Kutundika Jina La Allaah (عَزَّ وَجَلَّ) Na Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) Sambamba Ukutani Au Msikitini
Kutundika Jina La Allaah (عَزَّ وَجَلَّ) Na Muhammad
(صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) Sambamba Ukutani Au Msikitini
SWALI:
Jee kuweka saa au majina Allaah Subhaanahu wa T'aalaa au ya Rasuli Allaahu Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam mbele ya msikiti inafaa.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Miongoni mwa vitu ambavyo Shari’ah ya Kiislamu inashinikiza ni kuwekwa pamoja na kuunganishwa kwa Shahada ya Upweke wa Allaah na Shahada ya Ujumbe wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mifano wa miunganisho hii inaonekana katika Adhana ya Swaalah na katika Iqaamah. Kwa uzaidi, pia katika Hadiyth ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufundisha:
"Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: kushuhudia kwamba hapana Rabb [Anayestahiki kuaabudiwa kwa haki] isipokuwa Allaah, na ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Rasuli wa Allaah…"
Hii inawakilisha yale ambayo Mukallaf anapaswa kuamini. Mukallaf ni mtu ambaye Kishari’ah ana uwezo, ana jukumu juu ya vitendo vyake anavyovifanya, na anahitajika kutekeleza yale aliyoamrishwa, ambayo katika Shari’ah ya Kiislamu, yanaanza pindi anapobaleghe. Lazima [hizi Shahada mbili] zifahamike kwa pamoja, na kutamkwa kwa pamoja kama ni ushahidi wa imani.
Ama kuhusiana na swali lako kwa kuziandika katika maandishi yaliyoungana ima Msikitini, majumbani na penginepo, hakuna chochote katika haya ambayo yanaweza kupatikana katika Kitabu cha Allaah au katika Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na natija yake ni kwamba kuna hatari kubwa ndani ya jambo hili [kwa sababu haliko katika Qur-aan wala katika Sunnah]. Kwani haya yanafanana na kanuni ya kiongo ya utatu (trinity) ambayo iko katika Ukristo, dhana ambayo inadai kuwa; baba, mwana, na roho mtakatifu ni mungu mmoja. Zaidi ya hayo, tabia hii ya kuunganisha jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kimaandishi, inaweza kuchukuliwa kuwa kama nembo inayowakilisha dini ya kiongo ya umoja wa kuwepo. Kwa ujumla, inaweza kutumiwa vilevile kutetea uvukaji wa mipaka juu ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuabudu yeye pamoja na Allaah.
Kwa hiyo, kuandika jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) pamoja na jina la Nabiy wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hali kama hii (ya kufanya maandishi ya majina yao yaungane na kuyapandisha maandishi ya majina yao moja juu ya mwenzie, au moja pembeni ya jingine), lazima ikatazwe. Hairuhisiwi hata kuandika (Allaah - Muhammad) katika mlango wa Msikiti, au katika sehemu nyingine yoyote, hii ni kwa sababu ya utata, mawakilisho yasio ya kweli, na mashaka mazito yaliyokwishafafanuliwa na kuonywa juu ya jambo hilo hapo nyuma.
Soma makala ifuatayo kwa faida zaidi:
Je, Umenilinganisha Mimi Kuwa Sawa Na Allaah?
Na Allaah Anajua zaidi