05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Aina Za Mahari: (a) Mahari Yaliyobainishwa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الصَّدَاقُ

 

Mahari

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

05:  Aina Za Mahari: (a)  Mahari Yaliyobainishwa:

 

 

Kwa kuzingatia makubaliano kuhusu thamani yake, mahari yanagawanyika katika yaliyobainishwa na yasiyobainishwa.  

 

Ama kwa kuzingatia muda wa kulipwa kwake, yanagawanyika katika yanayolipwa kwa wakati na yanayolipwa baadaye.

 

Ama kwa kuzingatia kiasi ambacho mwanamke anastahiki kulipwa, yanagawanyika katika mahari kamili, nusu mahari na kiliwazo.

 

Mahari Yaliyobainishwa:

 

1-  Inapendeza kwa wafungao ndoa kupanga mahari, kuyabainisha na kuyaainisha ili kuepusha mizozo na migogoro.  Baada ya kupatana, mahari iliyokubaliwa inakuwa juu ya dhima ya mume ambaye ni lazima ailipe.

 

2-  Inajuzu kufunga ‘aqdi bila kutaja mahari kama linavyoashiria Neno Lake Ta’aala:

 

"لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِنْ طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً"

 

“Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia mahari yao”.  [Al-Baqarah:  236]

 

Hii inaitwa “Nikaahut-Tafwiydh”, nayo inajuzu kwa ‘Ijmaa ya ‘Ulamaa.  Katika hali hii, mwanamke ni lazima apewe mahari ya mfano wake.  Mahari ya mfano wake ni kiasi ambacho wanawake mfano wake katika jamaa zake toka upande wa baba yake kama madada na mashangazi wamelipwa, lakini si kutoka upande wa mama yake.  Kwa kuwa mama anaweza kutoka kwenye familia ambayo desturi zake zinapishana na desturi za familia ya baba yake.  Na kama hawatapatikana mfano wake toka kwa baba yake, basi ni wanawake wa mfano wake katika mji wake.

 

 

 

Share