Kumsubiri Bibi Harusi Nje Ya Mlango Kujua Kama Ni Bikra (Kijibu Harusi)

SWALI:

 

AWW,

1-UISILMU UNASEMAJE JUU YA KUJUWA UBIKIRA WA BIBI HARUSI PALE ANPOKUTANA

NA MUME WAKE SIKU YA KWANZA WATU KUSUBIRI NA KUPEWA HABARI KAMA VILE BI HARUSI KAHONGERA AU LA ? KAMA IFNYAVYO (BAADHI YA JAMII ZA WASWAHIL).

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako hili muhimu ambalo imekuwa ni ada katika jamii yetu kufanya jambo hili, na wengi wanaliulizia kama liko katika mafunzo ya dini yetu, hivyo tutalielezea kwa urefu tupate kufahamu kama linapasa kutendwa au halipasi.

Desturi ya kuwasubiri wana ndoa nje ya mlango kufanywa na mtu anayeitwa  kungwi. Na bi harusi huwekewa kitambaa cheupe anapoingiliana na mumewe kwa mara ya kwanza ili matone ya damu ya kuvunja bikra yaonekane katika kitambaa. Jamaa zake bi harusi na bwana harusi huwa wanasubiri nje ya mlango na wengine kumsikiliza bi harusi kama atalia kwa maumivu ya kuvunjwa bikra. Wanapomaliza maingiliano, kitambaa hicho huchukuliwa na kufurahikiwa na watu wa bi harusi na wengine hufikia hadi kukitambaza kwa watu waone na kutangaza au kuimba  'harusi imejibu!'.

 

Ada hii hakika ni ya fedheha na haiko katika mafunzo ya dini yetu ya Kiislamu. Yafuatayo yanapasa kuzingatiwa sana na wafanyao bado ada hii ili waache kabisa:

  1. Kumdhalilisha mwanamke na kumtia aibu kwa watu. Aibu gani watu waone damu yake?

 

  1. Pindi ikiwa haikupatikana kuvunjika bikra yake, labda kwa sababu mbali mbali nyingine ambazo sio kutokana na maasi ya kufanya zinaa, je, adhulumiwe mwanamke kwa kuhutumiwa kuwa kafanya zinaa? Na ataishi vipi na mumewe maisha yake yote katika fikra hiyo? Wengine husababisha mume kumkataa bi harusi hapo hapo.

 

  1. Mke na mume katika maingiliano wanapaswa wawe faragha ili wapate utulivu waweze kukamilisha matamanio baina yao na kupatikana furaha. Na hii ndio tofauti kubwa kati yetu na wanyama. Sasa vipi mke na mume wawe katika maingiliano na huku watu wengine wanawasubiri wakijua kinachoendelea baina yao? Vipi watapata utulivu? Ujinga gani huu jamii yetu inayojifunza?

Tutambue kwamba Nikaah ni katika mambo matatu muhimu ya mwanadamu; kuzaliwa, kuoa/kuolewa na kufa. Hivyo jambo muhimu kama hili khaswa la ndoa linahitaji kupewa heshima yake. Na hayo ni mambo ya siri ya baina ya mke na mume ambayo yamekatazwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

Hadiyth ya kwanza:

((إِنَّ مِنْ أَشَرِّ النَّاسِ عِنْدَ اللّهِ مَنْزِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ، الرَّجُلَ يُفْضِي إِلَى امْرَأَتِهِ، وَتُفْضِي إِلَيْهِ، ثُمَّ يَنْشُرُ سِرَّهَا))

((Hakika miongoni mwa watu waovu kabisa siku ya Qiyaamah ni mwanamume anayemuingilia mkewe kwa jimai akamuitikia, kisha akaeneza siri zake)) [ Muslim, Ibn Abi Shaybah, Ahmad na wengineo]


Ya pili:

 

عن أسماء بنت يزيد : أنها كانت عند رسول الله صلى الله عليه وسلّم ، والرجال والنساء قعود عنده . فقال: ((لَعَلَّ رَجُلاً يَقُولُ ما يَفْعَلُ اهْلِهِ، وَلَعَلَّ امْرَأَةً تُخْبِرُ بِمَا فَعَلَتْ مَعَ زَوْجِهَا؟)) ازَمَّ القَوْمُ، فَقلت: أي والله يا رسول الله، إنهم ليفعلون، وإنهنّ ليفعلن، قال: ((فَلا تَفْعَلُوا، فًّانَّمَا مَثَلُ ذَلِكَ مَثَلُ شَيْطانٍ لَقِيَ شَيْطَانَةً فَغَشِيَهَا وَالنَّاسُ يَنْظُرُونَ))

Imetoka kwa Asmaa bint Yaziyd ambaye amesema: "Alikuwa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na walikuweko wanaume na wanawake wamekaa. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema, ((Huenda mume akajadiliana anayoyafanya na mkewe au huenda mwanamke akamhadithia mtu aliyoyafanya na mumewe?)) Watu walikuwa kimya. Kisha nikasema: 'Ewe Mjumbe wa Allaah, hakika wanaume na wanawake wote tunafanya hivyo'. Kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema, ((Msifanye hivyo kwani ni kama mfano shaytwaan mwanamume amekutana na shaytwaan mwanamke njiani wakawa wanafanya jimai na huku watu wanawatazama)) [Ahmad: Hasan au Swahiyh kutokana na kukubaliana (na masimulizi mengine)]

Khitimisho ni kwamba haifai kabisa jambo hili na inatupasa sote tujitahidi kuwafunza wazazi, ndugu na jamaa zetu uovu wa jambo hili ili lisiendelee kutendwa na ujinga huu utoweke abadan, na abakie mwanamke wa Kiislamu katika hadhi yake ya heshima, ustaarabu na amani.

Na Allaah Anajua zaidi

Share