11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Yanayopelekea Kudondoka Mahari Yote
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
11: Yanayopelekea Kudondoka Mahari Yote:
1- Kutokea utengano -kwa matakwa ya mke- kabla ya kumuingilia.
Ni kama mke kusilimu -na mumewe kubaki kafiri-, au mume kuvunja ndoa kutokana na kasoro aliyonayo mke, au mke kuritadi, au kugundulika kwamba mke aliwahi kumnyonyesha mume aliyemwoa, au mke kuvunja ndoa kutokana na kasoro aliyonayo mume, au mume kuwa masikini kupindukia na mfano wa hayo. Hapo mahari iliyobainishwa na mahari ya mfano itadondoka. Ni madhehebu ya Mashaafi’iy, Mahanbali, Mahanafiy na Wamaalik. Lakini wao hawajatofautisha kati ya kuwa mtengano unatokana na mume au mke.
2- Khulu’u (Mwanamke kudai talaka kwa kumlipa mume kitu au kumrejeshea mahari yake): Ikiwa mume atakubali kuachana na mkewe kwa kuachia mahari yake, hapo mahari yote itadondoka. Na kama mke bado hajapokea, basi mume hatotoa, na ikiwa amemkabidhi, basi mke atarejesha.
3- Kusamehe mahari yote kabla ya kuingiliwa au baada ya kuingiliwa.
Mwanamke akisamehe mahari yake iliyobainishwa, na mahari hiyo ilikuwa ni deni katika shingo ya mume, basi mahari hiyo hudondoka, lakini kwa sharti mke awe na vigezo vya kusamehe na kutoa anachomiliki.
4- Mwanamke kutunuku mahari yake yote kwa mume:
Madhali mke ana vigezo vya kutoa anachomiliki, na mume akakubali kutunukiwa mahari kwenye baraza ya kufunga ‘aqdi, ni sawa tunu hiyo ikawa kabla ya kukabidhi mahari au baada yake, basi mahari itadondoka.