10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake: Hali Inayolazimu Apewe Mahari Nusu: Ni Kutalikiwa Mwanamke Kabla Hajaingiliwa, Na Mahari Ikawa Imebainishwa Kwenye ‘Aqdi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الصَّدَاقُ

 

Mahari

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

10:  Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake:  Hali Inayolazimu Apewe Mahari Nusu:  Ni Kutalikiwa Mwanamke Kabla Hajaingiliwa, Na Mahari Ikawa Imebainishwa Kwenye ‘Aqdi:

 

 

Mwanaume akimtaliki mkewe kabla hajamuingilia (na pia kabla hajakaa naye faraghani) na mahari ikawa ilibainishwa kwenye ‘aqdi, basi mwanamke atastahiki nusu ya mahari kwa itifaki ya ‘Ulamaa.  Na hii ni kwa Neno Lake Ta’alaa:

 

"وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"

 

“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”.  [Al-Baqarah: 237]

 

Kadhalika, hali inakuwa hivi hivi, pakitokea mtengano bila talaka (ikiwa ni kutoka upande wa mume) kama mume kufanya "إِيْلَاءُ" (Iylaau) au "لِعَانُ"  (Li’aan), au mume kuritadi, au akakataa kusilimu baada ya mkewe kusilimu na mfano wa hayo.  Haya ni madhehebu ya Mashaafi’iy na Mahanbali.

 

"إِيْلَاءُ"] (Iylaau), ni mume kumwapia mkewe kwa Allaah kwamba hatomjimai kwa zaidi ya miezi minne kwa lengo la kumdhuru.  Ama "لِعَانُ"  (Li’aan), ni mume kumtuhumu mkewe kufanya zinaa bila kuwa na mashahidi, na badala yake ataapa viapo vinne kwamba yeye ni mkweli kwa madai yake dhidi ya mkewe, na kiapo cha tano atajiapiza kwamba laana ya Allaah imshukie kama ni mwongo.  Mke kama anakanusha tuhuma, na yeye pia ataapa viapo vinne kwamba anasingiziwa, na kwamba yeye ni mkweli kwa anayoyasema, na kiapo cha tano atajiapiza ghadhabu za Allaah zimshukie kama madai ya mume wake ni ya kweli]

 

Kama mahari ilikuwa haijabainishwa, na mume akamtaliki kabla hajamuingilia (au kukaa naye faragha), katika hili, ‘Ulamaa wamekhitilafiana katika kauli tatu kuhusu kiasi cha mahari anachostahiki mwanamke:

 

Ya kwanza: 

 

Hapewi kitoka nyumba (kiliwazo).  Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Ath-Thawriy, Abu ‘Ubayd na wengineo.  Hoja zao ni:

 

1-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً ۚ وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ"

 

“Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia mahari yao.  Wapeni kiliwazo, kwa mwenye wasaa kadiri ya uwezo wake na mwenye dhiki kadiri ya uwezo wake.  Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan”.   [Al-Baqarah: 236]

 

2-  Kauli Yake Ta’alaa:

 

"وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ"

 

“Na wanawake waliotalikiwa wapewe kiliwazo (kitoka nyumba) kwa mujibu wa shariy’ah, ni haki juu ya wenye taqwa”.  [Al-Baqarah: 241]

 

3-  Kauli Yake Ta’alaa:

 

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا"

 

 

Enyi walioamini!  Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu.  Basi wapeni kitoka nyumba na waacheni huru, kwa mwachano mzuri”.   [Al-Ahzaab: 49]

 

Kauli ya pili: 

 

Hapewi chochote, lakini inapendeza kama atapewa kiliwazo.  Ni madhehebu ya Maalik na Al-Layth.  Dalili yao ni Neno Lake Ta’aalaa:

 

"مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ"

 

“Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan”.   [Al-Baqarah: 236]

 

Wanasema kwamba aayah hapa inaonyesha kwamba kiliwazo ni kwa njia ya ihsaan na kufanya wema tu, lakini si wajibu. Na kama ni wajibu, basi hilo lisingehusishwa na wafanya ihsaan.

 

Hoja yao imejibiwa kwamba kutenda wajibu ni katika ihsaan.

 

Kauli ya tatu:

 

Anastahiki kupewa mahari ya mfano.  Ni madhehebu ya Ahmad, na hoja yake anasema kwamba hiyo ni nikaah sahihi inayowajibisha mahari ya mfano wake baada ya kumuingilia, hivyo inawajibisha nusu ya mahari kwa kumtaliki kabla ya kumuingilia.

 

Ninasema:  “Kauli sahihi ni ya kwanza kutokana na uwazi wa aayah tukufu zilizotolewa dalili.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”

 

Faida:   Imeshakubalika na kupitishwa kwamba ikiwa mahari yamepangwa na kubainishwa kiasi chake katika ‘aqdi, kisha mume akamtaliki mkewe kabla ya kumuingilia, basi mke atapewa nusu.  Lakini, endapo kama mahari hayakutajwa au kubainishwa katika ‘aqdi bali yakaja kupangwa baada yake kwa maridhiano au kwa hukumu, je, mwanamke atastahiki kupata nusu ya mahari yaliyobainishwa baada ya ‘aqdi au la?

 

‘Ulamaa wa Kihanafi wamesema:  Mahari iliyopangwa baada ya ‘aqdi haikatwi tena nusu.  Inayokatwa nusu ni ile iliyobainishwa wakati wa ‘aqdi kama ilivyobainishwa na Qur-aan Tukufu.  Hapa mwanamke atapewa kiliwazo tu na si vinginevyo.

 

Lakini Jumhuwr ya ‘Ulamaa wana rai nyingine.  Wanasema kwamba mahari iliyopangwa baada ya ‘aqdi inagawika nusu kama ile iliyotajwa wakati wa kufunga ‘aqdi.  Na hili ni sahihi, kwa kuwa Neno Lake Ta’alaa:

 

"فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"

 

“Basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”, ni tamshi jumuishi kwa mahari yote katika ndoa sahihi, ni sawa mwenye kuoa akawa ameipanga katika ‘aqdi au baada ya ‘aqdi.  Na Allaah ‘Azza wa Jalla Hakusema: Basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha kabla au wakati wa kufunga ‘aqdi”.  Na kama Angelitaka hilo, basi Angelibainisha.

 

   

Share