Amekwenda Kwa Mtabiri Kutazamiwa Mkono Nini Hukmu Yake?

 

Amekwenda Kwa Mtabiri Kutazamiwa Mkono Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalam alykum warhmatullahi wabarakatu, ahsanteni kwa maelezo yenu, ishaallah mola atakupeni kila lenye kheri, palokua pazito ishaallah atapafanya pepesi juu yenu, ahsanteni sana kwa elimu yenu mlonipatia. ishaallah mola     atajalia nizisome nyiradi na dua mlizonipa kadri ya uwezo wangu ,na kwa uwezo wa allah atazipokea. nimepokea nasaha       zenu kwa moyo mmoja wala mimi sijaelekea huko hilo toeni hofu mimi najua mola hana mshirika,   laillah hailallah muhammada rasulullah, mimi nipo  london je mkowapi nyinyi? no yangu hii *********** zaidi nahitaji dua zenu juu yangu hifazghi ya mola juu ya maisha yangu, akili yangu bado haijachanganya,metia nia nije africa mwezi wa saba sasa kama itawezekana nataka nikuoneni, na kama hamuwezi kunipigia basi nipeni no yenu nitakupigieni, kuna mtu kanitizama mkono wangu, kanambia kuna mtu ananifanyia mambo ya kiswahili na bado anaendelea,sasa je kweli kama mtu katizama mkono wako na anauwezo wa kuona chochote,na hanijui

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Ndugu yetu, inaonyesha hukupokea nasaha zetu au hukuzitilia maanani, tulikutahadharisha kwamba usije kuingia katika shirki, lakini umetumbukia huko huko kwa kutazamiwa mkono wako na mtabiri!  Sasa utambue kwamba hukmu yake ni kama ifuatavyo:

 

1.     Kama ulikwenda kwa huyo mtabiri Dajjaal na kukubali aliyokwambia na kuyaamini basi umekufuru kwani umekanusha Qur-aan inayosema kuwa hakuna ajuaye mambo ya ghayb isipokuwa Allaah Pekee na wewe  kwenda kwa huyo mtazamiaji au kumkaribisha akutazamie ni kuthibitisha kinyume cha ilivyothibitisha Qur-aan  na huku ni kujitoa katika Uislamu na ni kufr. Dalili ni:  

((من أتى كاهناً فصدقه بما يقول فقد كفر بما أنزل على محمد صلى الله عليه وسلم))  رواه أبوداود

((Atakayemwendea mchawi na kuamini aliyoambiwa, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad [Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam])) [Abu Daawuud]

 

2.     Kama umekwenda kwa huyo mtazamiaji Dajjaal na kuangaliwa mkono kisha ukamuachia aliyoyasema bila ya kuyaamini wala kukushughulisha katika maisha yako ukawa unaona kuwa hakuna chochote cha maana basi hukumu yake ni kuwa Swalah zako za siku 40 hazikubaliwi; hata hivyo itakulazimu uswali kwani ni wajibu usiodondoka kwake; ni ahadi baina yao na Mola wako lakini hazitokubaliwa. 

((من أتى عرافاً فسأله عن شئ لم تقبل له صلاة أربعين ليلة)) مسلم

((Atakayekwenda kwa mtabiri akamuuliza kitu haitokubaliwa Swalah yake siku arubaini)) [Muslim]

 

Kama alikujia wewe au aliletwa kwako huyo mtabiri Dajjaal na kutazamwa au kusomwa mkono wako na kuambiwa ulichoambiwa; kisha ukamwambia huyo mtabiri mfano wa kauli "wewe ni katika waongo wakubwa na ni vyema uache uongo wako na kutafuta la kukusaidia katika dunia yako na Akhera yako"  basi  msimamo huo pekee utakuwa huna kosa ulilofanya In shaa Allaah.

 
Wengi wetu huwa tunakwenda baada ya kufikwa na matatizo na hilo lina maana kuwa tuna iymaan na itikadi hata kama ni 0.01 kuwa wao wana uwezo wa kutatua matatizo na wana uwezo wa kuondoa madhara na kuleta manufaa na hili ni katika yanayomuhusu Allaah Pekee hivyo huwa tumeingia katika shirki kubwa na hivyo kuporomosha ‘amali zetu zote bila ya kuhisi wala kuelewa.

 

Nasaha zetu kwako tunakupa haraka urudi kutubu kwa Mola wako tawbah ya kweli, kwani usipofanya hivyo na pindi ikawa ni ajali ya mauti yako, basi utaharamishwa na Pepo kama Anavyotahadharisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru. [Al-Maaidah: 72]

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate makala zinazohusu tawbah na jinsi ya kufanya tawbah ya kweli:

 

Tawbah Ya Kweli Na Masharti Yake

 

Tawbah

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share