04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Walima Wa Harusi: Nyudhuru Za Kutohudhuria Walima

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

وَلِيْمَةُ العُرْسِ

 

Walima Wa Harusi

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

04:  Nyudhuru Za Kutohudhuria Walima:

 

Tumesema kwamba kuhudhuria walima na kuitikia mwaliko kumefungamanishwa na kutokuwepo udhuru.  Kati ya nyudhuru hizo ni:

 

1-  Kuwepo munkari ndani ya walima wenyewe kama tembo, ulevi, muziki na kadhalika.  Hali ikiwa hivi, basi haijuzu kuhudhuria ila kama atahudhuria kwa lengo la kukataza na kuwaasa wahusika kuacha munkari zilizopo.  Dalili ya hili ni Hadiyth ya ‘Aliy ambaye amesema:

 

"صَنَعْتُ طَعَامًا فَدَعَوْتُ رَسُولَ اللهَ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَجَاءَ فَرَأَى في البَيْتِ تَصَاوِيْرَ فَرَجَعَ، فَقُلْتُ: يَا رَسُوْلَ الله، مَا أَرْجَعَكَ بِاَبِي أَنْتَ وَأُمِّي؟ قَالَ: إِنَّ في البَيْتِ سِتْرًا فِيهِ تَصَاوِيرُ، وَإِنَّ الْمَلاَئِكَةَ لاَ تَدْخُلُ بَيْتًا فِيهِ تَصَاوِيرُ"

 

“Nilitayarisha chakula nikamwalika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Akaja, lakini aliona picha ndani ya nyumba akarudi.  Nikamuuliza:  Ee Rasuli wa Allaah!  Kitu gani kimekurejesha, nakuapia kwa baba yangu na mama yangu.  Akasema:  Nyumbani kwako kuna picha, na hakika Malaika hawaingii nyumba yoyote ambayo ndanimwe kuna picha”.  [Ibn Maajah (3359) na Abu Ya’alaa (436)]

 

2-  Awe mwalikaji anawaalika matajiri tu bila masikini.

 

3-  Awe mwalikaji hajali chanzo cha pato lake kuwa ni la haramu, au akawa anajishughulisha na kazi zenye utata. 

 

Nyudhuru nyingine ni zile za kisharia kama udhuru unaomruhusu mtu kutokwenda kuswali Swalaah ya ijumaa kutokana na mvua nyingi, au matope, au kuhofia usalama wa mali, au kudhuriwa na adui na kadhalika.

 

Bi harusi Anaruhusiwa Kuwahudumia Wageni Wa Mumewe Siku Ya Harusi Yao:

 

Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’ad (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba:

 

"دَعَا أَبُو أُسَيْدٍ السَّاعِدِيُّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي عُرْسِهِ، وَكَانَتِ امْرَأَتُهُ يَوْمَئِذٍ خَادِمَهُمْ وَهِىَ الْعَرُوسُ، قَالَ سَهْلٌ: تَدْرُونَ مَا سَقَتْ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم؟ أَنْقَعَتْ لَهُ تَمَرَاتٍ مِنَ اللَّيْلِ، فَلَمَّا أَكَلَ سَقَتْهُ إِيَّاهُ‏"

 

“Abu Usayd As-Saa’idiy alimwalika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hafla ya harusi yake, na mkewe alikuwa ndiye  anayewahudumia siku hiyo akiwa yungali bi harusi.  Sahl akauliza:  Mnajua ni kinywaji gani alimpa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam?).  Alimloekea tende usiku, na baada ya kula, alimpa juisi anywe (ya tende hiyo iliyoloekwa)”.  [Al-Bukhaariy: (5176), Muslim (2006) na Ibn Maajah (1912)]

 

Tunasema:  Mahala pa kufanya hivi, ni kama mazingira yatakuwa mbali na fitna.

 

 

 

Share