032-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-'AFUWW

 

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

الْعَفُوّ

 

 

Mwingi Wa Msamaha

 

 

 

 

 

031-Al-‘Afuww: Mwingi Wa Msamaha.

 

 

Jina hili limekariri mara kadhaa katika Qur-aan. Miongoni mwa Kauli Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni zifuatazo:

 

ذَٰلِكَ وَمَنْ عَاقَبَ بِمِثْلِ مَا عُوقِبَ بِهِ ثُمَّ بُغِيَ عَلَيْهِ لَيَنصُرَنَّهُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ ﴿٦٠﴾

Ndivyo hivyo, na yeyote anayejilipizia mfano wa ubaya aliofanyiwa, kisha akaja kufanyiwa baghi (kudhulumiwa) tena, bila shaka Allaah Atamnusuru. Hakika Allaah bila shaka Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria. [Al-Hajj (22:60)]

 

فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَفُوًّا غَفُورًا ﴿٩٩﴾

Basi hao bila shaka Allaah Atawasamehe. Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria. [An-Nisaa :4:99)]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Al-‘Afuww, ni Ambaye Anafuta dhambi na kuzisamehe. Hatoi adhabu kwa dhambi hizo pamoja na kuwa mja anastahiki adhabu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Al-‘Afuww:

 

i-Mwenye kusamehe mno madhambi ya waja Wake, kusikokuwa na mwisho, Naye (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambae Anasamehe madhambi, na kufuta athari zake zote. Mtu hatotajiwa madhambi yale tena Siku ya Qiyaamah. Na madhambi hufutwa kutoka katika diwani ya waandishi watukufu (Kiraaman Kaatibiyna). Bali si hivyo tu, bali husahaulisha katika nyoyo zao ili wasione aibu pindi zitajwapo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ﴿٣٩﴾

Allaah Anafuta yale Ayatakayo na Anathibitisha (Ayatakayo), na Kwake kiko Ummul-Kitaab. [Ar-Ra’d (13:39)]

 

 

Na Huthibisha sehemu yake ile na kwa kila ovu moja zuri. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda amali njema. Basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Furqaan (25:70)][1]

 

 

Na kwa ujumla ni kuwa, msamaha unakuwa ni kwa kuacha wajibu, na maghfira ni kwa kufanya yaliyokatazwa.[2]

 

 

ii-Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ni Mwenye kheri nyingi, Hutoa mengi na fadhila zaka hazikatiki[3] iwe katikati ya usiku au mwishoni mwa mchana.

 

iii-Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hukubali msamaha ambao ni mwepesi[4] kwa kuwepesisha majukumu kwa waja Wake, pindi inapotokea mapungufu kwa mtu na udhaifu, kwa mfano, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewajibisha udhu kwa anayetaka kuswali, basi pindi unapotenguka udhu wake akakosa maji, Humtaka afanye tayammum, Akichunga udhaifu wa waja Wake.[5]

 

 

iv-Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ni Mwenye kutoa msamaha na Ambaye Anakubali tawbah na Anatoa malipo pamoja na mtu kuwa amefanya madhambi na kustahiki adhabu.

 

 

v-Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ni Mwenye kusamehe na husahilisha mambo ya kheri, na huyakurubisha mambo hayo ya kheri kwa watu na kwa njia nyepesi, kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hana baina Yake na waja Wake pazia yoyote ile.

 

 

vi-Na miongoni mwa ukamilifu wa msamaha Wake ni kwamba, athari za msamaha Wake umeenea kwa watu wote iwe ni usiku au ni mchana, hivyo msamaha na maghfira Yake yameenea kwa viumbe vyote, kwa wenye dhambi na waliopetuka mipaka.[6] Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا ﴿٤٣﴾

Hakika Allaah daima Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria. [An-Nisaa (4:43)]

 

vii-Miongoni mwa misamaha Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ni kwamba juu ya kuwa upungufu wa waja unapelekea kupata adhabu mbali mbali (adhabu za ndani na za nje), lakini msamaha wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na maghfira Yake unakataza adhabu hizi (Rejea iliyotangulia.)

 

Na msamaha wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) upo aina mbili:

 

a-Msamaha wa jumla kwa wakosefu wote, makafiri na wengineo, ili kulipa adhabu zilizowekwa sababu zake, na ambazo zinapelekea katika kukatika kwa neema kwao, wao wanamuudhi Rabb wao kwa kumtukana na kumshirikisha na mengineyo katika makosa, Naye Anawasamehe na huwapa riziki na huwapelekea neema mbali mbali zilizo nje na ndani na huwafungulia kwao dunia na huwapa manufaa na huwasubirisha kwa msamaha Wake na uvumilivu Wake.

 

b-Msamaha maalum na maghfira Yake kwa waliotubia, na walioomba maghfira, na wenye kuomba na waliopatwa na majanga na wakaweza kusubiri katika Uislamu.

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-‘Afuww:

 

1-Omba msamaha daima kwa Al-‘Afuww kwa kukumbuka kwamba, Yeye ni Mwenye Kusamehe makosa na madhambi mengi kama Anavyosema:

 

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ﴿٣٠﴾

Na msiba wowote unaokusibuni, basi ni kwa sababu ya yale iliyochuma mikono yenu, na Anasamehe mengi. [Ash-Shuwraa (42:30)]

 

2-Samehe wenzako pindi wanapokukosea kwa kukumbuka kwamba, ikiwa Al-‘Afuww Anasemehe waje Wake, basi vipi binaadam wasisameheane?

 

3-Utakaposamehe wenzako makosa yao au dhulma zao juu yako, basi Naye Al-‘Afuww Atakusamehe makosa na madhambi yako. Kwa hiyo Pendelea kumsamehe nduguyo Muislamu anapokukosea. Tuna funzo la hili katika kisa cha ifk (kusingiziwa kashfa Mama wa Waumini ‘Aaishah Radhwiya-Allaahu ‘anhaa). Aayah ziliteremshwa kumsafisha na kumtoharisha kutokana na tuhuma hizo. Na katika Aayah hizo, ni Aayah aliyoteremshiwa baba yake Abu Bakr (Radhwiya-Allaahu ‘anahu) ambaye aligoma kuendeleza kumpa swadaqa jamaa yake Mistwah bin Uthaathah, ambaye alikuwa miongoni mwa waliovumisha tuhuma hizo. ‘Aaishah (Radhwiya-Allaahu ‘anhaa) amehadithia kisa hicho kwa urefu; na katika maelezo yake akasema:  “Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaah ‘anhu) ambaye alikuwa akimkimu kimaisha Mistwah bin Uthaathah kutokana na ukaraba, alisema: “Wa-Allaahi, sitompa Mistwah chochote kamwe baada ya hayo aliyoyasema kuhusu ‘Aaishah.” Na hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akateremsha:

 

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ 

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [An Nuwr (24:22)]

 

Abu Bakr (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) akasema: Na’am, Wa-Allaahi, mimi hakika napenda Allaah Anighufirie. Akamrejeshea Mistwah fedha za matumizi alizokuwa anampa.   [Al-Bukhaariy]

 

Na katika Kauli Yake nyengine Al-‘Afuww, Anaamrisha na kuahidi maghfirah kwa anayesamehe wenzake:

 

وَإِن تَعْفُوا وَتَصْفَحُوا وَتَغْفِرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٤﴾

Na mkisamehe na mkapuuza na mkayafutilia mbali, basi hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [At-Taghaabun (64:14)]

 

 

4-Ukitaka kufikia daraja ya Muhsin, basi pendelea kuwa na sifa zilizotajwa katika Aayah ifuatayo, ikiwemo sifa ya kusamehe wanaokukosea. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾ 

Ambao wanatoa (kwa ajili ya Allaah) katika hali ya wasaa na katika hali ya shida, na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Aal-‘Imraan (3:134)]

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema  tena kwamba kusamehe kunapelekea katika daraja ya Muhsin, na kwamba Yeye Al-‘Afuww Anawapenda wenye kufanya ihsaan.

 

فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاصْفَحْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣﴾

Basi wasamehe na achilia mbali. Hakika Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Al-Maaidah (5:13)

 

 

5-Kusamehe, hakumaanishi kwamba mtu anajidhalilisha, bali kunazidisha hadhi kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ،  وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إلاَّ عِزًّا، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ عَزَّ وَ جَلَّ)) مسلم

                                                                                                

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  “Kutoa swadaqa hakupunguzi mali, Allaah Humzidishia mja ‘izzah (hadhi, daraja ya juu mbele ya Allaah) kwa ajili ya kusamehe kwake.  Na   yeyote anayenyenyekea kwa ajili ya Allaah, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atampandisha Daraja (Atamtukuza).  [Muslim]

 

 

6-Japokuwa inaruhusika kulipiza dhulma, lakini kusamehe kuna ujira mkubwa mbele ya Al-‘Afuww, Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَالَّذِينَ إِذَا أَصَابَهُمُ الْبَغْيُ هُمْ يَنتَصِرُونَ﴿٣٩﴾

Na wale wanapokabiliwa na baghi (ukandamizaji na dhulma), wao wanajitetea.

 

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ﴿٤٠﴾

 

Na jazaa ya uovu ni uovu mfano wake. Lakini atakayesamehe na akajenga mahusiano mema na aliyemkosea, basi ujira wake uko kwa Allaah. Hakika Yeye Hapendi madhalimu. [Ash-Shuwraa (42:39-40]

 

 

7-Kusameheana kwa wanandoa wanapofikishana katika talaka pia kuna fadhila, nayo ni kuwa karibu zaidi na taqwa kama Anavyosema Al-‘Afuww:

 

وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إِلَّا أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ ۚ وَأَن تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۚ وَلَا تَنسَوُا الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٢٣٧﴾ 

Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha, isipokuwa wakisamehe au asamehe yule ambaye fungamano la ndoa liko mikononi mwake. Na kusamehe kuko karibu zaidi na taqwa. Na wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kuona myatendayo. [Al-Baqarah (2:237)]

 

 

8-Muombe daima Al-‘Afuww Akusamehe, ikiwa katika ibaada zako, na khasa katika Masiku kumi ya mwisho ya Ramadhwaan kwa kuwa imethibiti duaa adhimu ya kuomba msamaha katika Laylatul-Qadr:

 

 عن عَائِشَةَ، قالَتْ: قُلْتُ: يا رَسُولَ اللهِ، أرَأيْتَ إنْ عَلِمْتُ أيُّ لَيْلَةٍ لَيْلَةُ الْقَدْرِ، مَا أقُولُ فِيها؟ قَالَ: ((قُولي: اللَّهُمَّ إنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ العَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي)).

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba amesema: “Ee Rasuli wa Allaah! Nieleze ikiwa nitajua usiku fulani ndio wa Laylatul-Qadr, niseme nini?” Akasema: ((Sema:

اللَّهُمَّ إنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ العَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa fa'fu 'anniy.” (Ee Allaah Hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe, Unapenda kusamehe basi Nisamehe)) [An-Nasaaiy, Sunan Al-Kubraa (7712) Ibn Maajah (3850), Ahmad (25384)]

 

 

Omba duaa nyenginezo zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Miongoni mwazo ni zifuatazo:

 

Kauli Yake Al-‘Afuww:

 

وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا

Na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe Ni Mawlaa wetu. [Al-Baqarah (2:286)]

 

 Na katika Sunnah:

 

 اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي، وَاهْدِنِي، وَارْزُقْنِي، وَعَافِنِي ، أَعُوذُ بِاللَّهِ مِنْ ضِيقِ الْمَقَامِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ

Allaahumma-ghfirliy wahdiniy, warzuqniy, wa ‘aafiniy, a’uwdhu biLLaahi min dhwiyqil-maqaami Yawmal-Qiyaamah

 

Ee Allaah, nighufurie, nihidi, niruzuku, nisamehe, najikinga kwa Allaah dhidi ya dhiki ya kisimamo Siku ya Qiyaamah [Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah. -  Swahiyh An-Nasaaiy (1/356), Swahiyh Ibn Maajah (1/226)]

 

Na katika duaa alizokuwa akiomba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika nyiradi za asubuhi na jioni. 

 

اللّهُـمَّ إِنِّـي أسْـأَلُـكَ العَـفْوَ وَالعـافِـيةَ في الدُّنْـيا وَالآخِـرَة، اللّهُـمَّ إِنِّـي أسْـأَلُـكَ العَـفْوَ وَالعـافِـيةَ في ديني وَدُنْـيايَ وَأهْـلي وَمالـي، اللّهُـمَّ اسْتُـرْ عـوْراتي وَآمِـنْ رَوْعاتـي، اللّهُـمَّ احْفَظْـني مِن بَـينِ يَدَيَّ وَمِن خَلْفـي وَعَن يَمـيني وَعَن شِمـالي، وَمِن فَوْقـي، وَأَعـوذُ بِعَظَمَـتِكَ أَن أُغْـتالَ مِن تَحْتـي

Allaahumma inniy as-alukal ‘aafiyah fid-dun-yaa wal Aakhirah. Allaahumma inni as-alukal ‘afwa wal ‘aafiyata fiy Diyniy wa dun-yaaya, wa ahliy, wa maaliy. Allaahumma-stur ‘awraatiy, wa-aamin raw’aatiy. Allaahumma-hfadhwniy min bayni yadayya, wamin khalfiy, wa ‘an yamiyniy, wa ‘an shimaaliy, wamin fawqiy, wa a’uwdhu bi’adhwamatika an ughtaala min tahtiy

 

Ee Allaah, hakika nakuomba msamaha na Al’-Aafiyah (hifadhi ya kila shari, amani, salama) duniani na Aakhirah. Ee Allaah, hakika nakuomba msamaha na Al’-Aafiyah katika Dini na dunia yangu, na ahli wangu, na mali yangu. Ee Allaah nisitiri aibu zangu na nitulize khofu yangu. Ee Allaah, nihifadhi mbele yangu, na nyuma yangu, na kulia kwangu, na kushoto kwangu, na juu yangu, na najikinga kwa Uadhimu Wako kwa kutekwa chini yangu.  [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ’anhu) Swahiyh Ibn Maajah (2/332), Swahiyh Abiy Daawuwd (5074)].  

 

 

 

 

[1] Angalia sherehe ya Asmaau-Allaahil-Husnaa cha Ar-Raaziy (340).

[2] Sherehe ya Al-Waasitwiyyah cha Imaam Ibn ‘Uthaymiyn  (2/92).

[3] Angalia Al-Iitiqaad cha Al-Bayhaqiy Uk (56).

[4] Tafsiyr ya Al-Qurtwubiy  (3/213).

[5] Rejea Asamaau-Allaahil-Husnaa cha Dr ‘Umar Al-Ashqar Uk. (255).

[6] Angali Fat-hur-Rahiym Uk. (27).

 

 

 

 

Share