Haifai Kutoa Mkono Kuamkiana Wanawake na Wanaume

 

Haifai Kutoa Mkono Kuamkiana Wanawake na Wanaume

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Asalaam aleikum.tafadhali ningependa munieleze kwa urefu vile Nabiy alivyofanya baiy kwa wanawake.yasemekana mtume alimwambia umar awape mikono hawa wanawake, je rai ni ya ukweli?

 

Jibu:

 
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  
 

Hili ni swali zuri na mara haswa wanaoishi katika nchi zilizo na wasiokuwa Waislamu huwa wanaona hayaa kusema kuhusu kutopeana mkono na jinsiya tofauti.

 

Ni maombi ya muulizaji kuwa swali hili lielezwe kwa urefu lakini jibu lake si refu hivyo isipokuwa tutataja Hadiyth kadhaa ili suala hilo wazi.

 

Uislamu umeweka kanuni ya uharamu kwa mwanamume kuugusa mwili wa mwanamke na kinyume chake. Hili ni kwa mujibu wa Hadiyth zifuatazo:

 

  • Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mwenye kuugusa mkono wa mwanamke bila ya kuwa na uhusiano wa kisheria naye (mahram yake), ataekewa kaa la moto kwenye kitanga chake cha mkono Siku ya Qiyaamah" [Fat-hul Qadiyr].

 

  • Mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema kuwa:  "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikubali Bay‘ah ya wanawake kwa mdomo tu bila kushikana mikono. Hakika hakugusa mkono wa mwanamke ambaye si mkewe. [Al-Bukhaariy]

 

  • Umaymah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema alikwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa pamoja na wanawake wenziwe ili kutoa Bay‘ah. (Nabiy) Aliwataka waahidi kuwa hawatamshirikisha Allaah, hawataiba, hawatazini, hawatakashifu wala kuzua uongo na kumuasi Nabiy. Baada ya Bay‘ah, walimuomba achukue mikono kama ishara ya utii. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Mimi sipokei mkono wa wanawake, makubaliano ya mdomo yanatosha” [an-Nasaaiy na Ibn Maajah].

 

Hii ni Hadiyth inayotufunza kuwa hili suala la kutopeana mikono ni kwa kila anayefuata Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) japokuwa hasa ni kwake.

 

Ni wazi kuwa katika Baiyah ya kwanza, waliyomuahidi kwayo Answaar waliokuwa wanaume watupu inajulikana katika Siyrah kama Bay‘ah ya kike kwani walitakiwa waahidi kama yale ya wanawake waliokuja baadaye, tofauti yake ni kuwa wanaume walimpatia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mikono yao. Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا جَاءَكَ الْمُؤْمِنَاتُ يُبَايِعْنَكَ عَلَىٰ أَن لَّا يُشْرِكْنَ بِاللَّـهِ شَيْئًا وَلَا يَسْرِقْنَ وَلَا يَزْنِينَ وَلَا يَقْتُلْنَ أَوْلَادَهُنَّ وَلَا يَأْتِينَ بِبُهْتَانٍ يَفْتَرِينَهُ بَيْنَ أَيْدِيهِنَّ وَأَرْجُلِهِنَّ وَلَا يَعْصِينَكَ فِي مَعْرُوفٍ ۙ فَبَايِعْهُنَّ وَاسْتَغْفِرْ لَهُنَّ اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾

12. Ee Nabiy! Wakikujia Waumini wa kike wanafungamana nawe ahadi ya utiifu kwamba hawatomshirikisha Allaah na chochote, na wala hawatoiba, na wala hawatozini, na wala hawataua watoto wao, na wala hawatoleta usingiziaji wa kashfa walioizua baina ya mikono yao na miguu yao na wala hawatakuasi katika mema; basi pokea ahadi yao ya utiifu, na waombee maghfirah kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Mumtahinah: 12]

 

Ni wazi kuwa jambo alilolikataza mwenyewe Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawezi kumuamrisha ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alifanye. Ikiwa labda umesoma kitabu kinachosema hivyo au una Hadiyth kuhusu hilo basi unaweza kututumia nasi tukaingalia hiyo kwa makini na kuihakikisha usahihi wake In shaa Allaah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.
 
Share