Kwenda Kwa Waganga Kujitibu Uchawi Nini Hukmu Yake?

 

Kwenda Kwa Waganga Kujitibu Uchawi Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Asalamu Alaykum,

Moja kati ya mambo yaliyoenea sana katika kanda yetu ya Afrika ya mashariki ni uchawi. Bila ya shaka uharamu wa uchawi unajulikana. Pia tunaelewa kuwa kuna watu ambao kazi yao ni kutibu wale waliofanyiwa uchawi. Mushkila wangu uko katika hawa watu ambao hawafanyi uchawi ila wanagangua. Kwani twaelewa kuwa kabla ya kukupa dawa inabidi kwanza walijue tatizo lako. Nao hutumia njia mbali mbali za kuweza kulijua tatizo kabla ya kulitibu. Naomba unielimishe kama yafaa kwenda kwa watibuji hawa. Na kama yafaa je ni mambo gani twatakiwa tujihadhari nayo tuendapo kwao ili tusije tukawa niwatenda dhambi.

 

Jazakumullahu Khayran.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kwa hakika Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wasallam)  wamekataza uchawi kabisa na wakatuwekea njia ya kujiepusha na uchawi au kukumbwa na mashetani. Zipo ayah ambazo ukisoma zinakulinda na mashetani na pia uchawi na pia zipo du'aa katika suala hilo. Sasa ni bora uwe ukizisoma ili ujilinde. Na miongoni mwazo ni aya kumi za Suwrah Al-Baqarah (Aayah nne za mwanzo, aya 255 – 257 na 284 – 286), Mu'awwadhatayn asubuhi na jioni mara tatu tatu na pia wakati wa kulala (Qul A'udhu birabbin Naas na Qul A'udhu birabbil Falaq).

 

Na zipo tofauti kubwa sana baina ya wachawi na matabibu. Wachawi kawaida watakuwa ni wenye kuangalia kwa kutumia nyota na mbinu nyinginezo na kutaka kafara au ulete vitu Fulani na njia hii haifai kabisa kwa Muislamu kuifuata wala kwenda kwao, kwani mwenye kufanya hivyo basi amemshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na amekanusha yale aliyokuja nao Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wasallam).  Njia ya pili ni kwenda kwa matabibu ambao wanatumia miti shamba wanakupima kama vile anavyopima daktari baada ya hapo atakupatia dawa ambazo mara nyingi ni za kunywa, njia hii haina tatizo bali inashajiishwa na Uislamu. Lakini hawa matabibu huwa hawatibu ugonjwa wa kurogwa kwani hiyo si fani yao. Lakini kwa wakati huu katika miji ya Afrika Mashariki wamejitokeza watu ambao wanasema kuwa ni matabibu lakini wanatumia uganga au uchawi.

 

Wale ambao watakuwa wanatoa uchawi kwa kutumia uchawi wanaingia katika haramu na jambo ambalo limekatazwa kabisa katika sheria yetu kama alivysema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wasallam):

((من أتى كاهناً فصدقه بما يقول فقد كفر بما أنزل على محمد صلى الله عليه وسلم)) [رواه أبو دا

"Atakayemkaribia mchawi na kuamini aliyoambiwa, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad." [Abu Daawud]

((من أتى عرافاً فسأله عن شئ لم تقبل له صلاة أربعين ليلة)) مسلم

"Atakayekwenda kwa mtabiri akamuuliza kitu haitokubaliwa Swalah yake siku arubaini." [Muslim]

 

Hivyo, mtu ambaye anaona kuwa amerogwa anafaa kwenda kwenye 'Ilaaj (matibabu) kwa wacha Allaah waliobobea katika mas-ala ya kutoa uchawi na majini kwa kusoma Qur’an na Adhkaar alizotufundisha Nabiy Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wasallam). Yeyote atakayetumia njia nyengine isiyokuwa hiyo basi atakuwa amefanya madhambi makubwa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share