Kufanyiwa Dawa Kwa Ajili Ya Kuvutia Wateja Kwenye Biashara
Kufanyiwa Dawa Kwa Ajili Ya Kuvutia Wateja Kwenye Biashara
SWALI:
Assalaam Alaykum,
Allaah awajalie kila lilo jema kwa kazi hii ya kuelimisha jamii (Elimu) Na pia ninashukuru kwa majibu ya maswali yenu ambayo yanazidi kunielimisha na kutoa utata ambao nilikuwa nao.
SWALI: Mimi nilifanya biashara ya duka, lakini ikawa pesa nikiza zinapotea katika mazingira ya utata na baadaye nikaona mtaji unakatika nikaacha kabisa. Niliulizia nikaambiwa hiyo ni chuma ulete inatakiwa ufanyiwe dawa, ya kwanza ni yakuweka katika sehemu ya biasha naa ya pili ni ya kupakaa pamoja na mafuta ile kuvutia wateja na kuzuia chuma ulete. Je, ni halali kutumia dawa hizi ilikuzuiya chuma ulete? Au itakuwa ni shirki?
Ni ndugu yenu katika Uislamu
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaana wa Ta'aalaa) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn
Na tunawaombea Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Awabariki pamoja na kuwaondolea matatizo tofauti ya kila aina.
Pia tunapenda kutoa nasiha ya kwamba tunapoandika Jina la Allaah tusiwe ni wenye kuandika kwa mkato kama M/M au M/ Mungu kwani huku kutakuwa ni utovu wa adabu na heshima Kwake na ni bora zaidi kuandika Jina Lake la asili 'Allaah'.
Swali halikueleweka sawasawa japokuwa inaonekana kuwa ni mas-ala ya sihri na majini. Inaonyesha kichwa cha habari na swali lenyewe yanapishana. Na ibara ambayo haikueleweka ni “Chuma ulete”. Jambo muhimu kwa kila Muislamu ni kujikinga na mambo ya sihri na mashetani kwa kusoma badhi ya aya na Surah za Qur’ani na Adhkaar alizozifundisha Nabiy Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Miongoni mwazo ni Suwrah Al-Faatihah, aayah kumi za Suwrah Al-Baqarah (aayah 1 – 5, 255 – 257 na 284 – 286), Suwrah Al-Kaafiruun, Suwrah Al-Ikhlaasw (mara 3), Suwrah Al-Falaq na Suwrah Al-Naas (mara tatu tatu) na Adhkaar ambazo kila mmoja anaweza kuzipata katika kitabu kidogo kinachoitwa Hisn al-Muslim ambacho kinapatika katika kiungo kifutacho:
Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)
Na Allaah Anajua zaidi