031-Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-'ALIYM

 

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

الْعَلِيم

 

031-Al-'Aliym

 

 

 

 

 

Al-‘Aliym: Mjuzi Wa Yote Daima

 

 

Mwenye Ilimu kubwa: Yeye ni Ambaye kujua Kwake kumezingira mambo ya dhahiri na ya ndani, ya siri na ya bayana, yaliyopita, ya sasa na yajayo. Kwake hakijifichi kitu chochote, ni Mjuzi daima wa kila kitu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٣٢﴾

Wakasema: Utakasifu ni Wako! Hatuna ilimu isipokuwa Uliyotufunza, hakika Wewe Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Baqarah (2:32)]

 

Jina hili tukufu limekariri mara nyingi katika Qur-aan. Mojawapo ni Aayah iliyotangulia kutajwa, na katika Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِن تُبْدُوا شَيْئًا أَوْ تُخْفُوهُ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٥٤﴾

Mkidhihirisha kitu chochote au mkikificha, basi hakika Allaah daima Ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-Ahzaab (33:54)]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ni Mjuzi wa kila kitu, Ambae kwa ukamilifu wa Ilimu Yake, Hujua yaliyo kwa viumbe Vyake na vilivyomo nyuma yao, wala haianguki ujani ila anajua wala atomu ila kwa ruhusa Yake kama Anavyosema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٥٩﴾

Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghaibu, hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua, wala punje katika viza vya ardhi, wala kinyevu na kikavu isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha wazi. [Al-An’aam (6:59)]

 

 

Anajua yenye kupita katika nyoyo za watu na Anajua yatakayokuwa, kilichojificha Kwake kiko wazi, kilichositiriwa kipo wazi, Hujua siri na yaliyowazi kama Anavyosema:

 

وَإِن تَجْهَرْ بِالْقَوْلِ فَإِنَّهُ يَعْلَمُ السِّرَّ وَأَخْفَى ﴿٧﴾

Na ukinena kwa jahara, basi hakika Yeye Anajua siri na yanayofichika zaidi ya siri. [Twaahaa (20:7)]

 

Siri ya mja na ndani ya dhamira yake hujulikana, na wakati gani ataitamka, na wakati gani ataifikiria moyoni mwake. Ilimu Yake ni ya tangu ya milele, ujinga haujamtangulia wala haimfikii kusahau. Anasema

(Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

قَالَ عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي فِي كِتَابٍ ۖ لَّا يَضِلُّ رَبِّي وَلَا يَنسَى ﴿٥٢﴾

 (Muwsaa) akasema: Ujuzi wake uko kwa Rabb wangu katika Kitabu. Rabb wangu Hakosei na wala Hasahau. [Twaahaa (20:52)]

 

 

Miongoni mwa ukamilifu wa Ilimu Yake ni:

 

i-Anajua yaliyokuwa na yatakayokuwa kabla ya kua, na yatakayokuwa na ambayo hayatakuwa kabla ya kua, Yeye Ndiye Mtukuka Anajua yaliyokuwa na yatakayokuwa mustakbali ambayo hayana mwisho.

 

ii-Ilimu Yake imeenea vitu vyote, ndani yake na nje yake, madogo na makubwa, kwa ukamilifu wake, Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِن تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا ۖ وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ﴿١٢٠﴾

Ikikupateni kheri (nusura, ushindi) inawachukiza, na likikusibuni baya hulifurahia. Na kama mtasubiri na mkashikamana na taqwa, basi hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kuyazunguka wayatendayo.  [Aal-‘Imraan (3:120)]

 

 

iii-Anajua yaliyo kwenye mbingu saba na ardhi saba, na yaliyo baina yake, na yaliyochini ya mchanga na chini ya kina cha bahari, na maoteo ya kila unywele, na kila mti na kianguko cha kila ujani, na idadi ya vijiwe na mchanga na udongo. Anajua kila kitu, wala haijifichi Kwake, Naye Yuko Juu ya Arshi (Istawaa: Yupo juu kwa namna inayolingana na Uadhama na Ujalali Wake Yeye Mwenyewe Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

 

iv-Katika ukamilifu wa Ilimu Yake, ni kwamba, Ilimu Yake katika kila kitu, na ya nyuma na yaliyopo na yajayo, hakuna sehemu ambayo Ilimu Yake haiingii. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿٧٥﴾

Hakika Allaah Ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-An’faal (8:75)]

 

v-Katika ukamilifu wa Ilimu Yake ni kuwa, Anajua matendo yote ya viumbe Vyake, viwe vinatendwa hadharani au kwa siri. Na Anajua kila kitu kiwe kikubwa au kidogo vipi hata kama saizi ya atomi, hakuna kinachofichika Kwake, kiwe angani, ardhini au baharini. kama Anavyosema: (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ ۚ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴿٦١﴾

Na hushughuliki katika jambo lolote, wala husomi humo katika Qur-aan, wala hamtendi amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichiki kwa Rabb wako hata cha uzito wa chembe (kama atomu) katika ardhi, wala mbinguni, wala kidogo kuliko hicho, wala kikubwa zaidi ya hicho, isipokuwa kimo katika Kitabu bainifu. [Yuwnus (10:61)]

 

Na Anasema pia katika kauli ya Luqmaan kumwambia mwanawe:

 

يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿١٦﴾

16.Ee mwanangu! Hakika likiweko (zuri au ovu) lolote lenye uzito wa punje ya hardali, likawa katika jabali au mbinguni au ardhini, Allaah Atalileta tu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Luqmaan 31:16)]

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah; Al-‘Aliym:

 

1-Tafuta ilimu ya Dini, na ilimu mojawapo kubwa ni kujifunza Majina Matukufu ya Allaah. Basi pindi utakapojifuza utafahamu kabisa nani Al-‘Aliym na Sifa Zake, na Uwezo Wake wa Kujua kila kitu. Basi ni muhimu wa hali ya juu kutafuta ilimu hii kwani vipi utajua kuwambudu ipasavyo na kutekeleza ibaada zako na kumtii Amri Zake na makatazo Yake ikiwa hutotafuta ilimu? 

 

 

 

2-Ilimu nyenginewe muhimu kabisa ni kujifunza Qur-aan na kuifahamu vyema na kufanyia kazi maamrisho yake na makatazo yake. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الرَّحْمَـٰنُ ﴿١﴾ عَلَّمَ الْقُرْآنَ ﴿٢﴾ خَلَقَ الْإِنسَانَ ﴿٣﴾ عَلَّمَهُ الْبَيَانَ ﴿٤﴾

Ar-Rahmaan.  Amefundisha Qur-aan. Ameumba binaadam. Amemfunza ufasaha. [Ar-Rahmaan 55-1-4)]

 

 

3-Tafuta ilimu ya kidunia utambue ulimwengu na Alivyoviumba Allaah Al-‘Aliym, ili utambue Utukufu Wake na Uwezo Wake mkubwa, na ndipo utakapomuadhimisha na kukmhofu, na pia ndipo utakapompwekesha katika Tawhiyd Zake za   Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji, Ufalme, Uendeshaji ulimwengu, Kuruzuku na kadhaalika) na Tawhiyd ya Al-Uluwhiyyah (ibaada).  Tawhiyd ya Majina Yake Mazuri na Sifa Zake Tukufu. Basi Muumini atamtambua vyema Rabb Wake na kumwabudu kwa kumpwekesha, na kutambua Utukufu Wake wa Uumbaji Wake, kinyume na makafiri.  Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ ۚ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿١٠﴾

 (Allaah) Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona, na Akaweka katika ardhi milima iliyosimama imara ili isiyumbe nanyi, na Akaeneza humo kila viumbe vinavyotembea. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji, Tukaotesha humo kila aina ya mimea mizuri yenye manufaa.

 

هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾

Huu ni Uumbaji wa Allaah, basi nionyesheni nini walichokiumba wasiokuwa Yeye. Bali madhalimu wamo katika upotofu bayana. [Luqmaan 31:10-11)]

 

Na Anasema pia:

 

قُلِ انظُرُوا مَاذَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَن قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ﴿١٠١﴾

Sema: Tazameni yaliyoko mbinguni na ardhini. Lakini Aayaat (Ishara, Dalili) zote na maonyo (ya Rusuli) hayawafai kitu watu wasioamini. [Yuwnus (10:101)]

 

Basi watu wangapi wanapitia Uumbaji wa Allaah lakini hawaamini kwa kuwa hawakuaamini na kutafuta ilimu ya kumtambua vyema Muumba na Mjuzi kila kitu. Huzipitia Ishara Zake na kuzipuuza.  Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

 

وَكَأَيِّن مِّنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ ﴿١٠٥﴾

Ni Aayah (Ishara, Dalili) nyingi sana katika mbingu na ardhi wanazipitia na huku wao wanazipuuza. [Yuwsuf (12:105)]

 

 

4-Utakapotafuta ilimu ukawa na ujuzi wa kutosha, basi hapo utakuwa miongoni mwa ‘Ulamaa wanaomkhofu Allaah kama Anavyosema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ  

Hakika wanaomkhofu Allaah katika Waja Wake ni ‘Ulamaa. [Faatwir (35:28)]

 

5-Omba duaa ya kukuwezesha kuzidishiwa ilimu. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۗ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِن قَبْلِ أَن يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ ۖ وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا ﴿١١٤﴾

Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Na wala usiiharakize Qur-aan (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kabla haikumalizwa kufunuliwa Wahy kwako. Na sema: Rabb wangu! Nizidishie Ilimu. [Twaahaa (20”114)]

 

 

6-Tambua kwamba mwenye ilimu na asiye ilimu hawalingani sawa, mwenye ilimu ndiye mbora zaidi mbele ya Allaah kwa kuwa ndiye atakayekuwa anatekeleza ibaada zake kumwabudu na kumnyenyekea na kutaraji Rehma Zake.  Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٩﴾

Je, yule anayeshikamana na ibaada nyakati za usiku akisujudu na kusimama (kuswali) ilhali anatahadhari na Aakhirah, na anataraji Rehma ya Rabb wake (ni sawa na aliye kinyume chake?). Sema: Je, wanalingana sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Hakika wanakumbuka wenye akili tu. [Az-Zumar (39:9)]

 

 

7-Tahadhari na kutenda maasi, na tambua kwamba Al-‘Aliym Anajua kila utendayo. Kumbuka kwamba Anakuona na Anajua unapokuwa peke yako na unapokuwa pamoja na wengine, na Anajua ya dhahiri na ya siri zako na Anajua niyya yako na mpaka unayoyafikiria akilini mwako, Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

Na kwa yakini Tumemuumba binaadam na Tunajua yale inayowaza nafsi yake na Sisi. Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo. [Qaaf (50:16)]

 

 

8-Amini na kubali Qadar na Qadhwaa ya Allaah juu yako pindi linapokufika jambo usilolipenda au inapokusibu misiba kwani Yeye ni Al-‘Aliym (Mjuzi zaidi) wa yanayokusibu. Maumivu yoyote, mfadhaiko, kukatishwa tamaa, na dhuluma yoyote unayopitia, Al-‘Aliym Anaijua na Anajua sababu zake, na kwamba ndani ya misiba kuna kheri kwako ambazo huzijui lakini Al-‘Aliym Anazijua. Na Amekujaalia Aliyokujaalia kwa mipango Yake na Hikma Zake. Basi jikumbushe hili ili kumkaribia Yeye na kumbuka tu kwamba Yeye Ni Al-‘Aliym (Mjuzi daima wa yote) nawe hujui kitu!

Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾

Mmeandikiwa sharia kupigana vita nako kunachukiza mno kwenu. Lakini asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni la kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah (2:216)]

 

9-Mdhukuru Al-‘Aliym katika Adhkaar za asubuhi na jioni kwa kuomba duaa ya kinga  ambayo imethibiti pindi ukitamka hivyo mara tatu asubuhi na jioni hutodhuriwa na chochote: 

 

بِسـمِ اللهِ الذي لا يَضُـرُّ مَعَ اسمِـهِ شَيءٌ في الأرْضِ وَلا في السّمـاءِ وَهـوَ السّمـيعُ العَلـيم (ثلاثاً)

Kwa jina la Allaah Ambaye hakidhuru kwa jina Lake kitu chochote kile kilicho ardhini, wala mbinguni, Naye ni Mwenye Kusikia yote daima Mjuzi wa yote daima.

 

 

 

Share