Wazazi Wangu Wako Kwenye Maasi Na Ushirikina Wa Waganga Na Wanasoma Albadiri (Ahlul-Badr)

 

Wazazi Wangu Wako Kwenye Maasi Na Ushirikina

Wa Waganga Na Wanasoma Albadiri (Ahlul-Badr)

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Bismillah rahman rahiim

Asalaam aleykum,

mimi ni muislam mwezenu naishi na wazazi na wadogo zangu.

Ila nyumbani kwetu kuna mtihani mkubwa yani dada yetu mkubwa anaumwa kipindi kirefu kwa kipindi kirefu tulimpeleka hospital ikashindikana sasa wazazi wamempeleka kwa waganga ambao wanaagiza kuku,mbuzi,kusoma albadir,na kutaka kugeuza kitabu cha Allaah kwa kufru wakati haya yakiindelea mimi nipo chuo nasoma na wakati mwingine narudi nyumbani lakini roho ilikuwa inaniuma mno nikiambiwa maneno hayo. Sasa ikafika wakati mgonwa haponi na wazazi wanasema lazima tuwepo wote kwenye tiba hiyo, mimi nikasema sitashiriki mpaka apatikane mtu wa anayetumia ruqya pekee, kutokana na hivyo basi nashangaa wazazi wanaaza kuwa maaadui na mashaka na mimi mpaka wanafikia kusema niache kuswali nitachanganyikiwa nikiendelea.Wazazi wangu hawasalibaba yeye hadi pombe na mungu kamjaliia kifedha lakini anatumia madaraka yake vibaya. Mimi nimeomba dua sana nisigombane nao,warejee kwa Allaah,tutubu zambi lakini sheikh bado ndio chuki inazidi ikipungua kidogo sana mpaka mimi imani yangu najihisi inaudhoohofu kwa Allaah(s.w) yaani sielewi.

Sheik kwa elimu aliowapa Allaah (s.w) na maarifa mazuri naombeni mnishauri cha kufanya nisije nikakosa radhi za Allaah (s.w).

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Haya nayo ni baadhi ya matatizo ya kijamii ambayo hujitokeza pindi nyumba ikikosa mwelekeo wa kidini. Ikiwa maadili ya wazazi si ya Kiislamu basi matatizo kama haya hutoa kichwa chao nje na huleta mvurugano hasa kukiwa na mtoto ambaye anataka kushika na kutekeleza mas-ala ya Kidini ndani ya nyumba hiyo. Mitihani yake inakuwa mingi kwani anavutwa na jamii yake kuingia katika maasiya na kuacha uchaji Allaah.

 

Hii inakwenda sambamba na Sunnah (mipango/kanuni) za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika huu ulimwengu, nazo huwa hazibadiliki. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٦٢﴾

Ni desturi ya Allaah kwa wale waliopita kabla. Na wala hutopata mabadiliko katika desturi ya Allaah. [Al-Ahzaab: 62].

 

Pia,

..فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ ۚ فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَحْوِيلًا ﴿٤٣﴾

Je, basi wanangojea nini isipokuwa desturi ya watu wa awali. Basi hutapata katika desturi ya Allaah mabadiliko, na wala hutapata katika desturi ya Allaah mageuko. [Faatwir: 43].

 

Tufahamu kuwa katika Sunnah za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni kuwapatia waja wake mitihani. Mitihani hiyo inakuwa kulingana na Imani ya mja mwenyewe.

Wenye mitihani mikubwa na mizito ni Rusuli na Manabii (‘Alayhimus-salaam) na wale walio chini yao. Kati ya mitihani ni mtu kuwa mgonjwa au jamaa yake wa karibu sana kuwa katika hali hiyo ya ugonjwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatueleza wale waliotetemeshwa kwa mitihani mikubwa pale Aliposema:

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم ۖ مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ وَزُلْزِلُوا حَتَّىٰ يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ اللَّـهِ ۗ أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّـهِ قَرِيبٌ ﴿٢١٤﴾

Je, mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali bado haijakufikieni (mitihani) kama ya wale waliopita kabla yenu? Iliwagusa dhiki za umasikini na maafa ya magonjwa na njaa na wakatetemeshwa mpaka Rasuli na wale walioamini pamoja naye wanasema: Lini itafika nusura ya Allaah? Tanabahi! Hakika nusura ya Allaah iko karibu. [Al-Baqarah: 214].

 

Pia tusidhani kuwa kwa kusema kwetu tumeamini tutaachiliwa tu hivi bila kutiwa katika mitihani. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ ﴿٢﴾وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ ﴿٣﴾

Je, wanadhani watu kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao ndio wasijaribiwe? Kwa yakini Tuliwajaribu wale wa kabla yao, ili Allaah Awatambulishe wale walio wakweli na ili Awatambulishe walio waongo. [Al-'Ankabuwt: 2 – 3].

 

Mitihani ipo mingi kama alivyotaja Aliyetukuka:

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri. [Al-Baqarah: 155].

 

Mtu anapotahiniwa ni wajibu wake kuwa mwenye subira, imara na kutoyumbayumba na kutoka katika maadili na muruwa wa Kiislamu. Ni makosa makubwa kwa Muislamu kuingia katika shirki pindi anapotiwa katika misukosuko. Shirki kubwa inamtia mwenye kuifanya daima Motoni nayo ni kwenda kwa wachawi wanaomuagizia kuchinja kuku, mbuzi na kadhalika. Na yote hayo ni udangayifu wa hali ya juu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuhusu jambo hilo kuwa ni dhulma:

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno! [Luqmaan: 13].

 

Ovu hilo linamfanya mtu asisamehewe madhambi yake:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ 

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae.  [An-Nisaa: 48, 116].

 

Waislamu wengi wasioelewa Dini yao wanatishwa na kutishika kwa kusikia neno hilo lakini hata hawashtuki wala kujali pindi wanaposikia jina la Allaah, Jalla Jalaaluh. Hilo ni kosa na shirki kwani albadir ni neno la Kiarabu lililopotoshwa maana yake na makusudio, kwani usawa ni Ahlul Badr (watu wa Badr). Katika kisomo hicho kunasomwa majina 313 – 319 ya wale Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walioshiriki katika vita baina yao (Waislamu) na makafiri wa kutoka Makkah. Kuyatumia majina hayo kuomba kwayo au kumlaania mtu ni shirki na haifai Muislamu kufanya hilo.

 

Hakika ni kuwa Muislamu anapopatwa na tatizo au shida anatakiwa amuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), Naye Atamuondolea tatizo lake au matatizo yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ ﴿٧٨﴾وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ ﴿٧٩﴾وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

Ambaye Ameniumba, Naye Ananiongoza. Na Ambaye Ndiye Anayenilisha na Ananinywesha. Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha. [Ash-Shu'araa: 78 – 80].

 

Muislamu mwenye Imani thabiti ni lazima ahisi vibaya kwa kuambiwa maneno kama hayo uliyoambiwa miongoni mwa kauli za shirki. Hiyo ni dalili kuwa Alhamdullillah Imani yako ni hali ya juu lakini inatusikitisha kusikia kutoka kwako kuwa Imani hiyo imeanza kupungua na kudhoofu kwa sababu ya kutaka kuwaridhisha wazazi wako.

 

Ni muhimu kuelewa kuwa ni muhimu sana kwa mtoto kuwatii wazee wake kama alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ 

Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. [Al-Israa: 23].

 

Hata hivyo, inatakiwa tufahamu kuwa twaa hiyo inakuja baada ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haifai kuwafuata katika kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Anasema Aliyetukuka:

وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ 

Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Na suhubiana nao kwa wema duniani. [Luqmaan: 15].

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakuna twaa kwa viumbe katika kumuasi Muumba".

 

Kwa hiyo, haifai kabisa kuwatii kwa wanayoyataka kwani yanakwenda kinyume na kanuni za Kiislamu, katika kutekeleza hilo ni lazima usimame wima na uwe imara kabisa. Kwa kuwa jamaa zako wanakushurutisha kufanya maasiya ni mtihani mkubwa. Ndugu yetu katika Imani! Tambua kuwa haupo peke yako kwani Waislamu waliopita walipata mitihani mikubwa zaidi. Pia tunapata wengine katika wakati wetu huu waliofikiwa na zaidi ya hayo lakini walivumulia katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mpaka faraja ikaja kwao. Kwa hiyo, watu hao walifanikiwa kupita mtihani wao huo. Tazama jinsi gani Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alivyosumbuliwa na Mayahudi:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا ۚ وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا ﴿٦٩﴾

Enyi walioamini! Msiwe kama wale waliomuudhi Muwsaa, lakini Allaah Akamtoa tuhumani kutokana na yale waliyoyasema. Na alikuwa mbele ya Allaah mwenye kuheshimika. [Al-Ahzaab: 69].

 

Jukumu lako wewe ni kuendelea kuzungumza na jamaa zako pamoja na wazazi wako kwa hekima huenda wakaongoka na usikate tamaa kwa hilo. Jaribu kutumia Mashaykh na wazee wenye busara wazungumze na babako kuhusu madhara kwake kwa kunywa pombe na pia kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), huenda akabadilika. Hiyo ni kuwa mwenye kuongoza ni Allaah aliyetukuka nasi hatuwezi kumuongoa tumtakaye. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿٥٦﴾

Hakika wewe huwezi kumhidi umpendaye; lakini Allaah Humhidi Amtakaye, Naye Anawajua zaidi wenye kuongoka. [Al-Qaswasw: 56].

 

Kuomba du’aa ni miongoni mwa Ibaadah kubwa kwa Muislamu kuitekeleza. Lakini hufai wewe kumwekea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) muda wa Yeye kukujibu maombi yako. Kusema kwako kuwa umeomba sana du’aa unamaanisha nini? Je, unaona kuwa ukiomba kwa muda fulani ni lazima uone tija yake au vipi? Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametoa ahadi kuwa Atatujibu maombi yetu lakini kwa njia ambayo Anaiona kuwa ni maslahi kwako hapa duniani na Kesho Aakhirah. Mwanachuoni mmoja amesema kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anamjibu mja Wake kwa maombi yake kwa njia zifuatazo:

 

1.    Kumjibu alivyotaka hapa hapa duniani kwa haraka sana.

2.    Kumbadilishia alichotaka kwa kizuri zaidi.

3.    Kumpatia alichotaka Kesho Aakhirah.

 

Kwa hiyo, wewe usiweke sharti katika kujibiwa kwako na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani ndiye Mjuzi wa yote hayo uyatakayo na ni juu yako kuendelea kuomba kwani Yeye Amesema:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186].

 

Na ile kauli yako kuwa watu wanazidi kukuchukia kwa sababu ya kufanya kwako Ibaadah si lolote wala chochote kwani hiyo ni dalili ya ima kuzidi mtihani au kupungua. Mara nyingi mtihani unapokuwa mkubwa nawe ukaweza kuvumilia na kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), Yeye Hukutolea njia kwa tatizo hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا

Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani).[Atw-Twalaaq: 2].

 

Na pia,

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ

Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. [Atw-Twalaaq: 3].

 

Tufahamu kuwa mitihani ni aina nyingi kama tulivyotaja hapo awali na mojawapo ni kupigwa vita na jamaa zako wa karibu kwa misimamo yako ya Kidini na Imani yako.

 

Ni mapema sana kwako kufa moyo. Tutambue kuwa hiyo si sifa ya Muislamu kwa kuwa anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ

.....Hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri. [Yuwsuf: 87].

 

Inafaa ushikilie kabisa kanuni za Dini na ukitofanya hivyo hasara itakuwa kwako hapa duniani na Kesho Akhera. Zama na nyakati hubadilika sana, hupata wakati mmoja ukiwa katika ufanisi na mwingine ukiwa katika janga na matatizo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 إِن يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِّثْلُهُ ۚ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَتَّخِذَ مِنكُمْ شُهَدَاءَ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ ﴿١٤٠﴾

Inapokuguseni majeraha basi yamekwisha wagusa watu majeraha kama hayo. Na hizo ni siku Tunazizungusha zamu (za mabadiliko ya hali) baina ya watu na ili Allaah Adhihirishe waloamini na Afanye miongoni mwenu mashahidi. Na Allaah Hapendi madhalimu. [Aal: 'Imraan: 140).

 

Ni dhahiri kuwa hakuna dhiki wakati wote kwani baada ya dhiki ni faraja. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٦﴾

Hakika pamoja na kila ugumu kuna wepesi. [Ash-Sharh: 6].

 

Huu si wakati wa kwako kudhoofu Ki-Imani mbali na matatizo bali ni wakati wa kuzidisha ili uweze kupambana vilivyo na mitihani inayokukabili.

 

Njia nzuri kabisa ya kukabiliana ni kutaka msaada wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa subira na kwa kusimamisha Swaalah:

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45].

 

Pia inatakiwa tuwe watiifu zaidi katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni hakika kuwa Imani hupanda (huzidi) kwa twaa na hupomoka kwa maasiya. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣﴾

Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan, na kwa Rabb wao wanatawakali. Ambao wanasimamisha Swalaah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa. [Al-Anfaal: 2-3].

 

Kwa kutekeleza hayo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atakusaidia na InshaAllaah utaweza kuipita mitihani hiyo. Kuwa imara na usife moyo kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) yu pamoja nawe. Nasi ndugu zako tunakuombea at-taawfiyq katika mambo yako.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share