Kumfuata Babu Mganga Mkristo Wa Loliondo Anayetibu Kwa Dawa Aliyooteshwa Inafaa?
Kumfuata Babu Mganga Mkristo Wa Loliondo
Anayetibu Kwa Dawa Aliyooteshwa Inafaa?
SWALI
Assalaamun aleikum
Mashekhe wetu Alhidaaya tunawaomba mtuongoze kuhusu huyo babu aliyoko Loliondo anayetibu watu magonjwa sugu kwa kutumia dawa ya mti aliooteshwa kama ilivyojulikana. Baadhi ya ndugu zetu ambao wakaidi kusikia kwamba kwenda huko kuifuata hiyo dawa haifai hawasikii wanakuja na hoja kama zifuatazo:
- La Kwanza Kubwa: Je kwenda kwa Babu ni Shirk?
- wanasema wao wamekwenda kwa imani kuwa mponeshaji ni mungu, je kuna dhambi gani hapo?
- ikiwa tunasema kuwa huyo babu ni kafiri mbona tunakwenda mahospital na madaktari wanaotutibu ni wakristo?
- babu anasema yeye ni mwanadamu kama wengine, kwa hiyo kila mtu amuombe mungu anapokunywa hiyo dawa. Muislam atamuomba Allah je kuna ubaya gani hapa?
- kaletwa mtu amebebwa hawezi kutembea miezi mingi sana na baada ya kunywa hiyo dawa akanyanyuka na kuanza kutembea polepole na umma ikishuhudia? je hii uwongo? imekuwaje hata kaweza kutembea? kaletwa mtu mahtut hazungumzi muda mrefu baada ya kumya dawa akaanza kuzungumza polepole. Hii imekuwa vipi?
- nini hukumu ya mtu aliyekwenda Hija miezi minne tu iliyopita na kwa kuwa anaumwa sana na miguu, amekwenda kwa Babu kuchukua dawa?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kabla hatukuanza kujibu maswali hayo yanayowatatiza Waislamu kutokana na kushawishika na dawa ya mganga huyo, tunapenda kuwatambulisha kwamba Allaah (Subhaanahuu Wa Ta'aalaa) Hakuacha jambo lolote analolihitaji binaadamu katika maisha yake kwa ujumla isipokuwa Amelieleza katika Qur-aan au kupitia Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na kuhusu mas-ala ya ugonjwa amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
"Allaah Ameteremsha maradhi na dawa zake. Kwa kila maradhi kuna dawa yake, basi jitibuni wala msijitibu kwa yaliyo haraamu". [Al-Bukhaariy na Abu Daawuud]
Amesema pia,
"Allaah Hakuteremsha maradhi ila Ameteremsha dawa zake, basi juu yenu (kunyweni) maziwa ya ng'ombe kwani yanatokana na kila aina ya miti." [Hadiyth sahiyh au hasan- Shaykh Al-Albaaniy]
Poza tulizojaaliwa katika Uislamu ni nyingi mno: Qur-aan pekee ni poza:
وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ۙ
Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rahmah kwa Waumini; [Al-Israa: 82].
قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ۖ
Sema: Hiyo ni kwa walioamini ni mwongozo na shifaa. [Fusswilat :44].
Katika Qur-aan pia mna Aayah za Ruqyahh (kinga na tiba) ya kila aina ya maradhi. Pia imetajwa humo kuwa asali ni poza:
وَأَوْحَىٰ رَبُّكَ إِلَى النَّحْلِ أَنِ اتَّخِذِي مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا وَمِنَ الشَّجَرِ وَمِمَّا يَعْرِشُونَ﴿٦٨﴾ثُمَّ كُلِي مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ فَاسْلُكِي سُبُلَ رَبِّكِ ذُلُلًا ۚ يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاءٌ لِّلنَّاسِ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴿٦٩﴾
Na Rabb wako Akamtia ilhamu nyuki kwamba: Jitengenezee nyumba katika majabali, na katika miti, na katika wanavyojenga. Kisha kula katika kila matunda, na fuata njia za Rabb wako zilizofanywa nyepesi (kuzipita). Kinatoka katika matumbo yao kinywaji cha rangi mbali mbali ndani yake mna shifaa (ya magonjwa) kwa watu. Hakika katika hayo, bila shaka ni Aayah (ishara, dalili) kwa watu wanaotafakari. [An-Nahl 16: 68-69].
Kadhalika Suwrah Al-Faatihaah, Suwrah Al-Ikhlaas na Al-Maw’idhataan, pamoja na Suwrah kadhaa na Aayah nyingi ambazo zimethibiti kuwa ni Ruqyah (Tiba na kinga kutokana na Qur-aan na Sunnah) kwa Muislamu.
Pia, habbat sawdaa (haba soda) ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Kuna poza (tiba) katika Habbat Sawdaa (haba soda) kwa kila magonjwa isipokuwa mauti". [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na miti shamba mbali mbali ambayo imethibitika katika elimu ya sayansi kwamba ina tiba ya kila aina ya maradhi (herbal treatment).
Kadhalika maji ya zamzam ni tiba na huponya kwa kile anachoomba kwayo mtu. Anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Maji ya zamzam kwa (jambo liloombewa) wakati wa kunywa". [Swahiyh Ibn Maajah na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]
Pia Al-Hijaamah (kuumikwa/kupigwa chuku) ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameusiwa na Malaika kuhusu umuhimu wake kutokana na dalili zifuatazo:
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amerepoti kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sikumpitia Malaika yeyote miongoni mwa Malaika Usiku wa Israa Wal-Mi’raaj isipokuwa waliniambia (kuniusia) “Juu yako (unasisitizwa) kufanya Hijaamah ee Muhammad”)) [Swahiyh Ibn Maajah 2818, Swahiyh Al-Jaami’ 5672]
Na katika masimulizi ya ‘Abdullaahi bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba ((Malaika walisema: “Ee Muhammad, waamrishe Ummah wako kufanya [kuumika] Hijaamah)) [Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy].
Pia ‘Abdullaahi bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) ameripoti kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Poza imo katika matatu; kuumikwa na Hijaamah, kunywa asali, na kuchomwa chuma cha moto, lakini nakataza Ummah wangu kuchomwa chuma cha moto)) [Al-Bukhaariy, Swahiyh Sunan Ibn Maajah] – Maana ya kukataza Ummah ni kwamba imekatazwa maadam kuna tiba nyinginezo ila ikiwa kwa dharura pindi tiba nyinginezo hazikumfaa mtu na amehitajia kuchomwa moto kwa chuma. Kwa manufaa zaidi, tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho:
Tiba Gani Zimo Katika Qur-aan?
Ni masikitiko kwamba Waislamu wameacha kutambua na kuzitumia tiba hizo ambazo hakika zinamtosheleza mgonjwa kwa magonjwa hata yaliyo sugu. Na wamewaachia makafiri waliothibitisha umuhimu na faida zake nao ndio wanaozitumia kutibu watu katika kila pande za dunia. Wengineo wametumia asali na habbat sawdaa kutengeneza kila aina ya madawa, vipodozi, mafuta ya mwili n.k. na ikawa ni biashara kubwa kwao ya kujichumia mali kutokana na mafunzo ya Dini yetu lakini bado hawakubali haki! Na Wachina hasa wao wamethibitisha tiba ya Al-Hijaamah na hivi sasa zimejaa zahanati zao wanakotibu watu kwa Al-Hijaamah.
Pia kuna Du’aa za kila aina za kujikinga na kujitibu maradhi alizotufunza Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), nazo pia zimeachwa kando na watu badala yake wanafadhalisha waganga washirikina na kama hao wenye ‘Aqiydah potofu kabisa ya kumshirkisha Allaah (Subhaanahuu Wa Ta'aalaa). Hivyo ni kutokana na udhaifu wa imani ya mtu, na kupendelea maisha ya dunia zaidi ya Akhera kwani lau kama Muislamu atatawakali kwa Rabb Wake ‘Azza wa Jalla akafuata tiba zilizohalalishwa katika Qur-aan na Sunnah, atathibitisha imani yake na atapata malipo mema kabisa na atajipeusha na shirki. Bali ambaye atakuwa na imani zaidi ya kutawakali zaidi ya hivyo kwa kufuata Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ifuatayo atakuwa ni miongoni mwa wale watakaoingizwa Peponi bila ya hesabu.
Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ummah zote walipitishwa kabla yangu, nikamuona Nabiy akiwa na kundi dogo la watu, na Nabiy akiwa na mtu mmoja au wawili, na Nabiy akiwa hana mtu yeyote. Kisha nikaonyeshwa idadi kubwa ya watu niliodhania ni katika Ummah wangu, lakini nikaambiwa: Huyo ni Muwsaa na watu wake. Kisha nikatazama nikaona kundi kubwa ambalo nikaamibwa: Hawa ni watu wako, miongoni mwao ni watu elfu sabiini watakaoingia Peponi bila ya kufanyiwa hesabu au adhabu)) Kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka kwenda nyumbani kwake na nyuma yake watu wakaanza kujadiliaina ni nani hao watakaoweza kuwa. Wengineo wakasema: “Labda Nabiy na Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)” Wengine wakasema: “Labda ni wale waliozaliwa katika Uislamu na hawakumshirikisha Allaah kwa chochote”. Walipokuwa wakijadiliana, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatoka na kuja na wakamwambia (waliyokuwa wakiyajadili). Aksema: ((Ni wale ambao wasiojitibu kwa Ruqyah, wala kujichoma chuma cha moto, wala hawaamini rajua nzuri na mbaya, bali wanamtegemea Rabb wao na kutawakali Kwake (Pekee))) ‘Ukaashah bin Mihsan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliposikia alisimama akasema: “Muombe Allaah niwe mmojawapo” Akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Wewe ni mmoja wapo)). Kisha mtu mwengine akasimama na akasema: “Muombe Allaah niwe mmojawapo (pia)”. Akasema: (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((‘Ukhaashah amekutangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Fali au rajua (superstition) ni itikadi ya kubashiria ya ghaibu mfano jicho likimpiga mtu upande wa kushoto hubashiriwa kuwa ni shari, na likimpiga jicho la kulia huamini kuwa ni kheri n.k.
Basi ajiulize aliyekwenda huko Loliondo au anayetaka kwenda, je lipi bora? Aponyeshwe kwa kumshirikisha Allaah (Subhaanahuu Wa Ta'aalaa) kisha hatima yake iwe ni motoni au atawakali kwa Rabb wake na mwisho wake uwe mwema? Kwani kwa vyovyote, hakuna atakayebakia duniani milele bali kila mmoja ataaga hii dunia na aliyeisalimisha nafsi yake kutokana na shirki ndiye atakayekuwa amefuzu kikweli kwenye maisha ya milele. Ama aliyejiendekeza kufuata mapenzi ya kuishi sana duniani kwa kumshirikisha Allaah (Subhaanahuu Wa Ta'aalaa) huyo ndiye mwenye kupata khasara kubwa duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahuu Wa Ta'aalaa):
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ ۖ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١١﴾يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُ وَمَا لَا يَنفَعُهُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ ﴿١٢﴾يَدْعُو لَمَن ضَرُّهُ أَقْرَبُ مِن نَّفْعِهِ ۚ لَبِئْسَ الْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ الْعَشِيرُ ﴿١٣﴾
Na miongoni mwa watu yuko anayemwabudu Allaah ukingoni. Inapompata khayr, hutumainika kwayo; Na inapompata mtihani hugeuka nyuma juu ya uso wake (kurudia kufru). Amekhasirika duniani na Aakhirah. Hiyo ndiyo khasara bayana. Humwomba badala ya Allaah ambavyo visivyomdhuru na wala visivyomnufaisha. Huo ndio upotofu wa mbali.Humwomba yule ambaye dhara yake iko karibu kuliko manufaa yake. Bila shaka ni mlinzi muovu kabisa, na bila shaka ni rafiki muovu kabisa. [Al-Hajj: 11-13]
Kuna fadhila nyingi mno za mwenye kuvumila mitihani, ikiwemo ya kusibiwa na maradhi. Na lau kama Muislamu atazitambua na kuziamini fadhila zake, basi atabakia kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kumchagua kuwa miongoni mwa Aliyewapa mitihani hiyo. Kwa maelezo zaidi tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate kuzijua fadhila hizo na uzidishe imani yako:
04- Subira Anaposibiwa Muislamu Na Maradhi
Ama kuhusu hayo maswali majibu ni yafuatayo:
Swali 1- La Kwanza Kubwa: Je Kwenda Kwa Babu Ni Shirk?
Ndio! Kumfuata huyo Babu bila ya shaka ni shirki ambayo ni dhambi kubwa kabisa isiyosamehewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾
Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48],
Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa anasema:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦﴾
Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa :116]
na Muislamu anayemshirikisha Allaah Ameharamishwa Pepo:
إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾
Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru. [Al-Maaidah: 72]
Na hivyo ni kwa sababu mganga huyo ana itikadi batili ya kumshirikisha Allaah (Subhaanahuu wa Ta'aalaa) kuhusu Yesu (Nabiy ‘Iysa ‘Alayhis-salaam) kuwa ni Allaah, na ‘Aqiydah ya Muumini inapaswa iwe safi kabisa bila ya kumshirkisha lolote kwani haiwezekani kuchangaya ubatilifu na haki pamoja kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قُل لَّا يَسْتَوِي الْخَبِيثُ وَالطَّيِّبُ وَلَوْ أَعْجَبَكَ كَثْرَةُ الْخَبِيثِ ۚ فَاتَّقُوا اللَّـهَ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿١٠٠﴾
Sema: Haviwi sawasawa viovu na vizuri japokuwa utakupendezea wingi wa viovu. Basi mcheni Allaah, enyi wenye akili ili mpate kufaulu. [Al-Maaidah 5:100]
Sababu nyingine kuwa haifai ni kama inavyosemekana kutoka vyombo vya habari na kutoka kwake mwenyewe huyo mtu kuhusu yeye na dawa zake ni kama ifutavyo:
- Ameoteshwa kuhusu hiyo dawa, na hapo kuna mas-ala ya ndoto kwa hiyo dawa inahusiana na mas-ala ya kiroho (spiritual faith).
- Ameweka masharti kadhaa kwamba: (i) lazima unywe hapo hapo mbele yake (ii) hataki kupokea zaidi ya shilling 500 na kazigwa kipato chake (iii) hairuhusiwi dawa hiyo kuhamishwa wala kupelekewa mgonjwa aliye mbali, akifa na afe!
- Fungu ya pesa inaingia katika kanisa, na huko ni kusaidia katika kuineza, kuijenga dini batilifu. Hilo limekatazwa kabisa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
...وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾
Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Maaidah 5:1].
- Pia huko na kuwasaidia katika njama zao za kuipiga vita Dini yetu tukufu ya Kiislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametoa tahadharisho kali kabisa Anaposema:
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ ۗ
وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ﴿٣٦﴾لِيَمِيزَ اللَّـهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا
فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿٣٧﴾
- Hakika wale waliokufuru wanatoa mali zao ili wazuie njia ya Allaah. Basi watazitoa, kisha itakuwa ni majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam. Ili Allaah Apambanue waovu na wema, kisha Aweke waovu juu ya waovu wengine, kisha Awarundike pamoja Awatie katika Jahannam. Hao ndio waliokhasirika.[Al-Anfaal 8:36-37].
-
Mtu anapopewa dawa hiyo kuinywa anapewa kwa kufuatiwa na maneno ya bwana akuponye, au upone kwa jina la bwana, au kwa jina la Yesu n.k. Na yote hayo ni ushirikina. Muislamu huomba kwa jina la Allaah na haombi kwa jina la Yesu.
- Na hata kama Muislamu yeye atasema au kudai kuwa yeye wakati anapokunywa, basi humtaja Allaah au humuitakidi Allaah na si Yesu, basi tunamfahamisha kuwa misingi ya dawa hiyo ni batili na kila jambo ambalo husimamishwa au kujengwa kwa misingi batili basi shari’ah ya Dini yetu hulipinga na huwa ni batili. Kwa hali zozote atakazodai kunywa kwazo hiyo dawa, basi haitokubalika wala kumsaidia.
- Imethibiti kwa mamia ya watu waliokwenda kuwa hawajapona na wengine wamefariki baada ya muda si mrefu na hakuna ushahidi kuwa dawa hizo ndizo ziponyeshazo, na hata kwa ushahidi wa madaktari ambao wengine ni wakiristo walioonekana kwenye vyombo vya habari wamelalamika kuwa baadhi ya wagonjwa wao wamerudi na kuwa ta’abaan zaidi kwa kuacha madawa na masharti waliyopewa na madaktari wao na kutegemea kikombe cha maji ya huyo babu muongo wa kanisa.
- Watu waongo, wajanja, malaghai wa namna hiyo wanaodai kuoteshwa, wenye malengo ya kutafuta umaarufu, utajiri au kutangaza dini zao kwa njia kama hizo za kudai kuoteshwa, hawajaanza leo, na wataendelea kutokeza wengi.
- Tunasema, hata akitokea Muislamu ambaye atakuwa na madai kama ya huyo babu wa kanisa, basi madai yake hayatokubaliwa na yatakuwa batili hata kama atayaegemeza na Uislamu. Hakuna wa kuoteshwa wala kuletewa ufunuo hivi sasa. Hizo ni njia za kitapeli za kujitafutia umaarufu na utajiri wa njia ya mkato. Na wajinga ndio waliwao.
SWALI 2- Wanasema Wao Wamekwenda Kwa Imani Kuwa Mponeshaji Ni Allaah, Je Kuna Dhambi Gani Hapo?
Nadhani hilo tumeshalijibu katika nukta ya kwanza inayohusiana na ‘Aqiydah ya mganga na kwamba haiwezekani kuchanganya ubatilifu na haki hata kama nafsi inadhania kuwa ni jambo jema. Na juu ya hivyo ni kuijidanganya na kufuata matamanio ya nafsi vile inavyotaka kuitikadi ili tu kujiridhisha nafsi kwa jambo lilokwishabainishwa kuwa haramu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya kujiepusha na mambo yanayotia shaka kwamba yanampeleka mtu motoni.
Amesema: ((Hakika halali imebainika na haramu imebainika (ziko dhahiri, waziwazi). Baina ya mawili hayo mna yenye kutia shaka. Wengi miongoni mwa watu hawayajui. Basi atakayejiepusha yenye kutia shaka atakuwa amejiepushia shaka katika Dini yake na heshima yake. Na Atakayetumbukia katika yenye kutia shaka, ataingia kwenye haramu... [Al-Bukhaariy na Muslim]
SWALI 3- Ikiwa Tunasema Kuwa Huyo Babu Ni Mzungu Mbona Tunakwenda Mahospital Na Madaktari Wanaotutibu Ni Wakristo?
Shari’a ya Kiislamu imeweka wazi kila jambo. Katika kutafuta poza kwa kutibiwa na madaktari, inampasa Muislamu kwanza atafute daktari Muislamu. Lakini pindi akikosa ndipo ameruhusiwa kutibiwa na daktari asiyekuwa Muislamu. Ni sawa na mwanamke anayehitaji kutibiwa magonjwa ya kike yanayohitajia kuchunguzwa sehemu zake za siri kwamba anapaswa amtafute kwanza daktari mwanamke Muislam, pindi akimkosa, atafute daktari miongoni mwa Ahlul-Kitaab (waliopewa Kitabu; Mayahudi na Manaswara). Atakapokosa basi hana budi kutibiwa na daktari mwanamke mwenye dini yoyote nyingine. Na mwishowe akikosa hapo anaweza kutibiwa na daktari mwanamume aliye Muislamu na kuendelea kama tulivyotaja juu. Lakini hivyo ni mwenye ugonjwa unaohitaji atibiwe ka dharura.
Lakini, ikiwa daktari yeyote asiyekuwa Muislamu akijulikana tu kuwa anatibu kwa kutumia itikadi yake ya upotofu, basi hapo hakuna shaka ila kuepukana naye kwa hali yoyote. Lakini ikiwa madaktari hao wanatumia tiba zao kutokana na elimu ya sayansi waliyojifunza isiyohusiana na itikadi yoyote ya dini zao au itikadi yoyote ile ya kishirikina, basi kutakuwa hakuna uharamu wa kutibiwa nao.
SWALI 4- Babu Anasema Yeye Ni Mwanadamu Kama Wengine, Kwa Hiyo Kila Mtu Amuombe Allaah Anapokunywa Hiyo Dawa. Muislam Atamuomba Allaah Je Kuna Ubaya Gani Hapa?
Kwanza: Hilo pia takriban sawa na Swali la nukta ya tatu, mme na tano, na jibu lake ni katika jibu la nukta ya kwanza na ya pili.
Pili: Juu ya hivyo hizo ni propaganda zenye mielekeo ya kidini na kutaka kuimarisha kanisa! Suala la mtu kudai kaoteshwa na Yesu na kutengeneza dawa inayotibu maradhi kadhaa tena yaliyowashinda mpaka sasa wanasayansi na wataalam wa tiba kuyapatia ufumbuzi ni jambo lisilo na shaka kuwa ni mipango na mbinu za hao jamaa kujitangaza na kuweza kwa njia moja au nyingine kuwatoa wale wenye imani dhaifu katika dini yao ya kweli. Wamesikika baadhi ya viongozi wa makanisa wakiunga mkono na kutetea na hata kupambana kwa nguvu na serikali dawa hiyo isifanyiwe uchunguzi ikiwa inatibu na vipimo vyake ni sahihi, na hata wengine wanafanya propaganda ya kuujengwa hospitali rasmi hapo ili kuimarisha dawa na itikadi za kanisa.
Na kuonekana kuwa hizo ni mbinu za kanisa waziwazi, baadhi ya makanisa mengine yaliyo na madhehebu tofauti na dhehebu la huyo babu wamekadhibisha hizo mbinu za huyo mzee na wamepinga ukweli wa madawa hayo na uhusiano na Yesu na kanisa! Sasa ikiwa wao wenyewe hawajakubaliana na ya kwao, je, haiwi tu ni fundisho kwa Waislamu kutanabahi mchezo unaochezwa hapo? Lakini mgonjwa ambaye imani yake ya dini ni dhaifu na isitoshe kaishakata tamaa ya kupona, huwa ni rahisi kukubali wito wowote ule atakaoletewa wa 'kupona' au wa kutibu maradhi yake aliyoyakatia tamaa! Na huo ndio mtihani na si rahisi kumkinaisha mtu wa aina hiyo mpaka kwanza imani yake ya dini ikuzike na kuimarika. Ndio maana Waislamu wengi wanaokatazwa kwenda huko wanakuwa hawasikii lolote lile; Aayah wala Hadiyth haimuingii kwani imani yake bado haijaimarika, utakuta mtu hata kuswali tabu, na wengine wengi hawajui hata mambo ya msingi ya dini yao. Ndio tunaona tukio hili ni funzo kubwa na muamsho kwa wasimamizi, waalimu, mashaykh na maimaam na walinganiaji kuweza kuongeza kasi ya kuifunza jamii dini yao na kuwapa mwamko wa dini yao na kuwazindua na hatari ya kuchezewa katika imani zao. Na vilevile tukumbuke daima kuwa makafiri hawatoridhika daima abadan hadi Waislamu waache mila yao na kufuata mila zao. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَلَن تَرْضَىٰ عَنكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَىٰ حَتَّىٰ تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ ۗ
Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao. [Al-Baqrah: 120]
Tatu: Muislamu hatakiwi kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) mbele ya mkristo. Hapo atakuwa amechanganya waungu wawili, kwani hiyo dawa imeambatana/inahusiana na mungu wa babu ambaye anaamini Allaah wake ni Yesu. Haiwezekani mtu kuwa na nyoyo mbili; moyo unaotaka kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Pekee na moyo unaotaka kuchanganya shirki. Anasema Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa):
مَّا جَعَلَ اللَّـهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ ۚ
Allaah Hakufanya mtu yeyote kuwa na nyoyo mbili kifuani mwake; [Al-Ahzaab 33:4]
Na hizo ni mbinu zake huyo babu kama zilivyo mbinu za makafiri wengineyo kuwapendezesha dini yake na kuwavuta watu kwenye dini yake kwa njia hiyo na kuwawekea watu kiwango kidogo cha pesa kuwahadaa ili waone kuwa lengo lake si utajiri. Lakini kiwango hiko kidogo kwa maelfu waliohadaika leo kimempatia utajiri na kinapangiwa kujenga nguvu ya kanisa. Werevu ndio wenye kuzinduka.
SWALI 5- Kaletwa mtu amebebwa hawezi kutembea miezi mingi sana na baada ya kunya hiyo dawa akanyanyuka na kuanza kutembea polepole na umma ikishuhudia? je hii uwongo? imekuwaje hata kaweza kutembea? kaletwa mtu mahtut hazungumzi muda mrefu baada ya kumya dawa akaanza kuzungumza polepole. Hii imekuwa vipi?
Kwanza: Hilo si ajabu hata kidogo, kwani hata dawa na tiba za Kiislamu kama tulizozitaja zinamwezesha mtu aliye mahtuti kuinuka ghafla au akapona. Mfano wa Suwrah Al-Faatihah ambayo Swahaba walimsoema mkuu wa kijiji aliyeumwa na nge akawa mahtuti kukaribia kufa, akapona. Kuna waliopata shifaa kabisa kwa kunywa maji ya zamzam; kwa haraka kuna mfano wa watu wawili, mmoja mtu wa makamo alikuwa hawezi kuswali kwa kusimama kwa kufa nguvu miguu yake na baada ya kunywa maji ya zamzam alipokuwa Hijjah mara akaweza kuswali kwa kusimama japokuwa kwa miaka mingi alikuwa akiswali kwa kukaa kwenye kiti. Mwengine ni majuzi tu alielezea mwenyewe kijana huyo kuwa alikuwa hasikii na kuzungumza kwa miaka mingi na alipokuwa Hijjah akanywa maji ya zamzam akawa anaweza kusikia tena na kuwashangaza wengi waliokuwa wakimjua. Kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"Maji ya zamzam ni kwa kile kilichonywewa" [Swahiyh Ibn Maajah na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy] Yaani kwa Niyah ya mnywaji wakati anapoyanywa maji hayo na kile alichoomba (du’aa ya kitu fulani anachohitaji) wakati anayanywa, na huku ana imani kamili na yakini ya tiba yake na kuyaamini maneno hayo ya Nabiy wetu.
Pia kuna visa vingi vya kuaminika kutokana na matibabu ya Hijaamah (kuumikwa/kupigwa chuku). Iliyowaponyesha watu maradhi sugu kadhaa; cancer, maradhi ya moyo, high blood pressure, ukosaji wa uzazi (infertility), kufa ganzi (paralysation), kichwa sugu (migrane), kila aina ya maumivu ya mwili, mgongo, viungo (rheumatic pain and muscles), macho na mengi mengineyo. Mfano, mwanamke ambaye mkono wake wote mmoja ulikufa ganzi (Paralyzed) kwa muda mrefu, na baada tu ya kutibiwa kwa Hijaamah alianza kupata hisia na mkono ukaanza harakati. Mwanamke mwengine aliyekuwa hakujaaliwa kupata kizazi miaka kadhaa, na baada ya kutibiwa kwa Hijaamah alishika mimba na akajaaliwa kuendelea kupata kizazi. Pia mwanamke aliyebanwa na mshipa wa mgongo na kiuno (sciatic nerve) aliyeshindwa kutembea vizuri na hata kunyanyua mguu kutawadha ilikuwa ni shida, lakini baada ya Hijaamah aliondokewa na maumivu na akaweza kutembea vizuri siku ya pili yake tu! Na daktari aliyekuwa kafiri, aliyevimba mguu, na alipofanyiwa tiba ya Hijaamah, na baada ya kuifanyia utafiti damu iliyovutwa kutokana na Hijaamah alitambua kuwa ni damu iliyokusanya sumu na kila aina ya uchafu (toxins) inayoziba mishipa ya damu mwilini. Alipoulizwa na kuambiwa kuwa ni dawa ya Nabiy (Swalla Allaahu wa ‘alayhi wa aalihi wa sallam) miaka zaidi ya elfu kumi na nne naye ni Ummiyy (asiyejua kusoma na kuandika) aliamini kwamba amesema maneno ya wahyi na akachukua shahada. Naye alipona maradhi yake. Na hivi vyote ni visa vya kweli na vikielezwa na wenyewe. Na yote hayo ni kwa Tawfiyq ya Allaah na matakwa Yake.
Pili: Huenda mtu akauliza swali kama hilo kwamba: “Vipi basi Allaah Ampe uwezo kafiri wa kutibu watu kama hivyo?” Jibu ni kwamba Allaah (Subhaananu wa Ta’aalaa) Ameweka mitihani Yake katika njia nyingi na sababu nyingi.
Na hata kama angekuwa ni mganga wa kweli na tiba ya kweli isiyo na mashaka wala ushairikina ndani yake, basi tunapaswa kujua kuwa Allaah Hakuwazuia makafiri wasiwe na ujuzi wa elimu ya aina yoyote. Ila tu Ameweka mipaka Yake kama Anavosema:
وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ
Wala hawawezi kufikia kuelewa chochote kuhusu ujuzi Wake isipokuwa kwa Alitakalo. [Al-Baqarah: 255].
Na hiyo ni miongoni mwa Rehma Zake ‘Azza wa Jalla kwa makafiri kwani ingelikuwa si Rehma Yake, basi kafiri asingeliweza hata kupata maji ya kunywa! Na kumiminiwa kwao Rehma za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) za uhai, afya, mali, watoto, ujuzi, si kwamba Anawapenda, bali kuzitumia kwako neema hizo ni mitihani na wao kuzidisha kufru zao:
((Wala wasidhani wale wanaokufuru kwamba huu muhula Tunaowapa ni kheri yao. Hakika Tunawapa muhula wazidi madhambi. Na juu yao wao ni adhabu ya kuwadhalilisha)) [Aal-‘Imraan 3:178].
فَذَرْهُمْ فِي غَمْرَتِهِمْ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٥٤﴾أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ ﴿٥٥﴾نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ ۚ بَل لَّا يَشْعُرُونَ ﴿٥٦﴾
Basi waachilie mbali katika mkanganyiko wao kwa muda. Je, wanadhani kwamba kwa vile Tunavyowakunjulia kwa mali na watoto. Tunawaharakishia katika ya khayr? Bali hawahisi.[Al-Muuminuwn: 54-56]
Kwa hiyo huyo mganga huenda naye akawa anaachiwa tu aendelee kujiaminisha itikadi yake potofu huku Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anamkokotezea adhabu. Na hilo ni dhahiri kwani hivi karibuni wameshaibuka wengineo huko Tanzania wanaodai nao kuwa ima wameoteshwa kama alivyooteshwa huyo babu. Nao ni mwanamke aliyedai kaoteshwa na Maryam mama yake Yesu kama wanavyodai. Na kuna baadhi ya wenye majina ya Kiislamu wamejitokeza nao na kufuata nyendo hizo za hao makafiri na kutafuta ima utajiri au umaarufu kwa mgongo wa ‘ndoto’ za tiba.
SWALI 6- Nini Hukumu Ya Mtu Aliyekwenda Hija Miezi Minne Tu Iliyopita Na Kwa Kuwa Anaumwa Sana Na Miguu, Amekwenda Kwa Babu Kuchukua Dawa?
Hukmu yake atakuwa amemshirkisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na tumeshataja juu kwa dalili za Aayah kwamba anayemshirikisha Allaah hatasamehewa madhambi yake na wala hataingia Jannah (Peponi) isipokuwa akirudi kutubia kikweli. Na hivyo atakuwa ameiharibu hijjah yake kwani haki na ubatilifu hauchanganywi! Na hiyo ni moja ya dalili kuwa Hijjah ya huyo mtu haikutakabaliwa. Mtu anapotoka Hijjah alama za kukubaliwa Hijjah yake ni kubadilika matendo yake na kuwa bora na mema na kuwa mbali na maasi na madhambi. Na si kutumbukia katika ushirikina. Ima awe mtu huyo hana elimu ya dini na hajui anachokifanya, na ikiwa ni hivyo, mtu huwa hana udhuru katika mazingira ambayo kuna waliosoma, wenye elimu, mashaykh, maimaam, walinganiaji na wenye ujuzi wa Dini ambao angeweza kuwauliza na kuwataka ushauri. Hivyo, kwa mazingira tuliyonayo na zama tulizonazo, mtu anakuwa hana hoja ya kufanya jambo bila elimu.
Tunawaombea ndugu zetu Waislamu waliofikwa na masaibu ya maradhi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Awathibitishie imani zao na wadumishe subra ili wabakie salama katika ‘Aqiydah zao na wapate ujira mwema kabisa wa Pepo ya milele. Na tunawaomba wale waliokwishakwenda warudi kutubia kwa Rabb wao toba ya kweli ‘asaa Allaah ‘Azza wa Jalla Awasamehe. Na wale waliofariki (ambao si wachache) kabla ya kufika na baada ya kufika na kunywa dawa hiyo ya huyo babu muongo, wakawa wamefanya hayo kwa ujinga na kutokujua na haikuwabainikia ushirikina uliokuwepo, wakafariki katika hali hiyo, tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Awaghufurie nao vilevile.
Na Allaah Anajua zaidi