Nini Maana Ya Unajimu (Kutabiri Kwa Nyota) Na Nini Hukmu Yake?
Nini Maana Ya Unajimu (Kutabiri Kwa Nyota) Na Nini Hukmu Yake?
SWALI:
Assalam alakum wa Rahmatoullahi wa Barakatuh;
Nini maana ya unajimu, na upi hukumu yake katika uislam? Jazakallahul khayrun
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Maana ya unajimu ni elimu ya nyota. Unajimu ni elimu ambayo ina manufaa yake katika Uislamu kwa ajili elimu hiyo Waislamu waliweza kusafiri na majahazi na meli kuelekea sehemu nyingi baharini na kwa ajili hiyo Waislamu waliweza kueneza Uislamu na kufanya biashara bila ya matatizo yoyote.
Lakini wapo baadhi ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu wanatumia nyota kutabiri mambo yatakayokufika au yatakayotokea. Kuna wanaotabiri kwa njia ya unajimu (kutazamia nyota) kuhusiana na mwezi aliozaliwa mtu inayojulikana kama 'horoscope'. Unajimu huu hutiwa magazetini na watu husoma kila mara kutabiri bahati zao au shari zitakazowasibu katika siku fulani. Wanadai kuwa sayari kama gemini, taurus, aries n.k. zinahusiana na mwezi wa mtu aliozaliwa na hivyo basi waliozaliwa katika sayari hizo siku hiyo kwao huwaathiri nafsi zao na kadhaa wa kadhaa.
Haramisho la kutazamia kwa unajimu ni katika Hadiyth:
Amehadithia ‘Abdullaah bin ‘Abaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayejichumia tawi katika ujuzi wa unajimu, atakuwa amejichumia tawi katika sihri, na itaendelea kuzidi na kuzidi.” [Abuu Daawuwd kwa Isnaad Swahiyh]
Kusoma elimu hiyo na kuamini ni ushirikina na hivyo dhambi kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu kwa sababu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimza sana tusiwe ni wenye kwenda kwa wapiga bao, ramli au kutizamia kwa kutumia nyota au mkono kwani mwenye kufanya hivyo atakuwa amekufuru kwa aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayemwendea kahini au mpigaji ramli akamuamini asemayo, basi atakuwa ameshakufuru yale aliyoteremshiwa nayo Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).” [Ahmad, na Aswhaabus-Sunan wanne, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb (3047)
Na pia:
((Atakayekwenda kwa mtabiri akamuuliza kitu haitokubaliwa Swalaah yake siku arubaini)) [Muslim]
Na Allaah Anajua zaidi