06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Aina Za Mahari: (b) Mahari Inayolipwa Kwa Wakati Bila Kucheleweshwa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
06: Aina Za Mahari: (b) Mahari Inayolipwa Kwa Wakati Bila Kucheleweshwa:
Kiasili, mahari hukabidhiwa mara moja kwa mwanamke kabla ya mumewe kumuingilia, na mwanamke huyu ana haki ya kukataa kuingiliwa na mumewe mpaka apokee mahari yake. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَنْ تَنكِحُوهُنَّ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ" ۚ
“Na wala si dhambi kufunga nao nikaah mkiwapa mahari yao”. [Al-Mumtahinah: 10]
Imepokelewa toka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) akisema:
تزوَّجْتُ فَاطِمَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهَا، فَقُلْتُ: يَا رَسُوْلَ اللهِ، ابْنِ بي، قَالَ: أَعْطِهَا شَيْئًا، قُلْتُ: مَا عِنْدِيْ مِنْ شَيْءٍ، قَالَ: فَأَيْنَ دِرْعُكَ الحُطَمِيَّةُ؟ قُلْتُ: هِيَ عِنْدِي، قَالَ: فَأَعْطِهَا إيَّاهُ"
“Nilimwoa Faatwimah (Radhwiya Allaah ‘anhaa). Kisha nikamwambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Naomba niruhusu nimuingilie. Akaniambia: Mpe chochote. Nikasema: Sina kitu. Akaniambia: Liko wapi deraya lako la kihutwamiyya? Nikamwambia: Ninalo. Akaniambia: Basi mpe (hilo hilo)”. [Hasan Swahiyh. Swahiyh An-Nasaaiy (3375)]
Na hili limekwishafanywa na watangu wema.
Lakini pamoja na hivyo, inajuzu kuchelewesha mahari au sehemu yake, au hata kuilipa kidogo kidogo kama hali ya mume hairuhusu au kuwepo sababu nyingine yeyote lakini kwa sharti mume na mke wakubaliane kucheleweshwa huko baada ya mke kuingiliwa na mumewe. Kwa kuwa mahari ni deni kama yalivyo madeni mengineyo, hivyo basi inajuzu kulipwa baadaye ingawa inapendeza zaidi ikilipwa haraka.
Lakini Je, Ni Sharti Kuainishwa Muda Wa Kulipa Ikiwa Mahari Yatacheleshwa?
1- Ikiwa yatacheleweshwa muda usiojulikana, kama mume kusema: “Nimekuoa kwa mahari ya milioni moja kwa sharti niwe na uwezo wa kuyalipa, au nitayalipa wakati wa kuvuma upepo, au kuwasili fulani na mfano wa hayo”, basi haitofaa kucheleweshwa.
2- Mahari yakicheleweshwa yote au baadhi yake bila kutajwa au kuainishwa muda wa kulipwa, hapa kuna mvutano baina ya Fuqahaa:
(a) Mahanafiy na Mahanbali wamesema: Uhalali wa mahari utabakia pale pale kwa mwanamke na haki ya kupewa pia itabaki atakapotalikiwa au mumewe akifariki kama ilivyo ada na desturi kwenye nchi za Kiislamu!!
(b) Mashaafi’iy wamesema: Uhalali wa mahari unakuwa haupo tena, na badala yake atapewa mahari ya mfano.
(c) Wamaalik wamesema: Ikiwa muda wa kulipwa haujulikani, kama kucheleweshwa hadi mume kufa au kuachana, basi ‘aqdi itakuwa ni lazima ivunjwe isipokuwa kama mume atamuingilia mke, hapo italazimu mahari ya mfano.