Ghiybah (Kusengenya) Katika Mwezi wa Ramadhwaan Nini Hukmu Yake

SWALI:

 

sheikh, swali langu ni kama mtu ameteta na wewe lakini wewe nia yako sio yakuteta sasa ramdhan utafanya nini kufanya saumu yako kamili?

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Muislamu anapofunga (Swawm) inampasa azingatie kwamba haina maana kujizuia kula na kunywa pekee bali pia kujizuia na kila aina ya maovu na maasi. Kufanya hivi ni kujibakisha katika lengo la Swawm lililokusudiwa nalo ni kuwa na Taqwaa (ucha Mungu) kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ))  

((Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama waliyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah)) [Al-Baqarah: 183]

Maana ya Swawm kilugha ni kujizuilia. Inaweza kuwa ni kujizuia jambo lolote la kawaida mtu alilolizoea kulifanya. Maryam ('Alyhas-Salaam) aliambiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa ajizuie kuzungumza baada ya kumzaa Nabii 'Iysa ('Alyahis-Salaam)

((فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا))

((Na kama ukimuona mtu yoyote (akauliza habari za mtoto huyu) sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa Rehma, ya kufunga, kwa hiyo leo sitasema na mtu)) [Maryam 19:26]

Maana ya Swawm kisheria ni kujizuilia kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), kula, kunywa, kuvuta sigara, kuingiza kitu chochote katika matundu mengine mawili kama vile pua na masikio, kujizuia na kujamii, kujitoa manii kwa makusudi au kwa matamanio na kujizuia kujitapisha kwa kipindi cha kati ya Afajiri ya kweli mpaka kuingia Magharibi. 

Muislamu anapoingia katika Swawm anaingia katika madrasa yenye faida na manufaa mengi kwake. Inahitaji subira kubwa ya kila aina, subira ya kujizuia njaa na kiu, subira ya kufanya ibada vizuri ipasavyo na subira ya kujiepusha na maasi na maovu yote ambayo viungo vya mwili vinaweza kutenda. Maovu ya ulimi ambayo ni kusengenya, kusema uongo, kuropokwa ovyo n.k. yanapaswa kabisa kujiepusha nayo. Kusengenya ni maovu mabaya kabisa na hatari mja kuyatenda kwani humpunguzia thawabu na kumpatia dhambi mja. Kwa hiyo ibada anayoifanya huwa na upungufu mkubwa au hata pengine yote isiwe na thamani kwa kutegemea wingi wa thawabu kupunguzwa na dhambi kuchuma. Inapasa kutahadhari sana na maovu hayo na mengineyo ya ulimi kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhadharisha:

 

 عن أبي هريرة رضي الله عنه، قال قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((من لم يدع قول الزور والعمل به، فليس لله حاجة في أن يدع طعامه وشرابه)) البخاري

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yule ambaye haachi kusema uongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allaah Hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake (yaani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)    Hana haja na funga yake)) [al-Bukhaariy]

 

 

Kwa hiyo inampasa Muislamu khaswa mwenye kufunga ajizuie na kujipeusha kabisa na maovu haya ya kusengenya ili abakie salama katika vitendo vya ibada zake na Swawm yake pia na badala yake ashughulishe ulimi wake kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kila aina ya dhikr, tasibyh, tahliyl, tahmiyd, takbiyr, kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) n.k.

 

 

Ingia katika kiungo kifuatacho usome mfululizo wa mada za 'Madhara ya Kusengenya' ili utanabahi hatari zake:

 

 

 Madhara ya Ghiybah

 

Swawm ya mwenye kusengenya itahesabika kuwa ni Swawm na haina haja ya kuikidhi ila tu itakuwa ameifisidi na kuiharibu kwa kuipunguzia thawabu zake na kujiongezea dhambi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share