03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Walima Wa Harusi: Kuitikia Mwaliko Wa Walima

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

وَلِيْمَةُ العُرْسِ

 

Walima Wa Harusi

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

03:  Kuitikia Mwaliko Wa Walima:

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba kuitikia mwaliko wa walima ni lazima isipokuwa kwa udhuru.  Wametoa dalili kwa haya yafuatayo:

 

(a)  Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا دُعِيَ أَحَدُكُمْ إِلَى اَلْوَلِيمَةِ فَلْيَأْتِهَا" 

 

“Akialikwa mmoja wenu walima, basi ahudhurie”.  [Al-Bukhaariy (5173)]

 

(b)  Hadiyth iliyotangulia ya Abu Hurayrah:

 

"وَمَنْ تَرَكَ الدَّعْوَةَ فَقَدْ عَصَى اللهَ وَرَسُولَهُ"

 

“Na atakayesusa mwaliko, basi hakika amemuasi Allaah na Rasuli Wake”.  [Al-Bukhaariy (5177) na Muslim (1432)] 

 

Mwanamke ni sawa na mwanaume katika hukmu hii, isipokuwa kama kutakuweko mchanganyiko wa wanawake na wanaume, au ufaragha wa haramu, hapo haitofaa kuhudhuria.

 

Ikiwa Mwalikwa Amefunga:

 

Ikiwa mtu amealikwa na yeye amefunga, ni sawa akiwa mwanamke au mwanaume, basi ni lazima aitikie mwaliko na ahudhurie mnasaba kutokana na Hadiyth zilizotangulia.  Anapofika, atakuwa na chaguo kati ya mambo mawili:  Ima atakula pamoja na waalikwa wengine -ikiwa swawm yake ni ya Sunnah na akataka kufungua- au atajizuia kula, na atamwombea du’aa mhusika wa walima.  Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"إِذَا دُعِيَ أَحَدُكُمْ إِلَى طَعَامٍ فَلِيُجِبْ وَإِنْ شَاءَ طَعِمَ وَإِنْ شَاءَ تَرَكَ"

 

“Akialikwa mmoja wenu chakula basi aitikie mwaliko.  Akitaka atakula, na akitaka ataacha kula”.  [Muslim (1430) na Abu Daawuwd (3722)]

 

Na neno lake Rasuli:

 

 "إِذَا دُعِيَ أَحَدُكُمْ إِلَى طَعَامٍ فَلْيُجِبْ فَإِنْ كَانَ صَائِمًا فَلْيُصَلِّ "

 

“Akialikwa mmoja wenu chakula, basi aitikie wito.  Na kama amefunga, basi amwombee du’aa (mhusika)”.  [Muslim (1431), Abu Daawuwd (3719) na Al-Bayhaqiy (7/263)]

 

Du’aa inakuwa ni katika zile zilizotajwa kwenye mlango wa adabu za chakula.

 

 

Share