Tashahhud: Wakati Unaotakiwa Kuanza Kutikisa Kidole Katika Tashahhud

 

SWALI:

 

 

 

Asalam Aleikum.

Baada ya kumshukuru Allaah s.w na kumtakia Rehma Mtume s.a.w.Suali langu ni kuhusu kutingisha kidole kwenye Atahiyatu.Sharti yake ni vipi?Nikuanzia unapo anza atahiyatu mpaka mwisho au unaposema shahada au unakinyosha tu kidole lakini hautingishi?

shukran

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ushahidi wa Hadiyth iliyopokelewa na Muslim, Abu ‘Awaanah na Ibn Khuzaymah unaonyesha kuwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akikaa kwenye tashahhud alitandaza mkono wake wa kushoto juu ya goti lake la kushoto, akikunja vidole vyake vya mkono wa kulia, akiashiria kidole chake cha karibu na gumba (kidole cha shahada) na huku akikielekeza Qiblah, na huku akielekeza macho yake hapo (kwenye kidole hicho).

 

Hivyo mwenye kuswali anaweza kuanza kutikisa kidole tokea mwanzo wa tashahhud. Au akakitikisa katika maeneo ya du'aa ndani ya tashahhud kama wanavyoeleza Wanachuoni kama Imaam Ibn 'Uthaymiyn na wengine.

Ama kukiendeleza kukitikisa imepatikana dalili kwamba akifanya hivyo kama ulivyokuja usimulizi ufuatao:

 

عن وائل بن حجر‏:‏  "أن رسول اللَّه صلى اللَّه عليه وآله وسلم  رفع إصبعه فرأيته يحركها يدعو بها"‏ - أبو داود والنسائي

Imepokewa na Waail bin Hujr kwamba, “Hakika (Mtume) (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinyanyua kidole chake (katika Tahiyaatu) na nikamuona akikitikisa, na akiomba kwacho.” [imekusanywa na Abu Daawuud na An-Nasaaiy].

 

Hata hivyo, kuna Wanachuoni walioiona Hadiyth hii kuwa ni dhaifu kutokana na mmoja wa wasimulizi katika mnyororo wa wasimulizi. 

 

Kuhusu 'kuomba du'aa nacho', Imaam At-Twahaawiy amesema: "Hii ni dalili kwamba ilikuwa ni mwisho wa Swalah". Hivyo kuna dalili kwamba Sunnah ni kuendeleza kukielekeza na kukitikisa hadi katika tasliym (wakati wa kutoa Salaam), kwani du'aa huwa hadi hapo. Hii ni rai ya Maalik na wengineo. - Swiffatus-Swalah, Shaykh Al-Albaaniy].

 

Kwa maelezo zaidi soma Swali na Jibu katika kiungo kifuatacho:

 

 

Hikma Ya Kutikisa Kidole Katika Tashahhud

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share