02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Kinachofaa Kutolewa Kama Mahari

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الصَّدَاقُ

 

Mahari

 

Alhidaaya.com

 

 

 

02:  Kinachofaa Kutolewa Kama Mahari:

 

1-  Ni kila kinachofaa kuwa thamani katika mauzo au manunuzi. 

 

Kinachotolewa ni sharti kiwe kinabeba thamani, kiwe twahara, kiwe halali, kiwezekanike kupatiwa manufaa, au kiwe chenye kuweza kukabidhika kama fedha, vitu na kadhalika.  Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ أَن تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ"

 

“Na mmehalalishiwa wengineo wasiokuwa hao, mtafute (kuwaoa) kwa mali zenu mkijistahi pasi na kuzini”.  [An-Nisaa: 24]

 

2-  Kazi ya kuweza kulipwa: 

 

Kazi kama hii inafaa kuwa mahari.  Ni kama kufundisha Qur-aan, kutengeneza bidhaa, kutoa huduma na kadhalika.  Ni madhehebu ya Shaafi’iy na Ahmad, Abuu Haniyfah amelikataa hili, na Maalik kalikirihisha.

 

Lililo sahihi ni kujuzu.  Allaah Ta’aalaa Ametuhadithia katika Qur-aan kisa cha mzee mwema aliyemwozesha Muwsaa (‘alayhis salaam) mmoja ya binti zake wawili, na akaifanya kazi ya kumtumikia kwa muda wa miaka minane iwe ndiyo mahari ya binti.  Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ ۖ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ"

 

“Akasema:  Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili kwa sharti kuwa unitumikie miaka minane; ukitimiza kumi, basi ni uamuzi wako”.  [Al-Qaswas: 27]

 

Na hii ni kwa mujibu wa ‘Ulamaa waliosema kwamba sharia za waliopita kabla yetu ni sharia ambazo zinatuhusu pia sisi mpaka iwepo dalili ya kuonyesha kwamba hazituhusu.

 

Na nyuma tumeielezea Hadiyth kuhusiana na mwanamke aliyejinadi mwenyewe kwa Rasuli ili amwoe bure bila mahari, lakini Rasuli hakumjibu kitu, kisha akajitokeza mtu kutaka kumwoa badala yake, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: 

 

"اذْهَبْ، فَقَدْ زَوَّجْتُكَهَا بِمَا مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ"

 

“Nenda, nishakuozesha yeye kwa Qur-aan uliyoihifadhi”, lakini kwa taawili ya kwamba makusudio ni amfundishe suwrah moja ya Qur-aan au zaidi.

 

3-  Kumwacha huru kijakazi:

 

Toka kwa Anas, amesema: 

 

"أَعْتَقَ رَسُولُ اللَّهِ صلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَفِيَّةَ وَجَعَلَ عِتْقَهَا صَدَاقَهَا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwacha huru Swafiyyah na akakufanya kumwacha huru huko kuwa ndiyo mahari yake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Daawuwd, hawa ndio waliojuzisha kuachwa huru kuweza kuwa mahari.  Lakini Fuqahaaul Amswaar (Fuqahaa saba wa Madiynah wa enzi hizo) wamelipinga hili kwa kuwa linapingana na usuwl.  Wanasema sababu ni kwamba kuacha huru ni kuvua umiliki, na kuvua huku hakujumuishi kupatiwa manufaa kwa jambo jingine lolote, kwani, kijakazi huyo akiachwa huru, hapo hapo anajimiliki mwenyewe, sasa vipi alazimikiwe kuolewa kwa hilo?  Ama kwa Hadiyth, wamesema kwamba la Rasuli na Swafiyyah, hilo ni jambo mahsusi kwake na si kwa wengine, kwani kuna mengi yahusuyo ndoa ambayo ni mahsusi kwake tu.

 

Ninasema:  “Inavyoonekana kwa picha ya nguvu ni kwamba kuachwa huru kunajuzu kuwa mahari kutokana na Hadiyth iliyotangulia.  Na asili ya matendo ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni yawe kiigizo na kielelezo kwetu isipokuwa kwa yale ambayo yana dalili ya umahususi kwake kama kumwoa mwanamke aliyejitolea kwake mwenyewe bila mahari au kuoa zaidi ya wanawake wanne.  Na hayo waliyoyaelezea ya kupingana na uswuwl hayakinzaniwi kwayo Hadiyth hii.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

4-  Kusilimu Mume

 

Anas amesema: 

 

"تَزَوَّجَ أَبُو طَلْحَةَ أُمَّ سُلَيْمٍ، فَكَانَ صَدَاقُ مَا بَيْنَهُمَا الْإِسْلَامَ، أَسْلَمَتْ أُمُّ سُلَيْمٍ قَبْلَ أَبِي طَلْحَةَ فَخَطَبَهَا فَقَالَتْ: إِنِّي قَدْ أَسْلَمْتُ فَإِنْ أَسْلَمْتَ نَكَحْتُكَ فَأَسْلَمَ فَكَانَ صدَاقَ مَا بَينهمَا"

 

“Abu Twalha alimwoa Ummu Sulaym, na mahari kati yao ilikuwa ni kusilimu.  Ummu Sulaym alisilimu kabla ya Abu Twalha.  Abu Twalha akamposa, lakini akamwambia:  Mimi nimesilimu, na kama na wewe utasilimu, basi nitakubali unioe.  Akasilimu, na kukawa ndio mahari kati yao”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na An-Nasaaiy (6/114)]

 

Hadiyth hii ni hoja kwa waliojuzisha kusilimu mwanaume kuwa mahari yake.  Lakini Muhammad bin Hazm amepinga kuitolea Hadiyth hii dalili kwa mambo mawili: 

 

La kwanza:  Hilo lilikuwa kabla ya kuhamia Madiynah kwa muda, na Abu Twalha alikuwa amesilimu kitambo.  Yeye ni katika watu wa mwanzo wa Madiynah kusilimu, na wala halikuwa bado limeshuka wajibisho la kuwapa wanawake mahari.

 

La pili:  Hakuna katika taarifa hii lolote linalojulisha kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ana habari nalo.

 

 

Share