03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Kiwango Cha Juu Zaidi Na Cha Chini Zaidi Cha Mahari

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الصَّدَاقُ

 

Mahari

 

Alhidaaya.com

 

 

 

03:  Kiwango  Cha Juu Zaidi Na Cha Chini Zaidi Cha Mahari :

 

 

1-  Hakuna mpaka wa kiwango cha juu zaidi cha mahari.  ‘Ulamaa wote -bila ya kupinga hata mmoja wao- wamekubaliana kwamba mahari anayolipa mwanamume kwa mkewe hayana mpaka wa kiwango cha juu.

 

Sheikh wa Uislamu amesema:  “Mwenye uwezo na mwenyewe akapenda kumpa mkewe mahari mengi, basi hakuna ubaya.  Ni kama Alivyosema Allaah Ta’aalaa:

 

"وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا"

 

Na mmempa mmoja wao mirundi ya mali, basi msichukue kutoka humo chochote”.  [An-Nisaa: 20]

 

2-  Na pia hakuna mpaka wa kiwango cha chini zaidi cha mahari kwa kauli yenye nguvu.  Mahari yanafaa kwa kila kile ambacho kinaweza kuitwa mali, au kinachotiwa thamani kwa mali madhali tu yapo maridhiano kati ya mke na mume.  Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Abu Thawr, Al-Awzaaiy, Al-Layth, Ibn Al-Musayyib na wengineo.  Na Ibn Hazm kafikia kujuzisha kila kile chenye nusu hata punje ya shayiri.  Dalili zinazotilia nguvu rai hii ya kutokuwepo mpaka wa kiwango cha chini kabisa cha mahari ni hizi zifuatazo:

 

(a)  Ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ أَن تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ"

 

“Na mmehalalishiwa wengineo wasiokuwa hao, mtafute (kuwaoa) kwa mali zenu mkijistahi pasi na kuzini”.  [An-Nisaa: 24]

 

Na hii ni kwa mali nyingi au kidogo.

 

(b)  Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa yule aliyetaka kumwoa mwanamke aliyejitolea aolewe na yeye bila mahari:

 

"اذْهَبْ فَاطْلُبْ وَلَوْ خَاتَمًا مِنْ حَدِيدٍ" 

 

“Nenda ulete hata pete ya chuma”.  [Imetajwa nyuma]

 

Hadiyth inaonyesha kwamba mahari yanafaa kwa kila kile kinachoitwa mali.

 

Bali mahari yanafaa kwa kila kile chenye thamani ya kugusika au isiyo ya kugusika.  Na hili ndilo ambalo dalili zinakutana kwalo na kukubaliana na maana sahihi ya uhalali wa mahari, kwani makusudio ya mahari si kutolewa mali tu, bali mahari ni alama ya utashi na nia ya kweli ya mwanaume ya kumwoa mwanamke. Na mahari hii hutolewa zaidi ikiwa mali, na pia kwa kila kile chenye thamani isiyogusika madhali mke yuko radhi nayo (kama kufundishwa Qur-aan na kadhalika). 

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwozesha mtu kwa Qur-aan aliyoihifadhi, mahari ya Abu Twalha kumwoa Ummu Sulaym ikawa ni yeye kusilimu, na Rasuli akakufanya kumwacha huru Swafiyyah ndio mahari yake.  Kunufaika kwa Qur-aan, elimu na kusilimu mume, na Bi Swafiyyah kunufaika kwa kupata uhuru wa kujimiliki mwenyewe, yote hayo yamekuwa ni mahari.  Na hii yote ikiwa mwanamke mwenyewe ataridhia, kwani kiasili, mahari ni haki yake.

 

Kupandisha Kiwango Cha Mahari Kupita Kiasi:

 

Si katika Uislamu tabia hii iliyotawala kwenye vichwa vya baadhi ya watu ya kutoza mahari ya juu kupita kiasi mpaka kufikia watu mara wanapotoka kwenye mnasaba wa ndoa, kuwa hawana jingine wanalolizungumzia isipokuwa mahari ya juu waliyoisikia.  Wanakuwa kama vile wametoka kwenye mnada wa kuuza bidhaa.

 

Mwanamke siyo bidhaa kwenye soko la ndoa mpaka watu wagandamane na tabia hii ya uchu wa mali ambayo matokeo yake yanakuwa ni mabaya kama tunavyoona katika picha hizi zifuatazo:

 

1-  Inawafanya vijana wengi kukimbia ndoa na wasichana wengi pia kubakia bila kuolewa.

 

2-  Mmomonyoko wa tabia huwakumba wasichana na wavulana wakati wanapokata tamaa ya ndoa, na hivyo kutafuta mbadala wa hilo.

 

3-  Magonjwa ya kisaikolojia huwapata wavulana na wasichana kutokana na mkwamo na matumaini yao kugonga mwamba.

 

4-  Watoto wengi huacha kuwasikiliza wazazi wao na wanaziasi desturi na tabia njema za vizazi na vizazi.

 

5-  Mwanaume akilipishwa mahari ya kumzidi uwezo wake, huzalikana uadui na uhasama kwenye moyo wake dhidi ya mkewe na watu wake.

 

Yanayotakiwa Kuhusiana Na Suala Hili:

 

1-  Ni kupunguza na kutopandisha.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"خَيْرُ الصَّدَاقِ أَيْسَرُهُ"

 

“Mahari yenye kheri zaidi ni yale yaliyo kidogo zaidi.”  [Mustadrak Al-Haakim (2/182)]

 

Ibn Al-Qayyim amesema:  “Kuweka mahari ya bei ya juu mno ni makruhu katika ndoa, hupunguza baraka ya ndoa na huleta ugumu”.

 

‘Umar bin Al-Khattwaab amesema:

" أَلَا لَا تُغْلُوا صُدُقَ النِّسَاءِ أَلَا لَا تُغْلُوا صُدُقَ النِّسَاءِ فَإِنَّهَا لَوْ كَانَتْ مَكْرُمَةً فِي الدُّنْيَا أَوْ تَقْوَى عِنْدَ اللَّهِ كَانَ أَوْلَاكُمْ بِهَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَا أَصْدَقَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ امْرَأَةً مِنْ نِسَائِهِ وَلَا أُصْدِقَتْ امْرَأَةٌ مِنْ بَنَاتِهِ أَكْثَرَ مِنْ ثِنْتَيْ عَشْرَةَ أُوقِيَّةً وَإِنَّ الرَّجُلَ لَيُبْتَلَى بِصَدُقَةِ امْرَأَتِهِ وَقَالَ مَرَّةً وَإِنَّ الرَّجُلَ لَيُغْلِي بِصَدُقَةِ امْرَأَتِهِ حَتَّى تَكُونَ لَهَا عَدَاوَةٌ فِي نَفْسِهِ وَحَتَّى يَقُولَ كَلِفْتُ إِلَيْكِ عَلَقَ الْقِرْبَةِ "

 

“Zindukeni!  Msipandishe juu mahari za wanawake.  Zindukeni!  Msipandishe juu mahari za wanawake.  Kwani, lau kama lingelikuwa ni jambo lenye kumletea mtu utukuzo duniani, au kuwa ndio uchamungu mbele ya Allaah, basi Rasuli angelikuwa ndiye anastahiki zaidi kulifanya hilo kuliko nyinyi.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakulipa mahari za wake zake, wala hakuna yeyote katika mabinti zake aliyelipiwa mahari ya zaidi ya uqiya 12 (dirham 480).  Na kwa hakika mtu anaweza kuingia kwenye matatizo makubwa kutokana na mahari ya mkewe.  Na akasema mara nyingine:  Mtu kwa hakika atamlipa mke wake mahari nyingi kisha hilo likazalisha uadui ndani ya nafsi yake na kujikuta akijiambia mwenyewe:  Umenifilisi kila kitu mpaka kamba ya kutundikia kiriba changu”.  [Ni Swahiyh.  Abu Daawuwd (2106), At-Tirmidhiy (1114), An-Nasaaiy (6/117), na Ibn Maajah (1887)]

 

Bibi ‘Aaishah alipoulizwa kuhusu kiasi cha mahari ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu: 

 

"كَانَ صَدَاقُهُ لأَزْوَاجِهِ ثِنْتَىْ عَشْرَةَ أُوقِيَّةً وَنَشًّا.‏ قَالَتْ أَتَدْرِي مَا النَّشُّ؟ قَالَ قُلْتُ لاَ.‏ قَالَتْ نِصْفُ أُوقِيَّةٍ‏.‏ فَتِلْكَ خَمْسُمِائَةِ دِرْهَمٍ، فَهَذَا صَدَاقُ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم لأَزْوَاجِهِ‏."

 

“Mahari ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wakeze yalikuwa ni uqiya 12 na nash.  Akauliza:  Unajua nash ni kiasi gani?  Nikasema:  Sijui.  Akasema:  Ni nusu uqiya,  kwa hivyo hizo ni dirhamu 500.  Na haya ndiyo mahari ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wakeze”.  [Muslim (1426), An-Nasaaiy (6/116) na Ibn Maajah (1886)]

 

Sheikh wa Uislamu amesema:  “Na yule ambaye nafsi yake itamghilibu kuzidisha mahari ya binti yake zaidi ya mahari ya mabinti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao wao ndio viumbe walio bora zaidi wa Allaah juu ya wanawake wa walimwengu katika kila sifa, au kuliko mahari za Mama za Waumini, basi mtu huyo ni jaahil na mpumbavu.  Na hii ni pamoja na uwezo na wasaa.  Ama aliye masikini na mfano wake, huyo hatakiwi kumpa mwanamke kile ambacho hana uwezo wa kukilipa na kujibebesha mwenyewe mazito”. 

 

2-  Ikiwa kupandisha juu sana mahari ni uzito na taklifu kwa mume, basi hilo linakuwa ni lenye kulaumiwa.

 

Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza mtu ambaye amekusudia kumwoa mwanamke wa Kianswaar:

 

"عَلَى كَمْ تَزَوّجْتَهَا؟  قَالَ: عَلَى أَرْبَعِ أَوَاقٍ، فَقَالَ لَهُ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: عَلَى أَرْبَعِ أَوَاقٍ؟  كَأَنّمَا تَنْحِتُونَ الفِضَّةَ مِنْ عُرْضِ هذَا الجَبَلِ"

 

“Utamwoa kwa mahari kiasi gani?  Akasema:  Kwa uqiya nne.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Kwa uqiya nne (mbona nyingi sana)?!  Kana kwamba mnachimba fedha toka kwenye kina cha mlima huu“.  [Muslim (1424) na An-Nasaaiy (6/69)]

 

Toka kwa Abu Hadrad Al-Aslamiy, amesema:

 

" أتَيتُ رسولَ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّمَ أَسْأَلُهُ في صَدِاقٍ، فَقَالَ: كَمْ أَصْدَقْتَ؟ قُلْتُ: مِئَتَيْ دِرهَمٍ، قَالَ: لَوْ كُنْتُمْ تَغرِفونَ مِن بُطحانَ، لمَا زادَ"

 

“Nilimwendea Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwomba anisaidie mahari.  Akaniuliza:  Umepanga kutoa kiasi gani?  Nikamjibu:  Dirhamu 200.  Akasema:  Hata mngelikuwa mnachota (dirham) toka kwenye bonde (kama maji), isingelipendeza kuzidi zaidi ya hizo”.  [Ahmad (3/448) na Al-Bayhaqiy (7/235) kwa Sanad swahiyh]

 

Katika Hadiyth hizi mbili, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapinga na kushangaa wanaume hawa kutozeshwa mahari kubwa wakati hali zao za kifedha ni ngumu.  Lakini yeye kama ilivyoelezwa hapo nyuma, aliwaozesha mabanati zake na kulipa kwa wake zake mahari zaidi ya hizo, na hii ni kwa mujibu wa uwezo wake yeye na wale waliowaoa mabanati zake.

 

3-  Ikiwa mtu ni tajiri mwenye uwezo, basi anaweza kutoa mahari nyingi awezayo kwa mkewe.

 

"فَقَدْ زَوَّجَ النَّجَاشِيُّ أُمَّ حَبِيْبَةَ لِرَسُوْلِ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَأَمْهَرَهَا عَنهُ أَرْبَعَة آلَاف وَبَعَثَ بِهَا إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَعَ شُرَحْبِيل بن حَسَنَة"

 

“Negus (An-Najaashiy, Mfalme wa Uhabeshi) alimwozesha Ummu Habiybah kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamlipia mahari ya dirhamu elfu nne [mahari za wakeze Rasuli zilikuwa ni dirhamu mia nne tu], kisha akampeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiandamana na Shurahbiyl bin Hasanah”.  [Hadiyth Swahiyh.  Abu Daawuwd (2107), Ahmad (6/427) na An-Nasaaiy (6/119)]

 

Toka kwa Ash-Sha’abiy amesema:  “ ‘Umar bin Al-Khattwaab aliwahutubia watu.  Akaanza kwa kumhimidi Allaah na kumsifu, kisha akasema:  Zindukeni!  Msipandishe juu mahari za wanawake, kwani hainifikii mimi habari kuhusu yeyote aliyetoza mahari zaidi ya mahari aliyotoza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au aliyoletewa, isipokuwa ninaichukua ziada na kuiingiza kwenye Baytul Maal.  Kisha akateremka, lakini hapo hapo mwanamke mmoja wa Kiquraysh alimpinga na kumwambia:  Ee Amiri wa Waumini!  Je, Kitabu cha Allaah ‘Azza wa Jalla kina haki zaidi kufuatwa au maneno yako?  Akasema:  Bali ni Kitabu cha Allaah ‘Azza wa Jalla.  Kwani kuna shida gani?  Akamwambia:  Wewe sasa hivi umewakataza watu kupandisha juu sana mahari ya wanawake nailhali Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema katika Kitabu Chake: 

 

"وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا"

 

“Na mmempa mmoja wao mirundi ya mali, basi msichukue humo chochote”,  ‘Umar akamwambia:  Kila mmoja ni mjuzi zaidi kuliko ‘Umar -mara mbili au tatu-  Kisha akapanda tena mimbari na kuwaambia watu:  Hakika nilikuwa nimewakataza kupandisha sana mahari ya wanawake.  Basi na afanye mtu katika mali yake analoliona sawa”.  [Sunan Sa’iyd bin Mansuwr (598), na toka kwake Al-Bayhaqiy (7/233).  Ni Hadiyth Hasan Lighayrihi, na ina Hadiyth wenza kama ilivyobainishwa kwenye Kitabu cha Jaami’u Ahkaamin Nisaa (3/301)].

 

Kiufupi:  Ni kwamba watu wanatofautiana katika utajiri na umasikini.  Hivyo basi ni lazima kuchunga hali ya mwoaji.  Asitakwe asichokuwa na uwezo nacho hadi kulazimika kwenda kukopa na mfano wa hivyo.  Lakini kama ana uwezo, basi si vibaya akizidisha, isipokuwa tu hilo lisikutanishwe na niya ya kujifaharisha na mfano wa hivyo, hapo itakuwa ni jambo baya.

 

 

 

Share