Mahari Niliyotoa Hayakumfikia Mke Na Mahari Yake Yamepunguzwa Afanyeje?

SWALI:

 

Asalaam alaykum ndugu zangu katika uislam,

Nimegundua mahari niliyotoa haikumfikia mke wangu kwa kuwa kuna mtu/ watu upande wa mke ambao walikabidhiwa ili wakampe muolewaji hawakumpa.

Binafsi nimekuja kutambua hilo wakati ndoa imeshafungwa. je nifanyeje . na je ikatokea mume katoa mahari kamili, lakini mtu aliyekabidhiwa kumpatia mke kadokoa ile mahali ( kaipunguza) na bila mtu yeyote kujua lakini baadae ndoa imeshafungwa muolewaji kagundua mahari yake imepunguzwa.

Nini kifanyike.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Mahari katika nikaha ni wajibu nayo ni haki ya mwanamke kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

"Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa. Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha."  An-Nisaa: 4.

Na kuyataja mahari wakati wa kufunga ndoa ni Sunnah, kama mke akipenda kumtunukia mumewe mahari yake siku za mbele sio vibaya kama ilivyobainisha Aayah yetu hapo juu.

Na hapana shaka kuwa mzazi ana haki kwa mwanawe, basi kama amechukuwa mahari ya mtoto wake na kuyatumia hakuna kitu ni haki yake, kwani yeye huyo mtoto na mali yake ni mali ya mzazi wake.  Kilicho muhimu ni kuwa afanye wema katika kuchukua na asimdhuru mtoto wake katika kuchukua kwake mpaka ikafikia kuwa hana kitu cha kutumia yeye mtoto, hivyo anaweza kuchukua kiasi cha haja yake na kumuachilia mtoto kitachomsaidia na kumfaa.

Hivyo basi mzazi anayo haki ya kuchukua akitakacho katika mahari ya mtoto wake kiwe kingi au kidogo na hukuna kosa.

Na wewe kama ni mume basi kilicho wajibu kwako kilikuwa kutoa mahari na kuwapa wahusika, na si juu yako kufuatilizia kama imefika au hayakufika maadam umempa mhusika na mtu aliyewakilishwa upande wa mke; haipendezi kufuatilizia na kuchunguza kama mahari uliyoyatoa yamemfikia mke uliyemuoa; kwani mzazi wake kama ilivyobainishwa ana haki ya kuchukua akitakacho kwani yeye huyo mkeo na mali yake ni vya mzazi wake 

Aliyepokea mahari huwa amepokea kwa niaba ya huyo mtoto wao ambae baadae uliozeshwa wewe, hivyo huna la kufanya wala hakuna hukumu yenye kufungamana na hilo kama wazazi wamechukuwa mahari ya mtoto wao, kinachukulazimu ni kumhudumia mkeo, na kama atakutunukia mkeo siku za mbele itakuwa ni halali kwako.

Moingoni mwa Sunnah kama ilivyoelezwa ni kutaja mahari wakati wa kufunga ndoa na kama unavyosema kuwa mume katoa mahari kamili, lakini mtu aliyekabidhiwa (inaonyesha makabidhiano yalikuwa sehemu ya siri hata ikafikia kutojulikana mpaka baada ya kuolewa) kumpatia mke kadokoa kitu na bila mtu yeyote kujua lakini baadae ndoa imeshafungwa muolewaji kagundua mahari yake imepunguzwa. 

Katika sharia ya Kiislamu jambo kama hili huwa ni tuhuma, na mtuhumiwa kwa kawaida ya sharia ya Kiislamu (hata iwe ni kweli unayomtuhumu) huwa hana kosa mpaka mwenye kutuhumu alete bayyinah (ushahidi ulio wazi) hivyo wewe kama ulimkabidhi mshenga wako akufikishie kwa wahusika na hakuna ajuaye ni kiasi gani isipokuwa wewe na yeye, sharia ya Kiislamu inakutaka ulete bayyinah. Kwa upande mwengine ndoa haina mashaka wala hakuna cha kufanya wewe ni mume na yeye ni mke kama ilivyothibitishwa katika ndoa yenu.

Na ikiwa huyo aliyeaminiwa kufikisha amana hiyo kaila au kamega fungu, na ikatokea wewe kuulizwa hayo mahari tena, basi utalithibitisha hilo na wao watajua hatua ya kuchukua; na huyo aliyetenda hayo atachukua dhima mbele ya Allaah kwa kutotekeleza amana na pia kuingia katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya yule mwenye alama za unafiki kwa kupewa amana na kutoifikisha.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share