Itikadi Potofu (Superstitions)
Itikadi Potofu (Superstitions)
SWALI:
JE inafaa kuamini ishara kama kuwashwa mkono wa kulia unapata pesa au kushoto unatoa na kweli inatoka nk... hii ni katika aina ya shirki au?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hizi ni katika itikadi potofu ambazo zilienea hapo zamani na kuendela kuwepo hadi sasa. Tukitazama tunakuta kuwa hapo zamani kaumu ya Nabiy Swaalih (‘Alayhis Salaam) walimwambia Nabiy wao:
قَالُوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَ ۚ
Wakasema: “Tumepata nuksi kwa sababu yako na kwa wale walio pamoja nawe.” [An-Naml: 47]
Na watu wa Fir’awn pindi walipokumbwa na shida au mitihani walisema:
وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَطَّيَّرُوا بِمُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ ۗ
Na likiwasibu ovu hunasibisha nuksi kwa Muwsaa na walio pamoja naye. [Al-A’raaf: 131]
Waarabu kabla ya Uislamu walikuwa na tabia hizi, nazo ziliondolewa baada ya kuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alizibatilisha.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliweka ukorofi na ukuhani na uchawi katika chungu kimoja pale aliposema:
“Si miongoni mwetu yule mwenye kuona jambo kuwa ni nuksi au kutaka atazamiwe kama jambo fulani ni nuksi, wala mwenye kuagua au kutaka kuaguliwa, wala mwenye kufanya uchawi au kutaka afanyiwe uchawi” [Atw-Twabaraaniy].
Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kupiga ramli kwa kuchora misitari kwenye mchanga kutokana na kuruka kwa ndege na kurusha vijiwe ni ushirikina” [Abu Daawuwd, An-Nasaa’iy na Ibn Hibbaan]
Hivyo, tufahamu kuwa kuamini ishara zikiwa mbaya au nzuri kama kuwashwa mkono huwa unapata pesa, au paka mweusi akikupita mbele yako utapata nuksi ni aina za kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na hivyo ni katika madhambi ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hamghufurii mtu!
Huku kupata kwa ishara iliyokutokea au kupatwa na ikatokea ni katika matendo ya shaytwaan ili uamini kabisa hayo upate kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Tutambue kuwa hakuna linalo kusibu, kukupata au kukutokea pasi na idhini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Yote yanayomfika mja ni katika yale tuliyoandikiwa kama alivyotujulisha hilo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ujue kwamba hakika lenye kukukosa haikuwa ni la kukupata, na la kukupata halikuwa ni lenye kukukosa” [Ahmad].
Na Allaah Aliyetukuka Anasema:
قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴿٥١﴾
Sema: “Halitusibu (lolote) isipokuwa lile Alilotukidhia Allaah. Yeye ni Maulaa wetu.” Basi kwa Allaah watawakali Waumini. [At-Tawbah: 51]
Zifuatazo ni baadhi ya itikadi hizo potofu ambazo zinaaminiwa sana na jamii yetu. Inapasa sote tujiepushe nazo:
1-Jicho likimpiga mtu upande wa kushoto husema ni shari hiyo inakuja!
2-Akimuona mtu paka mweusi basi siku hiyo itakuwa ni ya ukorofi.
3-Mkono umkimuwasha mtu anasema pesa.
4-Ukifagia usiku unaondoa baraka.
5-Akipaliwa mtu husema kuwa mtu anamtaja.
6-Ukikata kucha zote pamoja (ya mikono na miguu) ina maana kwamba shida zikija zitakuja zote pamoja.
Na ziko aina nyingi nyenginezo za itikadi potofu kama hizo ambazo Waislamu wasiokuwa na elimu kuwa ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) huwa wanaziamini.
Tafadhali bonyeza kiungo kifatacho upate elimu na faida zaidi:
21-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Kutabiria Ya Ghayb; Kheri, Shari, Nuksi, Unajimu
Na Allaah Anajua zaidi