyothibiti katika Adhkaar za asubuhi na jioni, ya kuomba hifadhi na usalama wa macho yako:
للّهُـمَّ عافِـني في بَدَنـي، اللّهُـمَّ عافِـني في سَمْـعي، اللّهُـمَّ عافِـني في بَصَـري، لا إلهَ إلاّ أَنْـتَ. اللّهُـمَّ إِنّـي أَعـوذُبِكَ مِنَ الْكُـفر، وَالفَـقْر، وَأَعـوذُبِكَ مِنْ عَذابِ القَـبْر، لا إلهَ إلاّ أَنْـتَ. (ثلاثاً)
Ee Allaah, nipe afya ya mwili wangu, Ee Allaah, nipe afya ya usikizi (masikio) wangu, Ee Allaah, nipe afya ya uoni (macho) wangu, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe. Ee Allaah, hakika mimi najikinga Kwako kutokana na ukafiri, na ufakiri, na najikinga Kwako kutokana na adhabu ya kaburi, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe. [Swahiyh Abiy Daawuwd (5090), Ahmad (5/42), An-Nasaaiy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah [22], Al-Bukhaariy katika Adab Al-Mufrad na isnadi yake ameipa daraja ya Hasan Al-‘Allaamah Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah) katika Tuhfat Al-Akhyaaar (Uk. 26).