Zingatio: Amka: (Maafa Yaliyotokea Mwaka 2007)

 

Zingatio: Amka (Maafa Yaliyotokea Mwaka 2007)

 

Na: Naaswir Haamid

 

 

 Alhidaaya.com

 

  

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema “Qiyaamah hakitosimama mpaka mitetemeko ya ardhi izidi”. [Al-Bukhaariy]

 

 

Mengi yameandikwa, mengi tumeyasoma, mengi tumeyasikia. Je, haujafika wakati wa kuamka na kuyazingatia yale ya kutusaidia Siku ya Mwisho? Haijawa bado funzo kwetu kama Qiyama kipo chini ya pua zetu kinasubiri amri tu kije kwetu. Dalili ngapi tushaziona? Dalili ngapi tushazishuhudia? Twasubiri hadi milango ya toba ifungwe ndio turudi kwa Rabb wetu? SubhaanaAllaah!

 

 

Ya Sunami hatuyaoni? yaliyowapata watu Duniani, hadi tukawa mashakani, bado tunamuasi Manani? Tumegeuka ashaddu wa kumuasi ar-Rahmaani, hadi kuwa sawa na nyani?  

 

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ لَهُمْ قُلُوبٌ لَّا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَّا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَّا يَسْمَعُونَ بِهَا ۚ أُولَـٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ ﴿١٧٩﴾

 

179. Kwa yakini Tumeumba Jahannam kwa ajili ya wengi katika majini na wana Aadam. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama, bali wao ni wapotovu zaidi. Hao ndio walioghafilika. [Al-A’araaf: 179]

 

 

Basi kama ndugu yangu Muislamu unazo nyoyo, fahamu umepewa na macho ya kusoma ukaekewa. Nakunasihi uyazingatie haya machache tu yaliyotokea kwa mwaka huu wa 2007.

 

 

Tarehe

Sababu

Eneo

Idadi Waliofariki

 

 

01/01/07

Ndege iliyokuwa inatoka Java kwenda Manado ilikumbwa na upepo mkali

 

Indonesia

watu 102

02/02/07

Kimbunga

Florida-Marekani

 

watu 20

19/03/07

Mlipuko wa machimbo ya makaa ya mawe

 

Urusi

watu 110

01/04/07

Mtetemeko wa ardhi uliwacha maelfu ya watu bila ya makazi na kuuwa

 

Honiara kwenye Visiwa vya Solomons

 

watu 34

05/05/07

Ndege ya Kenya kuanguka kutokana na hali mbaya ya hewa

 

Cameron

abiria wote

24/06/07

Kutokana na upepo na mkali

 

Pakistan

watu zaidi ya 200

17/07/07

Ndege iliyoruka kutoka Uwanja wa ndege ilianguka kutokana na mvua kali

 

Congonhas

abiria 176

 

 

Tena tutambue haya yote na mengine yanayotokea Allaah Amekwishayaandika na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwishabainisha kuwa maafa yatakuwa ni mengi karibu na Qiyaamah: Saa haitosimama hadi elimu ifutwe, wakati kukimbia kwa kasi, mitetemeko kuzidi kwa sana, fitna kutokea na al-Harj kuengezeka.” Ikaulizwa, “Ee Rasuli wa Allaah, nini hiyo al-Harj?” Akasema, Al Qatl, al Qatl (mauaji). [Imepokewa na Imaam Ahmad]

 

 

Kwa hakika uharibifu umedhihiri barani na baharini kwa sababu ya maovu yetu Binaadamu. Na Allaah Anatuonjesha baadhi ya tuliyoyafanya ili tutanabahi na kurudi.  

  

ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٤١﴾

 

41. Ufisadi umedhihiri katika nchi kavu na baharini kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono ya watu ili (Allaah) Awaonjeshe baadhi ya waliyoyatenda ili wapate kurejea. [Ar-Ruwm:41]

 

 

 

Nakunasihi Muislamu kwa mara nyengine tena,

Ghadhabu za Allaah jitahidi kuepukana,

Usije ukatufanya sisi pia maafa kukutana,

Hadi Rabb wetu Mtukufu Mkubwa Subhaanah,

Msamaha Kwake Qiyaamah tukawa hatuna.

 

Share