Ukitaka Kitu Sana Ina Maana Unakiabudu?

 

Ukitaka Kitu Sana Ina Maana Unakiabudu?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum, wahusika wa site hii na yeyote anayesoma. Namshukuru Allah kwa kuniwezesha kupata nafasi hii ya kuuliza maswala. Na pia napenda kuwapongeza wahusika wote wa site hii kwani ina mafundisho mengi.

 

Swala langu ni je matamanio yanaweza kumfanya mtu amshirikishe Allaah? Kwa mfano mtu unakitaka kitu fulani kupita kiasi, kila wakati unakiwaza. Siku haipiti kama hujakiwaza, hata usiku unakiwaza. Unamkumbuka Allaah lakini si kwa muda mrefu kama unavyokikumbuka hicho kitu. Au unasoma dhikri lakini akili yako iko katika kitu chengine. Je utakuwa unamshirikisha Allaah? Na je kama unajitahidi kuweka akili kwenye adhkaar lakini japo mara moja unakuja kufikiri kitu chengine ufanye nini? Kwani tangu nilipoisoma ile Aayah ambayo inasema hivi:

 

 Je, umemuona yule aliyefanya hawaa yake kuwa ndio mwabudiwa wake? 

 

Je, inamaanisha vile ambavyo nilielezea? 

 

JIBU: 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ili kupata ufumbuzi wa Swali lako inabidi  turudi katika Tafsiyr ya Qur-aan  Hapa itatosha kunukuu Aayah mbili ambazo zinazungumzia kuhusu mas-ala ya hawaa (matamanio). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:  

أَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ أَفَأَنتَ تَكُونُ عَلَيْهِ وَكِيلًا ﴿٤٣﴾

Je, umemuona yule aliyefanya hawaa yake kuwa ndio mwabudiwa wake?  Je, basi utaweza wewe kuwa ni mdhamini wake? [Al-Furqaan: 43]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّـهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ﴿٢٣﴾

Je, umemuona yule aliyejichukulia hawaa zake kuwa ndio mwabudiwa wake, na Allaah Akampotoa juu ya kuwa na elimu na Akapiga mhuri juu ya masikio yake na moyo wake; na Akaweka kifuniko juu ya macho yake? Basi nani atamuongoa baada ya Allaah? Je, basi hamkumbuki? [Al-Jaathiyah: 23]

 

Wafasiri wanasema: “Je! Umemwona aliyefanya hawaa (matamanio) zake kuwa ndiye mwabudiwa wake.

 

Kwa maana: Mtu awe ni mtumwa wa hawaa zake, mtu ni kufanya analotaka hata kama Allaah ('Azza wa Jalla)   Ameharamisha, na kutofanya asilopenda japokuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Amelifanya ni waajib.

 

Ikiwa mtu ataanza kutii kwa namna hii, inamaanisha kuwa mwabudiwa wake si Allaah bali ni yule anayemtii bila kuuliza maswali, na bila kujali kama anamuita bwana kwa ulimi wake au laa, au kama anachonga sanamu lake na kuliabudu au laa. Kwani anapomuabudu moja kwa moja bila suala, inatosha kumfanya yeye ni mwabudiwa; na baada hii shirki ya kimatendo, mtu hawezi kutolewa kutokuwemo katika uhalifu wa shirki kwa sababu tu hakukiita kitu anachokiabudu kuwa ni mwabudiwa kwa mdomo, wala hakukisujudia”.

 

‘Ulamaa wa Tafsiyr ya Qur-aan wengi wametoa tafsiri hiyo hiyo kwa Aayah hizo.  

 

Ibn Jariir amesema: “Amefanya hawaa zake kuwa ni mwabudiwa wake: Alitekeleza yanayopenda nafsi yake, bila kujali vitu vilivyoharamishwa na Allaah kuwa ni haraam, wala hakuchukulia vilivyohalalishwa na Yeye kuwa halaal”.

 

Abu Bakr al-Jaswaasw anatoa maana ifuatayo: “Anatii matamanio yake kama mmoja anavyomtii Allaah”.

 

Naye az-Zamakhshari anaeleza kama ifuatavyo: “Anatii hawaa (matamanio) ya nafsi yake; anafuata nafsi yake pindi tu inapomuita, kama kwamba ananitumikia kama anavyotakiwa kutekeza maagizo ya Allaah”.

 

Ash-Shawkaaniy anasema: “Kafiri amechukua dini yake kwa anavyotamani yeye. Hatamani kitu isipokuwa hukifuata bila kutizama kinachompendeza Allaah na kumridhisha au kinachomchukiza na kumkasirisha. Au maana yake ni anaabudu anachotamani au anachokiona kizuri”.

 

Huyu mtu ambaye ni Muislamu kisha akafanya hayo na kuyafuata, huwa amejifananisha na kafiri na hilo halistahiki kwa Muumini.

 

Na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

عَنْ أَبِي مُحَمَّدٍ عَبْدِ اللَّهِ بِنْ عَمْرُو بِنْ العَاصِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وآله وسلم: ((لا يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يَكُونَ هَوَاهُ تَبَعَاً لِمَا جِئْتُ بِهِ)) حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ، رَوَيْنَاهُ فِي كِتَابِ  الْحُجَّةِ  بِإِسْنَادٍ صَحِيحٍ.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muhammad ‘Abdillaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hatoamini mmoja wenu mpaka hawaa (matamanio) zake yatakapomili kutii yale niliyokuja nayo.” [Hadiyth Hasan Swahiyh, katika Kitabu “Al-Hujjah” kwa Isnaad Swahiyh]

 

Ikiwa mtu hatafuata muongozo huu basi hiko tayari ni cheti cha yeye kufanya anachotaka. Na pia tutazame Hadiyth ifuatayo:

 

عن أبي مَسْعُودٍ عُقْبَةَ بن عمرو الأَنْصَارِيّ البَدْرِيّ رضي اللهُ عنه قال : قالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((إِنَّ مما أَدْرَكَ النَّاسُ مِنْ كَلامِ النُّبُوَّةِ الأولَى: إِذا لمْ تَسْتَحِ فاصْنَعْ ما شِئْتَ)) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ  

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Mas’uwd ‘Uqbah bin ‘Amruw Al-Answaariyy Al-Badriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Katika maneno ambayo watu waliyapata kutoka kwa Manabii wa mwanzo (waliotangulia) ni:  Ikiwa huna hayaa basi fanya utakavyo.” [Al-Bukhaariy]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuepushe na kufuata hawaa zetu badala yake tuwe tunafuata mwongozo ambao Yeye Mwenyewe Ametupatia pamoja na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share