Kuapa Kwa Mswahafu (Qur-aan) Inafaa?

Kuapa Kwa Mswahafu (Qur-aan) Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

Assalam alaykum warahmutullahi wabarakatuh, sina budi kumshukuru Allah kwa mpaka hapa nilipifika, Allah atughufirie dhambi zetu na atujaaliye wenye kuipenda dini yetu na tupate uongofu kwake Amin, na nyinyi wana wa Alhidaaya Allah awamiminie kheri zake kwa kutuelimisha na mambo mengi humu. Amin

 

Suala langu : Mimi naishi UK katika utaratibu wa nchi kuna wakati tunafanikiwa kupata passport sasa kabla hujakabidhiwa passport huwa unaitwa kula kiapo ndio upewe na kiapo hicho cha kumtii Queen na sheria zake sasa huwa kuna viapo vya aina tatu (1) Cha Kiislaam (2) Cha Christian (3) Cha mtu ambaye hana dini.

 

Kama mimi Muislam nitachagua cha Islaam, sasa je hichi kiapo kitakuwa kinakubalika na sheria za kiislam kwa sababu mimi sitomtii Queen na kama hakikubaliki ni vipi nile kiapo na kiapo cha kukamata mas-haf kinakubalika? na kama hakikubaliki tukikamata mash-haf nakuapa hatutokuwa tunamkufuru Allah? Na kama hujaambiwa uchaguwe kiapo wakikuapisha cha kikiristo je itakuwaje? Naomba mnielimishe kwani ni jumla ya mazingira tunayoishi.

 

Wabillaahi Tawfik. Wassalam alaykum warahmatullahi wabarakatuh.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Suala lako hili ni Swali muhimu linalowahusu ndugu zetu wanaoishi nchi ze Kimagharibi.

 

Kuapa kwa maneno ya Allaah kunakubalika kwani maneno yake ni miongoni mwa sifa Zake.

 

Ama kutumia Mswahafu na kuapa kwa kuushika haifai kwa sababu utakuwa hujataja jina la Allaah bali umeashiria kwenye Mswahafu ambao ni kitabu kilichotengenezwa kwa karatasi na wino pamoja na kwamba unaweza kusema kuwa unakusudia maneno yaliyomo ndani ambayo yanatoka kwa Allaah! Lakini kwa kufanya hivyo kunahesabika kuwa ni kiapo ambacho si kwa Allaah bali cha Mswahafu. Na kuapa kwa kitu chochote haifai isipokuwa ni kuapa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee kwani kuapa kinyume Yake huwa ni shirk. Makatazo haya tumepata kutoka katika Hadiyth ifuatayo:

 

قال النبي صلى الله عليه وسلم : ((مَنْ حَلَفَ  بِغَيْرِ اللَّهِ فَقَدْ كَفَرَ أَوْ أَشْرَكَ))  رواه الترمذي   وأبو داود   وصححهالألباني في صحيح الترمذي .

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeapa pasi na Allaah, atakuwa amekufuru ameshiriki [amemshirikisha Allaah])) [At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd na ameipa daraja ya Swahiyh Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

 

 

Vile vile kuapa kwa niyya ya kutaka kukanusha jambo la uongo, kwa maana mtu anaposhadidiwa kuwa kafanya jambo fulani, lakini yeye akakanusha kuwa hakutenda jambo hilo, hulazimishwa ashike Mswahafu, au atie mkono wake ndani ya Mswahafu na afanye kiapo. Japokuwa atasema mfano: "Wa-Allaahi sikutenda jambo kadhaa na kadhaa." au mfano anapotaka kukiri jambo kuwa kalitenda aseme: "Wa-Allaahi nimefanya kadhaa na kadhaa." atakuwa ameapia Mswahafu badala ya kumuapia Allaah kwa kusema ‘Wa-Allaahi’, na hivyo itakuwa haikubaliki kishariy’ah kutokana na dalili katika Hadiyth hiyo ya juu.

 

 

Hakuna yeyote anayeruhusiwa kuapa kwa kitu chochote kingine pasi na Allaah. Ni Allaah Pekee Anayeweza kuapa kwa vitu vyovyote Avitakavyo, mfano: mbingu, jua, usiku, mchana, majabali, matunda au chochote Atakacho, kwani Yeye Ndiye Muumba wa hivyo vitu. Mifano tunaona mingi katika Qur-aan Anavyoapia mwanzoni mwa baadhi ya Suwrah, mfano:

 

وَالسَّمَاء والطَّارِقِ   -  وَالْفَجْرِ   -  وَالشَّمْس    - وَاللَّيْلِ  -   وَالضُّحَى   -   وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ   -   وَالْعَصْرِ

 

Hata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haikumpasa kuapia chochote, na ndio maana tunaona mara nyingine akisema anapotaka kuapa:

((والذي نفسي بيده ))

((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake…..)) [Akimkusudia Allaah]

 

Kuapa kwa jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kunapasa kwa kutumia herufi tatu pekee nazo ni 'wa', 'ta', na 'bi' Kwa maana kusema "Wa-Allaahi", "Ta-Allaahi", na "BiLLaahi".     

 

 

Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu hukmu ya kuapia Mswahafu alijibu: "Hairuhusiwi kuweka nadhiri au kuapa isipokuwa kwa Allaah au moja ya sifa Zake. Ikiwa mtu ataapa kwa jina la Allaah, basi hakuna haja tena kuleta Mswahafu kwa ajili ya kuapa kwa sababu kuapa kwa Mswahafu haikufanyika zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba. Hata baada ya Qur-aan kukusanywa katika kitabu kimoja hawakuwa wakiapia Mswahafu bali mtu alikuwa akiapa kwa Allaah bila ya kushika Mswahafu." [Fataawa Nuwr 'Alaa Ad-Darb]

 

Ama kwa mujibu wa maelezo ya wale waliokwishaapishwa huko Uingereza, ni kuwa watu hukusanywa kwa pamoja na huwa wanapewa maelekezo yaliyomo kwenye karatasi jinsi ya kutamka utiifu kwa Malkia, na hakuna anayeshurutishwa au kuambiwa ashike Mswahafu wakati anapofanya hivyo, au kusikilizwa anachotamka wakati huo.

 

Kwa hali hiyo, kunaonyesha kuwa hakuna uzito huo ulioutaja na hivyo mtu kuwa na khiyari katika jambo hilo.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida nyenginezo

Shaykh Fawzaan: Kuapa Kwa Kuweka Mkono Kwenye Qur-aan Ni Jambo Halina Dalili

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share