Kuandikiwa Kombe Na Kufukizwa Vikaratasi Vinavyoandikwa Inafaa?
Kuandikiwa Kombe Na Kufukizwa Vikaratasi Vinavyoandikwa Inafaa?
SWALI:
Assalam Alaykum kwanza napeleka shukran zng za dhati kwake subhanahu wataala, thumma nyie mlojitolea fiysabilillah kutuokoa sisi ktk shirki na kuyarekebisha matendo yetu, suali langu je mtoto mdogo kuandikiwa ktk vikaratas hati zisojulikana na kuambiwa uviroweke kisha umnyweshe (kombe) inafaa? Sina mushkila ikiwa itandikwa qur-an au dua bali mushkila ktk hati zisojulikana au kuchanganya aya na hati nyengine za kiarab au kuvichoma nakumfukiza mtoto
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kuhusu kombe, japo inaandikwa kwa maandishi yanayofahamika ya Aayah za Qur-aan ingawa kuna baadhi ya 'ulamaa wamesema inafaa kwa kudai kuwa Swahaba Ibn ‘Abbaas alitumia, lakini Qauli yenye nguvu na 'ulamaa wengi wanapingana nayo kwa kutokuwa na ushahidi sahihi wa hili na pia kutofundishwa njia hiyo na Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alifundisha njia zote za kutibu au kujikinga na uchawi, husda, kijicho, na hayo ya marohani n.k. kwa kutufundisha du’aa mbalimbali na Aayah za Qur-aan ambazo baadhi yake tunakutajia chini. Hivyo, ni bora uachane na hayo mambo ya kombe ambayo yana utata na ufuate zile njia sahihi zilizothibiti. Baadhi ya wanaojiita Mashaykh na waalimu wanatumia njia hizo kula pesa za Waislam.
Njia nyengine ni kuwa na muda wa wewe mwenyewe kusoma zile Aayah na Suwrah ambazo ni kinga kwa Muislamu kama alivyotufundisha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama Suwrah Al-Ikhlaasw, Al-Falaq na An-Naas asubuhi na jioni. Na Suwrah Al-Baqarah Aayah za 1-5, 255–257 na 284–286. Na pia kusoma Qur-aan sana. Pia kusoma Adhkaara za asubuhi na jioni ambazo pindi ukizidumisha basi zitakutosheleza kabisa kujikinga wewe na familia yako kutokana na kila balaa na shari . Nazo zinapatikana katika kiungo kifuatacho:
027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni
Na nyiradi na du’aa zote nyinginezo utakazozihitaji katika maisha yako ya kila siku utazipata katika kitabu kifuatacho. Na humu pia zimo du’aa za kuwakinga watoto:
Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)
048-Hiswnul-Muslim: Du’aa Ya Kuwakinga Watoto
Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akupatie shifaa kwa njia iliyo sahihi.
Na Allaah Anajua zaidi