Anataka Kujua Hukumu Ya Kumfanyia Mazingaombwe Mume Wake Ili Ampende
Anataka Kujua Hukumu Ya Kumfanyia Mazingaombwe Mume Wake Ili Ampende
SWALI:
Assalamu aleykum warahmatullah wabarakatuh.
Napenda kupongeza uongozi mzima wa Al-hidaaya kwa kazi nzuri waifanyayo. Swali langu ni kutaka kujua kutia viini vya macho kwa kumrembea mume vibaya?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Mazingaombwe ni aina ya udanganyifu na mara nyingi huingia uchawi na sihri. Udanganyifu katika Uislamu haufai, kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Mwenye kutudanganya si katika sisi" [Muslim].
Ama kwenda kwa mchawi au mtizamiaji au mpiga bao ni shirki na hivyo haifai kishari’ah kabisa. Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾
Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno! [Luqmaan : 13].
Mwenye kwenda kwa mtazamiaji Swaalah yake haikubaliwi siku arubaini. Na tufahamu shirki ni dhambi kubwa sana linalomtoa mtu katika Uislamu.
Kwa hiyo, inatakiwa kwa mke amfanyie mumewe mambo mazuri ya kishari’ah ambayo yatamfanya mumewe ampende kidhati. Huko ni kama:
1. Kuwa msafi daima na kujirembesha kwa ajili yake.
2. Kumfanyia mambo mazuri na mema.
3. Kumtii kwa lisilokuwa la haramu.
4. Kulinda heshima yake kwa kutofanya ya haramu.
5. Kumpikia kwa avipendavyo, vilivyo vizuri.
6. Kumliwaza na kumpooza anaporudi nyumbani.
7. Na mengi mengineo.
Na Allaah Anajua zaidi