07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake: Hali Zinazolazimu Apewe Mahari Kamili (a) Akiingiliwa Na Mume Jimai Halisia

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الصَّدَاقُ

 

Mahari

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

07:  Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake:  Hali Zinazolazimu Apewe Mahari Kamili  (a)  Akiingiliwa Na Mume Jimai Halisia:

 

 

 

‘Ulamaa wamekubaliana wote kwamba mwanamke anastahiki kupewa mahari kamili kama mume atamuingilia kutokana na Neno Lake Ta’alaa:

 

"وَإِنْ أَرَدتُّمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَّكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا ۚ أَتَأْخُذُونَهُ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا    وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ وَأَخَذْنَ مِنكُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا"

 

Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na mmempa mmoja wao mirundi ya mali, basi msichukue humo chochote.  Je, mnaichukua kwa dhulma na dhambi iliyo bayana?   Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana (kimwili na kustarehe), na wao wanawake wamechukua toka kwenu fungamano thabiti?”.  [An-Nisaa: 20-21]

 

Hapa Allaah Ta’aalaa Amemkataza mume kuchukua chochote katika mahari aliyompa mkewe kama atamtaliki, na Amekuzingatia kuchukua huko kama ni dhulma na dhambi bayana kabisa.  Na hii ni kwa vile mahari hayo yalikuwa kwa mkabala wa kumuingilia, na mume ashajishibisha haki yake ya kujimai.  Hivyo ni haki ya mwanamke kuchukua mahari yote.

 

Na pia kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"أَيُّمَا امْرَأَةٍ نَكَحَتْ بِغَيْرِ إِذْنِ وَلَيِّهَا فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ، فَإِنْ دَخَلَ بِهَا فَلَهَا الْمَهْرُ بِمَا اسْتَحَلَّ مِنْ فَرْجِهَا"

 

“Mwanamke yeyote atakayeolewa bila ya idhini ya walii wake, basi ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili.  Na ikiwa mume atamuingilia, basi mahari ni haki yake kwa uhalali alioupata wa kustarehe na utupu wake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma] 

 

Ikiwa mahari kamili ni wajibu kuyalipa kwa kumuingilia mwanamke katika ndoa iliyo batili, basi ulazima wa kuyalipa katika ndoa sahihi ni mkubwa zaidi.  

 

Faida:

 

Mwanamke ni lazima apewe mahari yake yote kwa kuingiliwa hata kama kwa mtindo ulio haramu kama kumuingilia kinyume na maumbile, au katika hali ya hedhi, au nifasi, au akiwa amehirimia, au amefunga swawm, au yuko kwenye itikafu na mfano wa hayo.

 

Ikiwa  Ndoa Ni Sahihi Na Mmoja Wa Wanandoa Akafariki Kabla Ya Kufanyika Tendo La Jimai Kati Yao, Nini Kifanyike?: 

 

Hapa kuna hali mbili:

 

Hali ya kwanza:

 

Ikiwa mahari imebainishwa katika ‘aqdi  na mmoja wa wanandoa akafariki kabla ya tendo la jimai, basi mwanamke atastahiki mahari kamili kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa.  ‘Ijmaa ya Maswahaba (Radhwiya Allaah ‘anhum) pia iko kwenye rai hii.  Hii ni kwa sababu ‘aqdi haivunjiki kwa kifo, bali inamalizika kwa kifo hicho ambacho ndio umri wa mtu, na hukumu zake zinabakia pale pale kwa kumalizika kwake yakiwemo mahari.

 

Hali ya pili:

 

Ikiwa mahari haikubainishwa katika ‘aqdi (Nikaahu Tafwiydh), na mmoja wa wanandoa akafariki, ‘Ulamaa kwa hili wamekhitilafiana katika kauli mbili:

 

Kauli ya kwanza:  Mwanamke anastahiki mahari ya mfano.  Ni madhehebu ya Mahanafiy na Mahanbali, na ni kauli ya Ash-Shaafi’iy.  Na hoja zao ni hizi zifuatazo:

 

1-  Hadiyth ya ‘Alqamah aliyesema:

 

"أُتِيَ عَبْدُ الله بنُ مَسْعُوْدٍ فِي امْرَأَةٍ تَزَوَّجّهَا رَجُلٌ ثُمَّ مَاتَ عَنْهَا، وَلَمْ يَفْرِضْ لَهَا صَدَاقًا وَلَمْ يَكُنْ دَخَلَ بِهَا، فَاخْتَلَفُوْا إليْهِ فَقَالَ: أَرَى لَهَا مِثْلَ صَدَاقِ نِسَائِهَا، وَلَهَا المِيْرَاثُ وَعَلَيْهَا العِدَّةُ، فَشَهِدَ مَعْقِلُ بنُ سِنَانِ الأَشْجَعِيُّ: أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَضَى فِي بَرْوَعَ ابنةِ وَاشِقٍ بِمِثْلِ مَا قَضَى"

 

“Abdullaah bin Mas-‘uwd aliendewa mara kadhaa na watu wakimuuliza kuhusiana na hukmu ya mwanamke aliyeolewa na mwanamume, kisha mume akafariki na hakuwa amemtajia mahari yake wala kuwahi kumuingilia.  Akawaambia:  Naona anastahiki apewe mahari mfano wa wanawake wenzake, pia ana haki ya mirathi, na lazima akae eda.    Mi-‘qal bin Sinaan Al-Ashja’iyy akalitolea hilo ushahidi akisema:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alihukumu kwa Bar-wa’a bint Waashiq sawa na alivyohukumu”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Abu Daawuwd (2114), At-Tirmidhiy (1145), An-Nasaaiy (6/121), Ibn Maajah (1891) na Ahmad (3/480)]

 

2-  Ndoa ni mkataba, na muda wa kudumu kwake ni umri.  Na kwa kufa mmoja wao, mkataba unaisha lakini malipo yake yanabaki pale pale.

 

Kauli ya pili:  Hapewi chochote.  Ni madhehebu ya Maalik na kauli nyingine ya Ash-Shaafi’iy.

 

Faragha Inayokubalika Kisharia Kwamba Ni Faragha Kati Ya Mke Na Mume Hata Bila Ya Jimai:

 

Kidhibiti cha faragha sahihi inayozingatiwa, ni kukutana mke na mume baada ya ‘aqdi sahihi mahala asipoweza mtu yeyote kuwaingilia na ambapo wanaweza kustarehe kwa raha zao na kujifaragua watakavyo.

 

Faragha hii ikifanyika baada ya ‘aqdi, ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na kiasi cha mahari anachostahiki mwanamke kama mume atamtaliki katika kauli mbili:   

 

Ya kwanza:   Anastahiki kupewa mahari kamili hata kama jimai haikufanyika.  Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy (msimamo wa kale).  Ni madhehebu mashuhuri pia ya Ahmad, Is-Haaq na Al-Awzaaiy.  Kadhalika, ni kauli iliyohadithiwa toka kwa Makhalifa Wanne Waongofu pamoja na Ibn ‘Umar na Zayd bin Thaabit.  Hoja ya kauli hii ni:

 

1-  Toka kwa Zuraaratu bin Awfaa, amesema:

 

"قَضَى الْخُلَفَاءُ الرَّاشِدُونَ الْمَهْدِيُّونَ أَنَّ مَنْ أَغْلَقَ بَابًا أَوْ أَرْخَى سِتْرًا فَقَدْ وَجَبَ الصَّدَاقُ وَالْعِدَّةُ"

 

 “Makhalifa Werevu Waongofu wamehukumu kwamba mwenye kufunga mlango, au akateremsha pazia, basi mahari na eda zimelazimu”. [Isnaad yake imekatika.  Imechakatwa na Al-Bayhaqiy (7/255) na Ibn Hazm]

 

2-  Toka kwa Sa’iyd bin Al-Musayyib kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu): 

 

 "قَضَى فِي الْمَرْأَةِ إذَا تَزَوَّجَهَا الرَّجُلُ، أَنَّهُ إِذَا أُرْخِيَتِ السُّتُوْرُ، فَقَدْ وَجَبَ الصَّدَاقُ وَالعِدَّةُ".

 

“Alihukumu kuhusu mwanamke kwamba akiolewa na mtu, na mtu huyo akateremsha pazia, basi mahari imelazimu”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imechakatwa na Maalik katika Al-Muwattwa (2/528) na Al-Bayhaqiy (7/255)]

 

3-  Toka kwa ‘Aliy amesema:

 

"إِذَا أُرْخِيَتِ السُّتُوْرُ، فَقَدْ وَجَبَ الصَّدَاقُ"

 

“Pazia zikiteremshwa, basi mahari ni wajibu”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imechakatwa na Sa’iyd bin Manswuwr (1/201) na Al-Bayhaqiy (7/255)]  

 

4-  Neno Lake Ta’aalaa:   

 

"وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ"

 

Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana (kimwili na kustarehe)?”.  [An-Nisaa: 21]

 

Wamesema "الإفْضَاءُ" ni "الخلْوَة" yaani faragha, kwa kuwa "الإفْضَاءُ" inatokana na neno "الفَضَاءُ" lenye maana ya "الخَلَاءُ" yaani sehemu tupu, kana kwamba Allaah Amesema: “Na hali nyinyi kwa nyinyi mmekaa faraghani bila mwingine”. 

 

5-  Wamelichukulia neno kugusa katika Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"

 

“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”.  [Al-Baqarah: 237]

 

6-  Kwa kuwa matokeo ya faragha kwa asilimia kubwa ni kuchezeana na kujimaiana.  Na mume akiwa faragha na mkewe (na hasa baada ya ndoa), utashi wa nguvu unachemka wa kufanyika hilo. 

 

Kauli ya pili:  Hastahiki mahari kamili isipokuwa kwa kuingiliwa tu. Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na riwaayah nyingine toka kwa Ahmad na Ibn Hazm.   Pia imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhumaa).  Hoja zao ni:

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"

 

“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”.  [Al-Baqarah: 237]

 

Wamesema kwamba makusudio ya kugusa katika aayah ni jimai.

 

2-  Wamefasiri "الإفْضَاءُ" katika Neno Lake Ta’alaa:

 

"وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ"

 

Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana (kimwili na kustarehe)?”… kwa maana ya kujimai.

 

3-  Imeripotiwa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba alikuwa anasema kuhusu mwanamume ambaye amekabidhiwa mkewe kisha akamtaliki, halafu akadai kwamba hajamgusa:

 

"عَلَيْهِ نِصْفُ الصًّدَاقِ"

 

“Ni lazima alipe nusu mahari”.  [Isnaad yake ni dhwa’iyf.  Imechakatwa na Sa’iyd bin Mansuwr (772)]

 

4-  Toka kwa Ibn Mas-‘uwd, amesema: 

 

"لَهَا نِصْفُ الصَّدَاقِ، وَإِنْ جَلَسَ بَيْنَ رِجْلَيْهَا"

 

“Ni haki yake nusu mahari, hata kama mume atakaa kati ya miguu miwili ya mkewe”.  [Isnaad yake imekatika.  Ibn Hazm (9/484)]

 

Ninasema:  “Lau riwaayah hizi zilizonukuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn Mas-‘uwd (ambazo moja Isnaad yake ni dhwa’iyf na nyingine imekatika) zingethibiti, basi zingekabilishwa na riwaayah zilizothibiti kunukuliwa toka kwa ‘Umar na ‘Aliy (ambazo zote Isnaad zake ni swahiyh), na mpingaji asingelikuwa na hoja yoyote, bali mvutano ungelibakia katika kuawilisha maana ya kugusa "المَسُّ" na kuingiliana "الإِفْضَاءُ" katika aayah mbili tukufu (237 Al-Baqarah na 21 An-Nisaa).  Na kwa mujibu wa ninavyojua, hakuna riwaayah kama hizo zilizopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas au Ibn Mas-‘uwd.  Kauli za ‘Umar na ‘Aliy na Maswahaba wengineo ndizo ninazozikubali.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Lakini mtu anaweza kujiuliza aseme:  Imekubalika kwamba mume atalipa mahari kamili kwa kukaa faragha na mkewe, kwa kuwa faragha ni chachu ya kumuingilia.  Na lau itathibiti kwamba mke hajaingiliwa kwa kukiri yeye mwenyewe, au ikathibiti kwa njia ya vipimo vya kisasa, je, hapo atapewa nusu mahari?  Jibu la hili litafitiwe na ‘Ulamaa na wajitahidi kulipembua kupata jawabu mwafaka. 

 

 

 

Share