Kumlipia Ada Za Shule Asiye Muislamu Inajuzu?

 

SWALI:
 
Assalamu alaikum,
Jee ina faa kumsomesha (kumlipia karo za shule) mtoto asiye kuwa wa kiislamu?
Jaza ka Allaah.


 
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
Shukrani kwa swali lako kuhusu hilo la kumsomesha asiyekuwa Muislamu. Ni vizuri sisi tuelewe kumsomesha huko ni kwa sabahu yeye ni jamaa yako kama mtoto wako na hivyo una jukumu au ni mtoto tu? Je, unataraji kupata nini kwa kumsaidia? Je, anahitaji kweli usaidizi kwa kuwa hakuna wakumlipia karo? Je, yeye ni jirani yako?
 
Haya ni baadhi ya maswali ambayo yanaweza kujitokeza kwani swali lako halipo wazi. Lakini InshaAllaah tutajaribu kukueleza na tunatumai kuwa tutaweza kukidhi hayo katika jibu letu hili.
 
Hakika ni kuwa elimu ni msingi mkubwa ambao Uislamu umehimniza sana wafuasi wake wawe ni wenye kutafuta. Na katika kulifikia hilo inabidi walio na uwezo wawe ni wenye kuwasaidia walio masikini ili kufikia katika kilele cha masomo. Ikiwa mtoto unayemlipia karo ni mtoto wako basi unawajibu wa kumsomesha au akiwa jirani pia wajibu huo uko ikiwa wazazi wake hawana uwezo au ni yatima. Ikiwa mtoto anaonyesha ishara ya kuupenda Uislamu basi pia unaweza kumvutia zaidi kwa kumsaidia hata pesa za Zakaah zinaweza kutumiwa kwa usaidizi aina hii kama alivyotujulisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Suratut Tawbah ayah ya 60.
 
Lakini la muhimu kwetu kujua ni kwamba Waislamu wanahitaji zaidi usaidizi huo kuliko wasiokuwa Waislamu kwani wao wana sehemu nyingi ya kupatia hasa wakiwa masikini. Hivyo, kabla ya kumsaidia asiyekuwa Muislamu kwa kumlipia karo tazama walio katika Uislamu. Ikiwa wapo wahitaji na kwa hakika wapo basi anza kuwasaidia wao na thawabu zako zitakuwa nyingi zaidi. Kwa hiyo, nasi tuanze kusaidiana sisi kwa sisi. Hilo ni kuwa Muislamu ana haki kutoka kwako ya kusaidiwa.
 
Na Allaah Anajua zaidi
 
 
Share