Kuamini Majini Na Nyota Kuwa Ndizo Zinazoendesha Maisha

 

Kuamini Majini Na Nyota Kuwa Ndizo Zinazoendesha Maisha

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Je Inaswihi Kwa Mtu Anaeamini Kuwa Kutumia Majini Na Kuamini Kuwa Nyota Ndizo Zinazoendesha Maisha Na Kuwashauri Watu Kufanya Hivyo Kupitia Vyombo Vya Habari, Ashauri Mambo Ya Dini Tena Kupitia Ktk Vipindi Vyake Hivyo Au Aitwe Sheikh Au Mtumishi Wa Quruani?                                     

                                                                          

Amani Ya Allaah Iwe Juu Yenu.

 
 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu masuala hayo uliyoyataja. Kama Waislamu tunatakiwa tuamini kuwa majini wapo nao ni viumbe kama binaadamu lakini haifai kuwaabudu wala kuwatumia kwa njia yoyote ile. Wapo watu wanaojidai kuwa wao ni mashekhe na kufanya shughuli hiyo inayokwenda kinyume na Dini ya Uislamu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anaeleza mtihani uliowapata wana wa Israili na baadaye kumsingizia Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis-salaam) kuwa alifanya kazi ya uchawi. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿١٠٢﴾

Na wakafuata yale waliyoyasoma mashaytwaan juu ya ufalme wa Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru. Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah; na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; na kwa yakini walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote, na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao, lau wangelikuwa wanajua. [Al-Baqarah: 102].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anauita utumiaji wa majini kuwa ni kufuru inayomtoa mtu katika Uislamu.

 

Ama kuhusu nyota, ni kiumbe kilichoumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) kuwa na manufaa aina fulani kwa watu. Wala nyota hazikuumbwa kwa ajili ya kuabudiwa wala kutumiwa kuangalilia.

 

Zayd bin Khaalid al-Juhaniy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha Swaalah ya Alfajiri Hudaybiyah baada ya mvua ya usiku. Baada ya kumaliza Swalah, alitugeukia na kusema:

 

"Je, mwajua Rabb wenu Mlezi aliyoteremsha?" Watu wakajibu: "Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi". Akasema: "Allaah Amesema: ‘Asubuhi hii baadhi ya waja Wangu wamebaki Waumini wa kweli na baadhi wengine kuwa makafiri; Yeyote anayesema kuwa mvua imenyesha kwa ajili ya baraka kutoka kwa Rehema ya Allaah Ameniamini na amekanusha nyota, na yeyote aliyesema kuwa mvua imenyesha kwa sababu ya nyota fulani hana Imani na Mimi lakini ameiamini nyota hiyo".  [al-Bukhaariy].

 

Hakika ni kuwa mtu yeyote anayefanya shughuli hiyo anafaa anasihiwe ili arudi katika njia ya haki na hafai kuitwa shekhe kabisa. Wala hatakiwi kupatiwa fursa ya kuweza kuwaidhi watu katika idhaa au runinga (televisheni). Na ikiwezekana mtu kama huyo asusiwe kabisa. Na hao wanaompa nafasi mtu kama huyo, Uislam wao una mashaka sana; ima maslahi ya kidunia wameyaweka mbele kwa kupata vitega uchumi fulani kama anavyofanya huyo anayejiita shekhe kwa kutapeli watu na kula mali zao kwa mwavuli wa Dini, au kuna ile hali ya kuoneleana muhali kwa kuwa kuna maslaha fulani ya kidunia yasiharibike. Kwa kifupi, mtu huyo anayepiga ramli na kutabiria watu mambo yao, ni mtu muovu sana na anamshirikisha Allaah, na hao wanaomwendea pia hawakubaliwi Swalah zao siku arubaini kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Atakayekwenda kwa mtabiri akamuuliza kitu haitokubaliwa Swalah yake siku arubaini"[Muslim]

 

Na ikiwa watamwamini kwa yale anayowatabiria, basi watakuwa wamekufuru kabisa yale aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) kama inavyonyesha Hadiyth hii "Yeyote atakayejimai (kufanya kitendo cha ndoa) na mwanamke mwenye hedhi, au kwa kutumia njia ya nyuma, au kumkaribia mtabiri na kuamini aliyoambiwa, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad". [Hadiyth Sahiyh imesimuliwa na Abu Daawuud, Ibn Maajah, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na wengineo]

 

Soma katika viungo vifuatavyo upate faida zaidi:

 

Mtabiri Wa Nyota Na Kufru Yake

 

Je,Inafaa Kwenda Kwa Waganga Kujitibu Uchawi?

 

Allaah Atulinde na hayo na Awaongoze wote.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share